Miradi miwili ilivyomgonga kichwa Samia

Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya usambazaji umeme vijijini kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Hassan Saidy (wa pili kulia), Mwanasheria wa REA, Mussa Muze (kulia) na watendaji wa kampuni ya ukandarasi katika hafla iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam Jumanne, Februari, 2023. Picha na Ericky Boniphace
Muktasari:
- Rais Samia alisema wingi wa fedha za ujenzi wa miradi ya Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP) na Reli ya Kisasa (SGR) ulimtisha mwanzoni lakini sasa anaona ujenzi wake unakwenda vizuri, wachumi waeleza zinakotoka.
Dar es Salaam. Wakati akikaribia miaka miwili madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza siri jinsi miradi ya Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP) na Reli ya Kisasa (SGR) ilivyomuumiza kichwa mara baada ya kuapishwa.
Hofu kuhusu miradi hiyo ilitokana na kutojua wapi angepata fedha za kukamilisha utekelezwaji wake.
Mkuu huyo wa nchi alipoapishwa Machi 19, 2021, mradi wa JHPP unaotekelezwa kwa Sh6.5 trilioni, ulikuwa umefikia asilimia 50 na sasa umefikia asilimia 80 ukitarajiwa kukamilika na kuanza kwa majaribio mwakani.
Wakati ule anaingia madarakani, mradi wa SGR kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro (Kilometa 202) kilikuwa asilimia 90 wakati kile cha Morogoro -Makutopora (Kilometa 348) kilikuwa asilimia 50.
Kwa sasa kipande cha Dar -Moro ujenzi wake umekamilika na Moro - Makutopora kimefikia zaidi ya asilimia 82.
Rais Samia alieleza siri hiyo juzi katika hotuba yake kwenye hafla ya utiaji saini wa mkataba wa uimarishaji wa gridi ya Taifa, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Mliponikabidhi dhamana hii, kitu kilichoniumiza kichwa sana sana ilikuwa ni mradi wa bwawa na mradi wa SGR, kila nikiangalia mapesa yanayohitajika nasema Mungu wangu, Samia nitapata wapi pesa hizi.
“Lakini kwenye nia pana njia, leo SGR nina pesa hadi kipande cha sita kufika Kigoma, lakini kwa bwawa nadhani mwakani tutakwenda kuliwasha, tutaanza kukusanya umeme wa awali,” alisema Rais Samia.
Hii si mara ya kwanza kwa mkuu huyo wa nchi kutaja miradi ya kimkakati kama jambo lililompa hofu zaidi baada ya kuapishwa, baada ya kufanya hivyo katika maadhimisho ya siku 100 madarakani.
Kinachofanya ajiamini na kuwa na uhakika wa fedha za miradi hiyo na mingine mipya, ni mbinu alizozitengeneza za kukusanya fedha kutoka ndani na nje ya nchi kama inavyoelezwa na Profesa Francis Matambalya, mtaalamu wa uchumi na biashara.
Profesa Matambalya alisema tangu alipoingia madarakani, Rais Samia aliandaa vyanzo mbalimbali vinavyomwezesha kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo.
“Amehakikisha anatengeneza mazingira mazuri na wawekezaji kutoka ndani na nje, ameweka ruzuku na tozo mbalimbali, zote hizi zote zimemwezesha kupata fedha ndiyo maana anajiamini sasa,” alisema.
Profesa Matambalya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (NMF), alisema pia mtindo wa mkuu huyo wa nchi wa kutumia rasilimali za nje kupata fedha zinaongeza na kuharakisha upatikanaji wake ukilinganisha na kutegemea vyanzo vya ndani pekee.
Mtazamo huo unafanana na wa Dk Timoth Lyanga, mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), aliyesema uimarishaji wa vyanzo vya mapato ndiyo msingi wa kujiamini kwake.
Tangu alipoingia madarakani, Rais Samia amekuwa akisimamia ukusanyaji wa mapato na hilo limedhihirika katika taarifa za makusanyo ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).
Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/23 TRA imekusanya Sh12.4 trilioni sawa na asilimia 99 ya lengo la makusanyo ya Sh12.48 trilioni.
Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la Sh1.35 trilioni ikilinganishwa na Sh11.11 trilioni zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka wa Fedha 2021/22.
“Hofu ni kawaida unapopewa jukumu jipya, lakini alichokifanya ni kusimamia misingi iliyomwezesha kupata fedha na kuanzisha misingi mipya ambayo hadi sasa inawezesha kupatikana fedha za kutekeleza miradi mbalimbali,” alisema Dk Lyanga.
Mikakati mingine ya upatikanaji wa fedha ni kupitia mikopo na misaada mbalimbali.
Utangazaji zabuni
Katika hotuba yake, Rais Samia alizungumzia zabuni akizitaka mamlaka za udhibiti zipime tuhuma zinazowasilishwa wakati wa utangazwaji wa zabuni kwa ajili ya kupata wakandarasi wa kutekeleza miradi.
Alisema baadhi ya watu hupeleka tuhuma kwa sababu tu waliowatarajia wapate tenda hizo wamekosa.
“Niwaombe sana ndani ya Serikali, mamlaka za udhibiti pimeni mnayoletewa msiturudishe nyuma kwa kipengele kwamba sheria inaruhusu kwenda PPRA miezi mitatu,” alisema.
Rais Samia alisema anatambua uwepo wa baadhi ya watu wenye tabia ya kwenda katika mamlaka hizo wanapoona waliopanga wapate zabuni hizo wamekosa.
“Kwa sababu natambua wenzetu wengi kila mtu alikuwa na mkandarasi wake mkononi na alipenda apate na kwa sababu hakupata fitina zinakuwa nyingi, mbio PPRA, PCCB, sijui wapi, nenda ule mradi usifanyike kwa matakwa yake binafsi,” alisema akisisitiza kuwa ili miradi hiyo ikamilike kwa haraka, maamuzi ya haraka yanahitajika.
Alizihusisha fitina hizo na urasimu katika utoaji wa vibali vya ajira za utekelezwaji wa miradi, akisema pamoja na baadhi ya mashirika kuhitaji haraka wafanyakazi, mamlaka zimekuwa zikichelewesha kwa karibu mwaka mmoja.
“Kama wanataka wafanyakazi mishahara ya kulipa wanayo haitoki kwenye mfuko wa Serikali wapewe ruhusa wafanye, sababu ajira hizi wala nyingine si za kudumu.
Aliwataka wakuu wa mashirika kuchukua hatua dhidi ya watendaji wasioendana na kasi ya miradi hiyo huku akionya watendaji nao kuacha kulalamika.