Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika yapoteza Sh216.8 trilioni kwa ufisadi

Seynabou Diakhate, ambaye ni mwenyekiti anayemaliza muda wake katika Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika ya Kupinga Rushwa ( AUABC), akizungumza leo katika makao makuu ya bodi hiyo jijini Arusha wakati wa kikao cha kawaida cha 49 kilichoenda sambamba na kuapisha wajumbe wapya wa bodi hiyo.

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya Umoja wa Afrika ya Kupinga Rushwa (AUABC), Yvonne  Mutepuka amesema kutokana na vitendo hivyo nchi za Afrika zinaweza kulazimika kukopa IMF na WB katika kutatua changamoto za kiuchumi na kukuza maendeleo.

Arusha. Licha ya juhudi za mapambano dhidi ya rushwa barani Afrika, nchi za Afrika zinakadiriwa  kupoteza kati ya Dola za Marekani 20 hadi 80 bilioni (Sh216.8 trilioni) mwaka kutokana na ufisadi.

Kutokana na changamoto hizo nchi hizo huenda zikalazimika kukopa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) kujaribu kutatua changamoto za kiuchumi na kukuza maendeleo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Juni 17, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika ya Kupinga Rushwa (AUABC), Yvonne Mutepuka, alipokuwa akizungumza katika kikao cha kawaida cha 49 cha bodi hiyo.

Kikao hicho kilikwenda sambamba na kuwaapisha wajumbe wapya wa bodi hiyo katika makao makuu yake yaliyopo jijini Arusha.

Amesema kuwa kutokana na sababu hiyo bodi ya AUABC ni muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa ili kuhamasisha nchi wanachama kuwa na sheria nzuri zinazozuia vitendo vya rushwa.

"Kwa hivyo bodi hii ya ushauri dhidi ya ufisadi ni muhimu na kama mnavyojua Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kupambana na Kuzuia Rushwa ndio mfumo unaoweka wazi kile tunachopaswa kufanywa, na kimsingi, tunapaswa kuhimiza nchi wanachama kuwa na aina ya sheria inayozuia rushwa," amesema.

"Ndani ya AUABC kuna sheria ambazo nchi zote wanachama zinatakiwa kuwa na mchakato huo na zinazitaka kusaini kwanza kwenye mkataba kisha kuridhia mkataba na kupitisha sheria na mifumo ya kisheria itakayohakikisha kuwa nchi zao zinaweza kupambana na rushwa."

Mjumbe huyo amesema kuwa wanaendelea kuimarisha mapambano na kuhimiza nchi kuangalia masuala ya mtiririko wa fedha, utajiri haramu na kuangalia suala la kurejesha mali.

Mwenyekiti wa AUABC aliyemaliza muda wake, Seynabou Diakhate amesema kati ya nchi 54 za bara la Afrika nchi 50 zimesaini Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Aidha amewataka wajumbe hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa ajili ya Afrika kwa kupambana na rushwa licha ya kazi hiyo kuwa ngumu.

Amesema wanaendelea na uhamasishaji wa nchi zilizosalia ili ziweze kusaini mkataba huo na kuwa wanaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika kupambana na rushwa kwani ni vita inayohitaji ushirikiano. Hali ilivyo nchini Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu kesi za ufisadi nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyotolewa Machi, 2025 ilionyesha kulikuwa na jumla ya kesi 978 za rushwa. Kati ya hizo 462 zilikuwa mpya zilizofunguliwa mwaka huo, na 516 zilikuwa za zamani zilizokuwa zikiendelea katika mahakama mbalimbali nchini. Takukuru ilishinda kesi 334 kati ya 440 zilizokamilika, ikiwa ni kiwango cha mafanikio cha asilimia 76, kilichoongezeka kutoka asilimia 67.7 mwaka uliopita.

Aidha, Takukuru ilifungua kesi 281 zinazohusiana na wizi wa fedha za Serikali kupitia mifumo ya kielektroniki, hasa mashine za POS. Kati ya hizo, kesi 73 zilitolewa hukumu, na jumla ya Sh6.2 bilioni zilizorejeshwa serikalini.

Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca). lilishughulikia kesi 289, na kuokoa mamilioni ya dola za Marekani kutokana na udanganyifu wa kifedha .

Katika kikao hicho wajumbe walioapishwa ni pamoja na Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo kutoka nchini Ghana, Edem Senanu, Benjamin Kapera (Tanzania), Absatou Ly Diallo (Senegal) na Graciano Domingos (Angola), Yvonne (Zambia) na Principe Ntibasume (Burundi).