Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makao makuu nchi wanachama ushoroba wa kati kujengwa Tanzania

Muktasari:

  • Jengo la makao makuu ya ushoroba wa kati linalotarajiwa kujengwa Tanzania linatarajiwa kurahisisha shughuli za usafirishaji kwa nchi wanachama ambao ni DRC, Tanzania, Zambia, Malawi, Rwanda na Uganda

Dar es Salaam. Nchi wanachama wa ushoroba wa kati zimekubaliana makao makuu ya ushoroba huo kujengwa Tanzania ili kuweka urahisi na kuimarisha shughuli za usafirishaji kwa njia ya bahari, reli na anga.

Hilo limefanyika wakati ambao Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimebadilisha hati za ardhi ambao kila nchi itakwenda kujenga bandari kavu kwa mwenzake kwa ajili ya kuhifadhi mizigo yake ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma.

Hayo yamesemwa Jumatano ya Juni 18, 2025 katika mkutano wa 14 wa mawaziri wa Usafirishaji kutoka nchi za ushoroba wa kati uliofanyika jijini Dar es Salaam. Nchi wanachama za ushoroba huo ni DRC, Tanzania, Zambia, Malawi, Rwanda na Uganda.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi Zambia, Frank Tayali amesema anafurahi kuona kanda inaanza kuzungumza kwa sauti moja kwani ipo haja ya kuwapo kwa juhudi za pamoja hasa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa kikanda.

“Tunashukuru Shirika la Kukuza Usafirishaji wa Kanda ya Kati linazidi kuimarika. Tanzania imetoa ardhi na tumeanza mipango ya kujenga jengo la kudumu la ghorofa nane, ambalo litakuwa ishara ya mshikamano wetu,” amesema.

Amesema kwa upande wa Zambia, kama nchi isiyo na bandari wanahitaji kuunganishwa kwa njia bora, hasa reli kwani moja ya gharama kubwa nchini kwao ni usafirishaji wa bidhaa.

“Tunajua reli inaweza kupunguza gharama hizo na hivyo kuweka urahisi kwa wananchi katika gharama nafuu za maisha na sasa kuna mazungumzo kuhusu kuunganisha kanda yote kwa reli.”

“Tuna wajibu kuwakilisha Kanda ya Kati, njia ya Ndola hadi Lubumbashi na pia njia mpya ya Lobito ambayo inakua kwa kasi. Tunatarajia ujenzi kuanza robo ya mwisho ya 2026,” amesema.

Amesema njia zote zitaiwezesha kanda kufanya biashara ndani ya bara na baadaye itafanya biashara na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Hii ndiyo njia bora kwa bara letu. Tunapolenga kutimiza ndoto ya Eneo Huru la Biashara la Afrika, tunaona fahari miongoni mwa wachangiaji. Tumejipanga kuhakikisha tunaunganishwa vizuri,” amesema Tayali.

Mwenyekiti wa ushoroba huo ambaye pia ni Waziri wa Uchukuzi wa Malawi, Jacob Hara amesema jambo atakaloanza nalo ni kuhakikisha uunganishaji wa nchi hizo ambao umekuwa ukijadiliwa kwa miaka mingi sasa unaanza kuzaa matunda.

“Utaona kwamba karibu kila nchi inayoshiriki mikutano hii ni nchi ambazo hazina bahari ndiyo maana Tanzania inakuwa mshirika wa kipekee na wa muhimu sana,” amesema.

“Kwa hiyo, kila tunachokifanya hapa ni kuhakikisha tunaweza kuunganishwa sisi kwa sisi na kupitia uunganishaji huo, tuweze pia kupata fursa ya kufika Dar es Salaam ambayo ni njia yetu kuu kuelekea baharini na duniani kote,” amesema Hara.

"Mikutano kama hii ni muhimu kwa sababu kila tunapokutana, tunaimarisha uhusiano wetu. Tunapata mawazo mapya kuhusu jinsi bora ya kuuboresha uhusiano huo. Mkutano huu ni mfano wa hilo, na tunaamini maazimio yake yatasaidia kuboresha na kupunguza gharama za uunganishaji barani Afrika," amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali ya Tanzania imejizatiti kikamilifu katika kuboresha ufanisi na kupunguza gharama za usafirishaji katika ukanda wa ushoroba wa kati.

“Jitihada hizi zinalenga kukuza biashara, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na hatimaye kuboresha kiwango cha maisha ya watu wetu katika eneo lote,” amesema Profesa Mbarawa.

Alitumia nafasi hiyo kuishukuru DRC kuitengea Tanzania ardhi katika maeneo matatu ya kimkakati ya Kasumbalesa, Kasenga na Kasambondo kwa ajili ya kujenga bandari kavu.

“Bandari hizi zitakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha biashara na shughuli za usafirishaji katika ukanda huu, hatua hii itaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda,” amesema.