Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tamisemi kutekeleza mambo 14 bajeti 2025/26

Muktasari:

  • Tamisemi imeomba Sh11.78 trilioni kwa bajeti ya 2025/26 kutekeleza vipaumbele 14, vikiwemo utawala bora, ukusanyaji mapato, huduma za jamii, miradi ya maendeleo na utunzaji mazingira.

Dar es Salaam. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeomba kuidhinishiwa Sh11.78 trilioni kutekeleza vipaumbele 14 katika mwaka wa fedha 2025/26.

Idadi hiyo ya vipaumbele vya mwaka huu ni mara mbili zaidi ya vile ilivyoahidi kuvitekeleza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25, kwa kiasi cha Sh10.1 trilioni ilizoidhinishiwa na Bunge.

Kukuza demokrasia, kusimamia shughuli za utawala bora, ushirikishwaji wa wananchi na ugatuaji wa madaraka kwa umma ni baadhi ya vipaumbele vitakavyotekelezwa kwa fedha hizo 2025/26.

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amewasilisha ombi la kuidhinishiwa kiasi hicho cha fedha leo, Jumatano, Aprili 16, 2025, alipowasilisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Tamisemi bungeni jijini Dodoma.

Kuhusu yatakayofanywa na wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, amesema itaratibu na kusimamia mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika ngazi zote.

Wakati Tamisemi ikiweka kipaumbele hicho, kumeonekana kasoro katika utekelezaji kama inavyoshuhudiwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Nimebaini mamlaka 26 za Serikali za mitaa zilielekeza Sh7.73 bilioni katika kutekeleza miradi na matumizi ya kawaida ambayo hayakuwa sehemu ya mpango uliokusudiwa awali,” amesema.

Mbali na hilo, vipaumbele vingine vinavyotekelezwa kwa bajeti hiyo, amesema ni kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na ugatuaji wa madaraka kwa umma.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, katika mwaka huo wanatarajia kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma za jamii.

Vingine, amevitaja kuwa ni ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zinazosimamiwa na ofisi hiyo.

Pia, ametaja uratibu wa usimamizi wa mifumo ya Tehama, kuendeleza rasilimali watu katika ngazi zote za Tamisemi na kuratibu na kusimamia shughuli za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa wizara hiyo mikoa na mitaa.

Mchengerwa ametaja kuratibu na kushiriki michezo ya shule za msingi (Umitashumta), sekondari- Umisseta na mashindano ya michezo ya shule za sekondari za Afrika Mashariki.

Vipaumbele vingine ni kuratibu shughuli za utendaji wa kazi wa taasisi zilizopo chini ya Tamisemi, kadhalika kuratibu na kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote za wizara hiyo.

Ametaja kuratibu uibuaji wa miradi ya kimkakati na inayopaswa kutekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika mamlaka za serikali za mitaa.

Amesema wizara hiyo itasimamia na kuratibu shughuli za utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili katika mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, kipaumbele kingine ni kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za mabadiliko ya tabianchi na uendelezaji wa utalii, uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia na uendelezaji wa biashara ya kaboni katika mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa.

Kipaumbele kingine, amesema ni kuratibu shughuli za uendelezaji wa vijiji na miji kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

Mchanganuo wa fedha alizoomba ni Sh7.83 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh6.26 trilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo, huku akitaja vipaumbele 14.

Kupitia bajeti hiyo, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), utakamilisha ununuzi wa mtoa huduma kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika awamu ya pili ya mradi huo.

Lingine, amesema wakala huo utaendelea na maandalizi ya usanifu na ujenzi wa miundombinu ya awamu ya tano ya barabara za Nelson Mandela, Mbagala na Tabata–Segerea–Kigogo zenye urefu wa kilomita 26.

“Kuendelea na ukarabati wa mara kwa mara wa miundombinu ya mfumo wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa vituo mlishi,” amesema.

Mchengerwa amesema wakala huo utakamilisha ufungamanishaji wa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji nauli na ule wa kuongozea magari, ikiwa ni sehemu ya maboresho endelevu ya huduma hiyo kwa wananchi wa Dar es Salaam.

Wakala huo pia, kwa mujibu wa Mchengerwa, utafanya pembuzi yakinifu nne kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya barabara za nyongeza za BRT: Rangi Tatu–Vikindu kilomita tano, Tegeta–Bunju kilomita 13, Kimara–Kibaha kilomita 20 na kuunganisha BRT awamu ya kwanza na nne kupitia Barabara ya Mwai Kibaki kilomita saba.

“Pia itafanya utafiti na kuibua vyanzo vipya vya mapato ya ndani kwa kuendeleza maeneo ya ushoroba wa mradi, ikiwemo ujenzi wa vitega uchumi kwenye maeneo ya Mtoni kwa Aziz Ally na eneo la Kariakoo Gerezani,” amesema.