Prime
WCB ya Diamond inachemka hapa

Muktasari:
- WCB inatajwa kati ya lebo kubwa baada ya Mavin Record (Nigeria), Davido Music World Wide (Nigeria), Chocolate City (Nigeria), Lilac Jeans na Super Black Tapes (Afrika Kusini). Lakini lebo hiyo imekuwa haitumii mfumo rasmi kutoa taarifa kuhusu wasanii wake mfano
Dar es Salaam. Lebo ya muziki nchini, Wasafi Classic Baby (WCB) inatajwa kama moja ya lebo kubwa Barani Afrika. Hasa ikiwa imetoa wasanii wakubwa kama vile Harmonize, Rayvanny, Zuchu, D Voice, Lavalava na wengineo. Lakini licha ya ukubwa wake kuna baadhi ya vitu bado inafeli hasa kwenye mfumo wa utoaji taarifa kuhusu mambo yanayohusu lebo hiyo.
WCB inatajwa kati ya lebo kubwa baada ya Mavin Record (Nigeria), Davido Music World Wide (Nigeria), Chocolate City (Nigeria), Lilac Jeans na Super Black Tapes (Afrika Kusini). Lakini lebo hiyo imekuwa haitumii mfumo rasmi kutoa taarifa kuhusu wasanii wake mfano

Mfano issue ya Mbosso, mapema mwaka huu ziliaza kusambaa taarifa kuhusu msanii huyo kujing'oa kwenye lebo hiyo, taarifa ambazo zilianza kusambazwa na Babalevo na baadaye ilikanushwa na mmiliki wa lebo hiyo, Diamond Platnumz.
Licha ya ukanushwaji huo Februari 5, 2025 baada ya kubananishwa na mwandishi wa habari siku ya miaka 48 ya Chama cha Mapinduzi, Diamond alithibitisha kuwa Mbosso kamalizana na lebo hiyo na kuwa msanii huru.
Tukio hilo lilizua mijadala mingi mtandaoni, mashabiki na wadau wakihoji kwa nini uongozi wa WCB haukutoa taarifa iliyo rasmi kuhusu msanii huyo kuondoka kwenye lebo hiyo.
Mbali na hilo leo Mei 8, 2025 zimesambaa taarifa kuhusu kuondoka kwa msanii Lavalava katika lebo hiyo. Taarifa hiyo imesambazwa na Babalevo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo amemuaga na kumtakia kila la heri msanii huyo.

"Safari njema mdogo wangu una kipaji kikubwa sana Lavalava. Na Watanzania watakuwa mashahidi kwa namna ambavyo mzee wangu LUKUGA alikipigania kipaji chako kibadilike kuwa pesa.
Kafanya kila namna ikiwemo kushirikiana na wewe kwenye nyimbo nyingi mno. Umekuwa sasa ni vyema kujitegemea ili kuwapa nafasi wadogo zako wengine," ameandika Baba Levo.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Babalevo kutoa taarifa kuhusu kinachoendelea kwenye lebo hiyo, kabla hata ya uongozi husika kusema chochote. Tabia hiyo imesababisha wengi kumuamini kwa sababu ni mtu wa karibu wa Diamond Platnumz.
Lebo ya WCB inakurasa rasmi za mitandao ya kijamii lakini pia ina vyombo vya habari ambavyo vipo chini ya mmiliki wa lebo hiyo. Lakini ni ngumu kukuta taarifa za wasanii kuondoka zikichapishwa kwenye kurasa zao mpaka mtu wa pembeni kuanza kuzitoa.

Kwa hili wameshindwa hadi na lebo changa ya Nandy, 'The African Princes' ambayo Mei 5, 2025 ilitangaza kumaliza mkataba na aliyekuwa msanii wake Yammy.Taarifa zilitolewa kupitia mitandao rasmi ya kijamii ya lebo hiyo.