Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Studio za nyumbani zinavyoongeza ubunifu

Muktasari:

  • Wasanii kama Diamond Platnumz, Bob Junior, Nahreel, Harmonize, Marioo na wengine wengi wote wanamiliki studio za nyumbani ambazo wanatumia kutengenezea kazi zao. Jambo linalojenga tafsiri ya mafanikio ambayo zamani yalikuwa yakifanywa na wasanii wa mataifa mengine.

Dar es Salaam, Muziki wa Bongo Fleva unaendelea kukua kwa kuonesha mabadiliko makubwa na ongezeko la studio za kurekodi nyimbo za majumbani zinazoendelea kutengenezwa na baadhi ya wasanii.

Kwa sasa imekuwa kawaida kwa baadhi ya wasanii kutenga maeneo maalumu ndani ya nyumba zao kwa ajili ya kurekodi nyimbo zao.

Wasanii kama Diamond Platnumz, Bob Junior, Nahreel, Harmonize, Marioo na wengine wengi wote wanamiliki studio za nyumbani ambazo wanatumia kutengenezea kazi zao. Jambo linalojenga tafsiri ya mafanikio ambayo zamani yalikuwa yakifanywa na wasanii wa mataifa mengine.

Wakiwa na vifaa vya kurekodi vya msingi, programu za kompyuta, wasanii chipukizi na nyota wengine katika tasnia hiyo wamegeuza vyumba vyao vya kulala na maeneo ya kupumzikia kuwa mahali pa kufanya muziki.

Hata hivyo, wanapohamisha mazingira ya kazi za kutengeneza muziki na kuyapeleka nyumbani, maswali yanaibuka: Je, hizi studio za nyumbani ni msaada wa kupeleka tasnia mbele, au ni anguko kwa studio za mitaani na maproduza?

Akizungumza na Mwananchi mtayarishaji wa muziki wa injili na msanii, Mathias Walichupa, anasisitiza umuhimu wa studio za nyumbani kuwa zinasaidia kuwaongezea ubunifu.

“Wasanii mara nyingi wanakumbana na changamoto kubwa wanapokwenda kurekodi wanakutana na foleni ndefu na wanapaswa kusubiri kwa muda mrefu, wakihatarisha kupoteza mawazo yao na sauti waliyoikusudia. Hata hivyo, wakiwa na studio ya nyumbani, wana uwezo wa kufanya kazi kwa haraka wakiwa na mawazo yaleyale na kisha kuwapelekea watayarishaji kwa ajili ya maboresho zaidi,” amesema.

Anasisitiza kuwa kumiliki studio ya kurekodi nyumbani kunapunguza hatari ya kupoteza rekodi za awali.

“Wakati mwingine, wimbo unapoanza kupata umaarufu na unahitaji remix, changamoto huja unapomfuata mtayarishaji na kugundua kuwa amefuta matirio ya awali. Hata hivyo, kumiliki studio ya nyumbani kunawawezesha wasanii kuepuka hali hii kwa kuhifadhi taarifa zao wenyewe kwa usalama,” anafafanua.

Anasisitiza umuhimu wa kushirikiana na watayarishaji wa kitaalamu ili kuhakikisha ubora wa hali ya juu kwenye kazi.

“Kumiliki studio ya kurekodi haimaanishi kuwa unapaswa kushughulikia kila kitu mwenyewe. Ni muhimu kushirikisha watayarishaji wa kitaalamu ili kuhakikisha kazi inafikia ubora wake wa juu zaidi. Kumiliki studio ya nyumbani peke yake hakukufanyi kuwa mtayarishaji wa kitaalamu wasanii wanapaswa kuelewa tofauti hii,” anasema Mathias.

Kwa upande mwingine, mtayarishaji wa Bongo Fleva anayesimamia hits kama ‘Kibango’ ya Lavalava ft. Diamond Platnumz, ‘Honey’ ya Zuchu, na Lugendo Zuberi, maarufu kama Mr. LG, anasema kuwa muziki sio tu kuhusu vifaa.

“Kumiliki studio za nyumbani ni muhimu kwa wasanii, lakini haimaanishi kuwa hakuna kazi. Hata baada ya kukamilisha kazi za awali, bado tutapanga vipindi vya kuboresha na kuleta ukamilifu kwenye nyimbo zilizotengenezwa nyumbani,” anasema.

Pia alisifu wasanii wengi kwa uwezo wao wa kujirekodi, jambo ambalo linapunguza mchakato mgumu ambao kwa kawaida hufanyika kwenye studio wanapopokea biti na nyimbo kutoka kwa watayarishaji.

“Hivyo basi, ili kupata sauti inayovutia duniani kote na inayochezeka, ni faida kwetu watayarishaji kuchukua jukumu la kuboresha sauti hiyo. Kurekodi nyumbani, hasa, kunategemea sana zana za kitaalamu,” amesema Mr.LG.

Jay Drama, anaamini ni muhimu kwa mamlaka kuhakikisha wanapitia miradi hii ili kuweka viwango vya studio hizo.

“Kuwa na studio nyingi sio jambo baya; haiko kama zamani ambapo zilikuwa chache na ilikuwa vigumu kwa watu kuonyesha vipaji vyao. Siku hizi, yeyote anaweza kuwa na studio ya nyumbani na kutengeneza kazi bora.

Hata hivyo, ninachopendekeza ni kwa haya mabaraza na taasisi kuweka viwango kwa studio hizi kwa sababu kuna uzalishaji mwingi, lakini ni wachache tu wanaofikia viwango,” anasema Jay Drama.

Mwanamitindo na mcheza dansi Ben Breaker, anasema kumiliki studio ya kurekodi nyumbani kunamaanisha kuwa mashabiki wanatarajia kuona muziki mzuri badala ya uzalishaji duni.

“Kila msanii sasa anamiliki nafasi ya kurekodi nyumbani, lakini naamini kuwa kwa sababu hii, baadhi ya wasanii wanatoa rekodi mbaya kwa sababu wanakwepa ukosoaji na hii inaathiri ,” anasema.

Kwa mujibu wa msanii wa hip-hop wa Bongo Fleva, Stamina, ambaye anamiliki studio yake ya kurekodi ‘Paradise Music’, ambapo amekuwa akitoa hits zinazoshika chati.
Anaamini kuwa ni muhimu kwa msanii kuwa na studio ya kurekodi nyumbani katika dunia ya leo.

Ingawa haimaanishi kwamba msanii anapaswa kufanya kazi yote mwenyewe, anaweza kuitumia kurahisisha kazi hizo na kupunguza muda wa mchakato.

“Unaweza kurekodi lakini haimaanishi kuwa ni wimbo unaotaka kutoa, unaweza kuanza kijirekodi na kisha kumsikilizisha mtayarishaji wa kitaalamu na kurekodi upya,” amesema.

Nyimbo maarufu kama ‘Underrated’, ‘Machozi’, na nyingi zaidi zilirekodiwa katika studio yake ya nyumbani.

Stamina anaeleza kwamba wakati mwingine wasanii wanahitaji kujifunza kutoka kwa  wengine na kujaribu kuunda muziki wao bila kutumia muda mwingi kwa watayarishaji.

“Hakuna kitu kinachoweza kuchukua nafasi ya mtayarishaji wa muziki wa kitaalamu, lakini ikiwa una ubunifu katika kipengele cha kiufundi cha kurekodi, unaweza kuunda muziki mzuri na kushirikiana na watayarishaji wa muziki wazuri,” anaeleza.