Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu, Jackie Chan kutowarithisha wanawe utajiri wake

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Staa huyo, urithi mkubwa anaotaka kuuacha si kwa ajili ya familia yake. Bali mchango utakaoendelea kuboresha maisha ya watu wengi hata baada ya yeye kuondoka duniani.

Hong Kong. Gwiji wa filamu za mapigano duniani, kutoka Hong Kong, Jackie Chan, amewahi kueleza sababu za kutowaachia watoto wake sehemu ya utajiri wake unaokadiriwa kufikia dola 400 milioni za Marekani (Sh1.5 trilioni). Akisisitiza mafanikio ya kweli yanapaswa kutafutwa kwa juhudi binafsi.

Chan amewahi kusema kuwa maisha yake ya utotoni yaliyojaa changamoto na umaskini ndiyo yaliyomjenga kuwa mtu anayethamini juhudi katika kazi. Hivyo anaamini urithi mkubwa unaweza kuwafanya watoto kukosa hamasa ya kujituma.

“Akiwa na uwezo, ataweza kutengeneza pesa zake mwenyewe. Asipokuwa na uwezo, basi atakuwa anapoteza pesa zangu tu,” amewahi kusema Chan akizungumzia suala la urithi kwa mwanawe wa kiume, Jaycee Chan.

Muigizaji huyo amesema jukumu la mzazi ni kuwajengea watoto msingi mzuri wa maisha, si kuwapa maisha ya kutegemea mali walizochuma wengine.

Gwiji wa filamu za mapigano duniani, kutoka Hong Kong, Jackie Chan, akiwa na mtoto wake wa kiume Jaycee Chan. Picha na Mtandao


Kifungo cha mwanawe kisa dawa za kulevya

Mwaka 2014, mtoto wake wa kiume Jaycee alikamatwa jijini Beijing, China, baada ya polisi kukuta zaidi ya gramu 100 za bangi katika nyumba yake. Jaycee alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kumiliki dawa hizo na kuruhusu matumizi yake nyumbani kwake.

Tukio hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Chan ambaye wakati huo alikuwa balozi wa kampeni za kupambana na dawa za kulevya nchini China. Licha ya ushawishi wake mkubwa, Chan hakujaribu kumwokoa mwanawe kupitia njia za kisiasa au kifedha, akisisitiza kuwa lazima awajibike kwa makosa yake.

Baadaye, Chan alieleza masikitiko yake kwa namna alivyomlea mwanawe na kusema alitamani angepata malezi yenye nidhamu zaidi.

Gwiji wa filamu za mapigano duniani, kutoka Hong Kong, Jackie Chan (kushoto), mwingine kulia ni binti yake Etta Ng Chok Lam. Picha na Mtandao


Maisha ya binti yake

Tofauti na Jaycee, binti yake Etta Ng Chok Lam amekua bila uhusiano wa karibu na baba yake. Etta, ambaye alizaliwa nje ya ndoa, aliwahi kuripotiwa kukabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha nchini Canada, ambako alienda kuishi na mwenza wake.

Gwiji wa filamu za mapigano duniani, kutoka Hong Kong, Jackie Chan. Picha na Mtandao


Utajiri kuelekezwa kwenye misaada

Badala ya kuwaachia watoto wake mali zake, Chan amesema anataka sehemu kubwa ya utajiri wake itumike kusaidia jamii kupitia taasisi ya Jackie Chan Charitable Foundation.

Kupitia taasisi hiyo, fedha zimekuwa zikielekezwa katika ujenzi wa shule, tafiti za afya, misaada ya majanga na miradi mingine ya kijamii duniani.

Kwa mujibu wa Chan, urithi mkubwa anaotaka kuuacha si kwa ajili ya familia yake. Bali mchango utakaoendelea kuboresha maisha ya watu wengi hata baada ya yeye kuondoka duniani.

“Wakati nitakapokufa, akaunti yangu ya benki itakuwa sifuri,” amewahi kusema Chan.