Jackie Chan afikisha miaka 72, aendelea kung’aa kwenye filamu
Muktasari:
- Chan, aliyezaliwa Aprili 7, 1954, anajulikana zaidi kwa umahiri wake wa kucheza katika filamu. Tofauti na waigizaji wengi, mara nyingi amekuwa akifanya mwenyewe ‘stunts’ vyenye mchanganyiko wa vichekesho, jambo lililomfanya kuwa maarufu zaidi
Hong Kong. Mwigizaji maarufu wa filamu za mapigano kutoka Hong Kong, Jackie Chan, ametimiza miaka 72 huku akibaki kuwa mmoja wa mastaa wenye mchango mkubwa katika tasnia ya filamu duniani.
Chan, aliyezaliwa Aprili 7, 1954, anajulikana zaidi kwa umahiri wake wa kucheza katika filamu. Tofauti na waigizaji wengi, mara nyingi amekuwa akifanya mwenyewe ‘stunts’ vyenye mchanganyiko wa vichekesho, jambo lililomfanya kuwa maarufu zaidi.
Umaarufu wake ulianza kuonekana miaka ya 1970 na 1980 kupitia filamu zilizompa nafasi kubwa katika soko la Asia kabla ya kuvuka mipaka na kuteka soko la Hollywood. Baadhi ya filamu zilizompa umaarufu ni Rush Hour, Police Story, Drunken Master na Shanghai Noon. Filamu hizi zilimfanya kuwa miongoni mwa waigizaji wachache wa Asia walioweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa katika soko la kimataifa.
Katika maisha yake ya sanaa, Chan ameigiza zaidi ya filamu 150, akijijengea heshima kama msanii mwenye nidhamu, ubunifu na uwezo mkubwa wa kuigiza. Mbali na uigizaji, pia ni mwimbaji, mtayarishaji wa filamu na mkurugenzi.
Jackie Chan anatajwa kuwa miongoni mwa waigizaji matajiri zaidi katika tasnia ya filamu. Utajiri wake unakadiriwa kufikia zaidi ya dola400 milioni. Akipata mapato kupitia uigizaji, utayarishaji wa filamu, matangazo ya kibiashara pamoja na uwekezaji katika biashara mbalimbali. Mafanikio yake katika soko la Asia na Hollywood yamechangia kumfanya kuwa miongoni mwa mastaa wanaolipwa vizuri zaidi katika filamu za mapigano.
Mbali na utajiri wake, Chan pia amejikusanyia tuzo nyingi kutokana na mchango wake mkubwa katika tasnia ya filamu. Mwaka 2016 alipokea tuzo maalum ya heshima ya maisha kutoka Academy of Motion Picture Arts and Sciences kupitia tuzo za Academy Honorary Award, ikiwa ni kutambua mchango wake wa muda mrefu katika filamu za kimataifa. Tuzo hiyo ilikuja baada ya zaidi ya miaka 50 ya kazi yake katika sanaa ya filamu.
Aidha, katika maisha yake ya sanaa, Chan ameshinda na kuteuliwa kwa tuzo nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya filamu duniani, ikiwemo Hong Kong Film Awards na MTV Movie Awards.