Neila:Kabla ya vichekesho nilikuwa nafanya kazi za ndani

Muktasari:
- Akizungumza na Mwananchi, Neila amesema hiyo ni changamoto kubwa kwa sasa kwenye tasnia ya ucheshi kwani wanashindwa kukuza vipaji vyao.
Dar es Salaam. Mchekeshaji Neyla Manga 'Neila' ametolea lawama kitendo cha baadhi ya matukio makubwa nchini kutowapa nafasi wachekeshaji wa kike kuonesha vipaji vyao.
Akizungumza na Mwananchi, Neila amesema hiyo ni changamoto kubwa kwa sasa kwenye tasnia ya ucheshi kwani wanashindwa kukuza vipaji vyao.

"Changamoto kubwa zaidi wanashindwa kukuza vipaji vyetu, naweza nikasema tunapata jukwaa lakini jukwaa letu halitoshelezi. Yanapotokea matamasha tumekuwa ni watu tunaosahaulika sana.
“Mfano inapotokea matamasha tumekuwa watu wa kusahaulika, tumekosa hiyo bahati ya kuonekana na kupewa nafasi," amesema Neila.
Neila ambaye ametambulika kupitia jukwaa la Cheka Tu ametolea mfano tukio la ugawaji wa tuzo kwa waandishi wa habari 'Samia Kalamu Awards' lililofanyika Mei 5, 2025 mbele ya mgeni rasmi Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo wachekeshaji wa kiume pekee ndio walipata nafasi ya kupafomu.
"Sio kwamba tunafanya vibaya tunafanya vizuri. Basi usinichukue mimi Neila mchukue mama Mawigi, mchukue Asmah. Inapotokea kitu kama hicho wanatusahau sisi wanawapa kipaumbele wanaume ambao wana uwezo wa kujimudu, bora watupe na sisi wanawake ili tuendelee kujifunza zaidi," amesema Neila.

Amesema alijisikia kutopewa nafasi kwa wanawake kupafomu kwenye jukwaa hilo, licha ya mgeni rasmi kuwa mwanamke namba moja nchini.
"Mimi binafsi nimejisikia vibaya nilitaka nijue changamoto ni nini mpaka hatujapewa nafasi. Kwanini hatujapewa nafasi wakati kuna wachekeshaji wa kike wanafanya vizuri kuliko hao wa kiume ambao wamewachukua,"amesema Neila.
Amesema kuwa mshikamano baina ya wanawake wanaofanya tasnia ya Ucheshi ni mkubwa na hakuna mikwaruzano zaidi ya kuwa na ushindani pekee.
Aidha, Neila ameweka wazi kuwa hakutegemea kama atakuwa mchekeshaji, kwani awali alikuwa mwimbaji wa nyimbo za injili mkoani Mara.
"Nilivyokuwa nyumbani Mara nilikuwa mwimbaji wa nyimbo za injili. Nimeingia Dar 2021 baada ya kufika nilikuwa najishughulisha na kazi za ndani lakini mshahara ulikuwa mdogo.
“Nikaingia kwenye uchekeshaji, mwaka 2023 niliacha kazi ya ndani baada ya muajiri wangu kuniona kwenye Tv na wakati nilimwambia naumwa, baada ya kuniona akaniuliza nichague moja kazi au sanaa nikachagua sanaa," amesema Neila.
Amesema japo hana muda mrefu kwenye tasnia ya ucheshi lakini amefanikiwa kupita kwenye majukwaa mengi ya komedi.

"Nimeingia Punch Line nikawa napewa dakika moja ya kupafomu, Evance Bukuku akanikutanisha na Watubaki nikakutana na Mc Kisoli akanifunza kuandika Jokes, akanifunza kumiliki jukwaa, nini cha kuongea.
“Akanifunza kuondoa matusi kwenye utani wangu maana nilikuwa natukana mno, baada ya kujua yote hayo ndio Clay akanitafuta mwaka jana 2024 kwa hiyo mimi hata ustaa wangu hauna muda sana," amesema Neila.