Mzee Onyango kuzikwa Juni 13
Mwigizaji mkongwe wa filamu nchini, Issa Joseph maarufu kwa jina la Mzee Onyango enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Familia ya marehemu imethibitisha kukamilisha taratibu za awali za mazishi na kueleza kuwa maandalizi ya kumuaga mpendwa wao yanaendelea huku wakiendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka kwa wadau wa sanaa na wananchi.
Dar es Salaam. Mazishi ya muigizaji mkongwe wa tasnia ya maigizo Tanzania, Issa Joseph 'Mzee Onyango', yatafanyika Jumamosi Juni 13 , 2026 katika Makaburi ya Kondo Ununio jijini Dar es Salaam.
Familia ya marehemu imethibitisha kukamilisha taratibu za awali za mazishi na kueleza kuwa maandalizi ya kumuaga mpendwa wao yanaendelea huku wakiendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka kwa wadau wa sanaa na wananchi.
Mtoto wa marehemu, Kabuti Onyango, amesema kuwa familia imepanga kumuaga rasmi baba yao siku ya Jumamosi na imewaomba watu wote walioguswa na msiba huo kujitokeza kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho.
Kabuti amesema marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa presha kwa muda mrefu, hali iliyokuwa ikiendelea kumdhoofisha kiafya kabla ya umauti kumkuta akiwa Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa hali ya baba yake ilibadilika ghafla siku chache zilizopita, hali iliyowalazimu kumkimbiza hospitalini kwa matibabu ya dharura, lakini juhudi za madaktari hazikuweza kuokoa maisha yake.
"Alikuwa akisumbuliwa na presha kwa muda mrefu, lakini ghafla hali yake ilibadilika na tukamkimbiza hospitali. Kwa masikitiko makubwa amefariki akiwa anapatiwa matibabu," amesema Kabuti.
Mzee Onyango atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya sanaa ya maigizo Tanzania, ambapo aliigiza nafasi mbalimbali zilizogusa hisia za watazamaji na kumfanya kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za sanaa hiyo.
Enzi za uhai wake Mzee Onyango ameonekana katika filamu na tamthilia mbalimbali ikiwemo, Babu The Perfect Man, Ripoti, Kimbembe na nyinginezo.