Ushuru wa nondo, mabati kutoka nje wapaa
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imependekeza kuongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa mbalimbali za chuma, mabati, nondo na mabomba ya chuma zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Hatua hiyo inalenga kulinda viwanda vya ndani, kuhamasisha uwekezaji, kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
Akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 leo Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari amependekeza ushuru wa bidhaa hizo kwa mfumo wa asilimia au kiwango maalumu kwa kila tani moja, kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa zaidi.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, baadhi ya bidhaa za chuma zitatozwa ushuru wa asilimia 10 au dola za Marekani 125 kwa kila tani moja badala ya asilimia 10 pekee kwa mwaka hivi sasa.
Aidha, baadhi ya mabati yatatozwa ushuru wa asilimia 35 au dola za Marekani 500 kwa kila tani moja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa zaidi badala ya asilimia 35 pekee inayotozwa sasa.
Mapendekezo hayo pia yanaonyesha kuwa baadhi ya mabati yatatozwa ushuru wa asilimia 35 au dola za Marekani 350 kwa kila tani moja badala ya asilimia 25 au dola za Marekani 200 kwa tani moja zinazotozwa kwa sasa.
Mabati mengine yatatozwa ushuru wa asilimia 25 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja badala ya asilimia 25 au dola za Marekani 200 kwa tani moja.
Kadhalika, baadhi ya mabati yatatozwa ushuru wa asilimia 35 au dola za Marekani 350 kwa kila tani moja badala ya asilimia 35 pekee inayotozwa sasa, huku mengine yakitozwa asilimia 10 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja badala ya asilimia 10 pekee.
Kwa upande wa nondo, Serikali imependekeza kuongeza ushuru kutoka asilimia 25 au dola za Marekani 200 kwa tani moja hadi asilimia 25 au dola za Marekani 250 kwa tani moja.Aina nyingine za nondo zitatozwa ushuru wa asilimia 35 au dola za Marekani 250 kwa kila tani moja badala ya asilimia 35 pekee inayotozwa sasa.
Mbali na hilo, baadhi ya bidhaa za chuma zitatozwa ushuru wa asilimia 25 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja badala ya asilimia 10 pekee inayotozwa sasa, huku nyingine zikitozwa asilimia 10 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja badala ya asilimia 10 pekee.
Pia, mabomba ya chuma na bidhaa nyingine za chuma zitatozwa ushuru wa asilimia 25 au dola za Marekani 250 kwa kila tani moja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa zaidi badala ya asilimia 25 pekee inayotozwa sasa.
Serikali imesema hatua hizo zinalenga kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hizo, kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda, kuongeza ajira na mapato ya Serikali pamoja na kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.