Mwanamuziki Enisa alivyotoboa kimtindo

Muktasari:
- Wapo waliojaribu na kuachia njiani na kuna wale wenye uthubutu kama ilivyo kwa msanii Enisa Nikaj ‘Ebisa’. Haikuwa kazi rahisi kutoboa kimuziki na kilichosababisha hilo ni kuanzia kurudia kazi ‘Cover’ za miziki ya wasanii wengine na kuzitangaza.
Marekani. Kuna namna nyingi ya mtu kutoka kimaisha hasa kama una kipaji. Ni namna gani tu wewe mwenyewe utajiongeza kutokana na kile ulicho nacho na kuvutia watu na kukigeuza kuwa fursa.
Wapo waliojaribu na kuachia njiani na kuna wale wenye uthubutu kama ilivyo kwa msanii Enisa Nikaj ‘Ebisa’. Haikuwa kazi rahisi kutoboa kimuziki na kilichosababisha hilo ni kuanzia kurudia kazi ‘Cover’ za miziki ya wasanii wengine na kuzitangaza.
Alianza safari ya muziki mwaka 2015. Licha ya kupitia magumu ya kujulikana, hakuacha ndoto yake ipotee na alianza kufanya kazi ya kutoa cover za wasanii maarufu kwenye mtandao wa YouTube, akilenga kuwavuta mashabiki na watu wa tasnia kwa kipaji chake halisi.
Amepita mulemule katika nyimbo za wasanii kama Chris Brown, wimbo maarufu wa ‘Allah Allah Ya Baba’ wa Dj wa Iran, Arash Mohseni mwaka 2017 na sauti yake ya kike ilimfanya azidi kupata umaarufu mkubwa.

Katika wimbo huo alibadili baadhi ya maneno na kuupa jina la ‘Count My Blessing’ na uliotoka mwaka 2021. Wimbo huo ulifikisha zaidi ya watazamaji milioni 86 na ikawa njia ya kumfungulia milango ya mafanikio kimuziki.
Baada ya kupata umaarufu alitoa nyimbo zake binafsi kama ‘Burn This Bridge’ na ‘Love Cycle’ zilizompa umaarufu mkubwa hasa Nigeria na alifanya remix ya wimbo Love Cycle na Davido na kubatizwa jina la Eniola na mashabiki wa nchi hiyo.
Enisa ni mtoto wa pili katika familia yao, akiwa na kaka mkubwa na mdogo. Wakati ndugu zake walichagua kujiingiza kwenye mchezo wa mpira wa kikapu na yeye alihisi kuvutiwa zaidi na muziki, alianza kuimba akiwa mtoto mdogo.

Mwanamitindo
Kabla ya kuingia rasmi kwenye muziki, Enisa ambaye ni mzaliwa wa Marekani katika jiji la Brookly na wazazi wa Kialbania alianzia kwenye uanamitindo akiwa bado shule ya sekondari, alionekana kwenye jarida la Prom Guide la mwaka 2014.
Hata hivyo, alianza kupata madili baada ya kujulikana kimuziki na mwaka 2016 alisaini mkataba na Kampuni Maarufu ya Wilhelmina Modeling Agency, uliomfungulia milango zaidi akionyesha umahiri wake wa kubadilika na kupendeza katika mazingira tofauti ya mitindo.
Hata hivyo staili yake ya uvaaji anayoipenda kuvaa nguo kubwa yaani oversize (Tshirt na Suruali) imeacha maswali kwa mashabiki zake na mwenyewe anadai anapendelea kuvaa hivyo kwa sababu mara nyingi amekuwa akiongozana na wazazi wake kwenye kazi zake, hivyo sio heshima kwake kuvaa nguo za ajabu mbele ya wazazi wake jambo ambalo alipongezwa na mashabiki wake.
Video nyingi za ngoma zake zinashutiwa na mama yake mzazi ambaye anakuwa nyuma ya kamera kuhakikisha anatoka vizuri kuanzia ‘make-up’ na vitu vingine ambavyo msanii anatumia.

Kolabo na Rayvanny
Mwaka 2020 Rayvanny wakati yupo chini ya lebo ya Wasafi alitoa ngoma na Zuchu ‘Number One’ iliyofanya vizuri kwenye mtandao wa Youtube ikiingiza watazamaji milioni 34.
Mwaka uliofuata akafanya remix ya wimbo huo na Enisa ambaye alikuwa Marekani, kipindi cha ugonjwa wa Corona ikafanya vizuri na kumuongezea mashabiki mwanadada huyo kwa upande wa Afrika.

Yuko kwenye lebo
Mwaka 2018, Enisa alipata mwaliko wa kwenda studio na msanii wa hip-hop, A Boogie Wit Da Hoodie, mwaka mmoja baadaye, alimwalika tena na kumtambulisha kwa wakubwa wa Atlantic Records na mwana huo alisaini mkataba wa kwanza.
Mwezi Desemba huo, Enisa alitoa wimbo wake wa sita, “Something Beautiful,” kama heshima kwa wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea Albania mwaka 2019.
Baadaye mwaka huo huo, alitoa wimbo mwingine uitwao ‘Dumb Boy’, nyimbo hizo mbili ‘Love Cycle’ zilipata jumla ya mauzo ya zaidi ya milioni 12 kwenye YouTube ndani ya mwaka mmoja, jambo lililodhihirisha rasmi kuwa Enisa ni nyota mpya wa muziki wa Pop.

Maisha binafsi
Msanii huyo hajawahi kuweka wazi maisha yake ya mahusiano jambo ambalo limefanya mashabiki wake kuwa na shauku ya kujua.
Kwenye moja ya mahojiano aliyowahi kufanya alipoulizwa kuwa kama ana mpenzi alisema;
“Sina mpenzi kwa sasa lakini nataka kuolewa na mwanaume anatakaye nipenda na kunijali na aelewe kazi yangu.”