Muziki wa singeli mbioni kuwa sehemu ya Urithi wa Dunia

Muktasari:
- Kabudi ameyasema hayo Bungeni, jijini Dodoma leo Mei 7,2025 alipokuwa akiwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi amesema muziki wa singeli upo mbioni kutangazwa rasmi kuwa sehemu ya Orodha ya Urithi wa Dunia.
Kabudi ameyasema hayo Bungeni, jijini Dodoma leo Mei 7,2025 alipokuwa akiwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

"Wizara kwa kushirikiana na UNESCO, iliratibu warsha ya wadau ya uteuzi wa muziki wa singeli kuorodheshwa kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia unaoratibiwa na UNESCO. Warsha hiyo ilifanyika Machi 24-25, 2025 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 120 kutoka Wizara, taasisi na wadau wa sekta ya utamaduni wa mikoa mbalimbali nchini.
"Muziki wa Singeli, unatumia vionjo vya ngoma za asili ikiwamo midundo na mikong’oso. Midundo ya Singeli imeendelea kuzalishwa kwa wingi kupitia kivunge cha mtozi kilichotengenezwa na BASATA.
"Upekee wa Singeli umeifanya kuwa kivutio kikubwa katika matamasha makubwa ya kimataifa kama vile “Nyege Nyege” Festival nchini Uganda, DUO Festival nchini Ubelgiji, Primavera Sound Festival Nchini Hispania, Apporlibation Festival nchini Ujerumani na Cora Festival nchini Ufaransa,"amesema
Amesema baada ya kumalizika kwa warsha hiyo, Wizara iliandaa nyaraka muhimu za uteuzi
(Nomination Dossier) na kuziwasilishwa UNESCO Makao Makuu Paris, Ufaransa kwa ajili ya hatua za kuidhinishwa.

"Hivi sasa kinachosubiriwa ni kukamilika kwa taratibu za UNESCO ili hatimaye kutangaza rasmi muziki wa Singeli kuwa sehemu ya Orodha ya Urithi wa Dunia, hatua ambayo itaimarisha zaidi hadhi ya utamaduni wa Tanzania Duniani,"amesema
Utakumbuka Desemba 16,2024, wakati Waziri Kabudi akipokelewa rasmi katika Ofisi za wizara hiyo, jijini Dodoma alisema kati ya mambo ya kuwekeza nguvu ni kuifanya dunia ijue vinyago vya kimakonde na picha za Tingatinga vinatoka Tanzania.
"Nataka tuweke nguvu kwenye muziki. Kwanza muziki huu ambao ni wa aina yake singeli, leo ikipigwa Brazil, Peru, na India ina mridimo na msisimko wa aina yake kwa wale Waafrika maelfu na mamilioni waliochukuliwa kama watumwa,"alisema Kabudi mwaka jana.
Hata hivyo, baada ya kauli hiyo mwanamuziki na mzalishaji wa muziki wa singeli nchini Mushizo ameiambia Mwananchi ni wakati wa wasanii wa muziki huo kuongeza juhudi.

"Prof Kabudi ni kiongozi katika sekta yetu ya sanaa, kutokana na kauli yake nadhani sisi wasanii tunatakiwa kuwekeza juhudi na kuufanya muziki wa singeli kwenye umakini zaidi. Kwa sababu hadi watu wakubwa wanaona muziki katika jicho la tatu hii ni fursa yetu 1kukaza 1zaidi. Ombi langu waanze kwa kugusa kwenye uwekezaji",Mushizo.
Kwa upande wake msanii wa muziki huo na mshindi wa Tuzo za TMA mara nne Dulla Makabila amesema singeli ndiyo muziki unaoweza kuleta tuzo ya aina yoyote nchini.
"Ni kitu kikubwa tunashukuru kwa kutoa hilo wazo. Singeli ni utamaduni wa Tanzania na ndiyo kitambulisho na una nguvu ya kuleta tuzo yoyote kwenye hii nchi. Ni watu tu wanafanya kazi ya kudandia miziki ya watu, lakini ni kitu kikubwa ambacho hatujaamua kukiwekea nguvu na kufanya uwekezaji mkubwa. Serikali ianze kugusa wasanii wenyewe wa singeli", amesema Makabila.

Mbali na hayo msanii Imo kutoka kundi la muziki wa singeli la Wamoto linalohusisha wasichana wawili, Suzibaby na Imo, amesema kauli ya waziri huyo ni faraja kwao.
"Kauli hii ina maana kubwa kwetu kwa sababu kaangalia kwa jicho la pili. Singeli ndiyo muziki unaosumbua kwa sasa siyo Tanzania tu hata nje ya nchi, tofauti na miziki mingine.
"Naona wasanii wa singeli tungeangaliwa zaidi kwa kupewa mikopo ili tuweze kuwekeza zaidi na kuutambulisha muziki wa singeli na taifa. Wasiache kutualika kwenye majukwaa makubwa,"amesema Imo.