Msigwa awasha moto asema sanaa ni biashara, siyo usela

Muktasari:
- Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umeweza kutoa mikopo ya Sh 5.250 bilioni kwa miradi 359 ya utamaduni na sanaa kwa mikoa 19 ambayo imezalisha ajira 497,213.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amewataka wasanii kufanyakazi kwani takwimu za mwaka 2023 zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu nchini (NBS) imeeleza sekta ya sanaa imekuwa kwa asilimia 17.1.
Amesema kutokana na takwimu hizo wasanii wanatakiwa kujikita kwenye uwekezaji wa sanaa na wasiogope kukopa kwenye mfuko wa utamaduni na sanaa, kwani waliowekeza kwenye biashara kubwa wanakopa na kulipa akiwepo msanii Nasib Abdul 'Diamond'.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania Nyakaho Mahemba akizungumza na wadau wa Utamaduni na Sanaa kwenye warsha iliyofanyika Makumbusho ya Taifa, Jijini Dar es Salaam
Msigwa amesema lengo la Serikali ni kuzalisha kina Diamond wengi ambao wanaweza kukopa na kurudisha ili waweze kufanya sanaa popote ndani na nje ya nchi na sio kukopa na kutoroka nazo. Kwani hawatapata mafanikio kwenye biashara zao kwa kukimbia na madeni.
"Tufanye kazi na sio usela kuna wakati nikiona msanii anaomba omba naumia najisemea huu mbona ni mgodi unaotembea. Wakati sisi ni uchumi wa Taifa na tunatakiwa kujivunia kwa sababu tunaongiza kwa kuchangia pato la Taifa,"amesema Msigwa.
Hayo amesema leo Aprili 17, 2025 kwenye warsha ya wadau wa utamaduni na sanaa na kueleza kuwa Serikali imechukua hatua madhubuti ili kuimarisha sekta ya utamaduni na sanaa na ilianzisha mfuko ili kusaidia wasanii.
Amesema mfuko huo umeweza kutoa mikopo ya Sh 5.250 bilioni kwa miradi 359 ya utamaduni na sanaa kwa mikoa 19 ambayo imezalisha ajira 497,213.
Pia, Msigwa amewataka wasanii wakubwa kuhudhuria kwenye warsha zinazoandaliwa na sio kutuma wawakilishi wao. Kwani kuna mengi ya kujifunza yatakayowasaidia kwenye shughuli zao ikiwepo uongozi unaowasimamia.

Wadau wa utamaduni na sanaa waliohudhuria warsha iliyoandaliwa na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyofanyika Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam.
"Wasanii hawafiki kwenye programu hizi na kuwatuma wasimamizi wadogo wadogo. Ndiyo maana hatusongi mbele kwa sababu ya asili ya wasanii wetu hawataki kukabidhi kazi zao kwa menejimenti zao,"amesema Msigwa.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania (TCAF), Nyakaho Mahemba amesema wameshatoa mafunzo kwa wasanii 11984 katika mikoa 18 kwa miaka miwii ya fedha ya mwaka 2023/24 na 2024/25.
"Malengo ya kutoa mafunzo ni katika kuwasaidia walengwa kufanya kazi zao za sanaa na kuibua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta hii ya utamaduni na sanaa hii itatusaidia kufanyia kazi mapungufu," amesema Nyakaho.
Amesema wasanii wanashindwa kuweka kumbukumbu ya mapato yao,kusimamia miradi yao na kushindwa kuweka akiba ya mapato yao na kutofahamu haki zao wanapoingia mikataba ya kazi.
Kwa upande wake, Meneja wa wasanii wa singeli, Masoud Kandoro amesema changamoto iliyopo ni wasanii hawana kipato cha uhakika ambapo mapato yao wanapata kupitia shoo ambazo zinakuwa za msimu.
"Mapato ya msanii yanabadilika kutokana na msimu unakuta kipindi hiki anaweza kupata pesa nyingi. Na wakati mwingine hakuna shoo hivyo pesa haitakuwepo hata kama ameweka akiba anaenda kuchukua pesa zake zote,"amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na wadau wa Utamaduni na Sanaa kwenye warsha iliyofanyika Makumbusho ya Taifa, Jijini Dar es Salaam
Mbali na hilo, amesema baadhi ya wasanii wametoka kwenye sekta isiyo rasmi hivyo hawana rasilimali ya maarifa na wanaweza kupata mkopo lakini elimu ikawa tatizo ya kuendeleza huo mkopo na kujikuta wanapoteza.
"Nitolee mfano wasanii wa singeli wamefungua email (barua pepe) kwa sababu ya kuingia kwenye mitandao ya kijamii. Lakini sio kwa ajili ya kutumiwa kitu na kukisoma na ikitokea umefanya hivyo ujue ni wazi ujumbe huo umepoteza,"amesema.

Msanii wa muziki wa Hip Pop, Farid Kubanda maarufu Fid Q ameshiriki kwenye warsha ya wadau wa utamaduni na sanaa iliyofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam.
Pia, amesema benki hazimtambui msanii kwa sababu ya kutokuwa na dhamana isiyohamishika ambapo walikuwa wanauwezo wa kutumia hati miliki zao kuwa dhamana wanapohitaji mkopo.
Msanii wa filamu nchini, Lumole Matovolwa maarufu Kobisi amesema warsha hii ipo kwa ajili ya kukumbushana na kufundishana kwa yale ambayo walikuwa hawayajui kwani mfuko ni jukumu lao kuwapa elimu.
"Ila kikubwa ambalo ni muhimu kwetu wasanii kuwepo kwa wahusika wa bima ya afya. Hili limekuwa ni changamoto kwetu inapotokea mtu amepata tatizo la kiafya, tunaanza kuchangishana lakini kueleza kuwa waweke bando maalumu kwa ajili ya wasanii kama ilivyo kwenye makundi ya watoto na wazee itatusaidia," amesema Kobisi.