Msanii Cassie aibua mazito akitoa ushahidi kesi ya P Diddy

Muktasari:
- Akiwa amevalia blauzi ya mikono mirefu ya rangi ya zambarau, alizungumza kwa sauti ya chini huku akionekana kuwa na mimba kubwa. Mara kadhaa alipumua kwa shida kutokana na kulia wakati wa kutoa ushahidi huo
Marekani. Msanii Casandra “Cassie” Ventura aliyewahi kuwa mpenzi Sean “Diddy” Combs jana Mei 13,2025 alitoa ushahidi dhidi ya kesi zinazomkabili Diddy huku mrembo huyo akieleza jinsi alivyoteseka kisaikolojia na kimwili kwa miaka 11.
Akiwa amevalia blauzi ya mikono mirefu ya rangi ya zambarau, alizungumza kwa sauti ya chini huku akionekana kuwa na mimba kubwa. Mara kadhaa alipumua kwa shida kutokana na kulia wakati wa kutoa ushahidi huo.
Msanii huyo alianza kutoa ushahidi wake mwanzoni kabisa mwa uhusiano wake na Diddy ambapo alieleza kuwa walikutana wakati yeye akiwa na umri wa miaka 19. Huku Combs akiwa na 38 kwa wakati huo, ambapo alimpa mkataba wa kutoa albamu 10 chini ya lebo yake, 'Bad Boy Records'. Licha ya mkataba huo Ventura alifanikiwa kutoa albamu moja pekee.

Alieleza kuwa kwa wakati huo hakuwa na uzoefu wala kumtamkia neno hapana zaidi ya kuvutiwa na Combs kutokana na ucheshi wake. Alianza kushiriki mapenzi na Diddy wakati alipofikisha miaka 22 na ndipo alianza kunyanyaswa kingono na msanii huyo.
Alisema Diddy alimueleza namna anavyofurahia kuwatazama wengine wakifanya tendo la ndoa. Ndipo Cassie aliamua kufanya atakacho mpenzi wake kwa lengo la kumridhisha.
Hatimaye, Diddy alianza kumpa maagizo ya kupanga vitendo hivyo ambavyo vilihusisha kuajiri wanaume wengine kufanya nao mapenzi na kupanga vyumba vya hoteli kwa ajili ya tukio hilo.
Ventura aliendelea kutoa ushahidi akiweka wazi kuwa matukio hayo yalikuwa yakifanyika mara moja kwa wiki huku tukio refu zaidi analolikumbuka lilidumu kwa siku nne. Alipewa dawa za kulevya ili aweze kufanya kwa muda mrefu kwa ajili ya Diddy na baada ya hapo, alilazimika kupumzika kwa siku kadhaa kutokana na kukosa usingizi na upungufu wa maji mwilini.
Mwanadada huyo aliendelea akisema hakutaka kufanya ngono na watu asiowajua lakini alifanya kwa ajili ya furaha ya Diddy na hakuwa na chaguo kutokana na rapa huyo kumrekodi video wakati wa kufanya vitendo hivyo na aliogopa kusambaza mitandaoni.
Kwa muda mrefu Ventura alisema alianza kuona upande wa ukatili wa Diddy ambapo alianza kumshambulia kimwili vurugu hizo zilizomuachia majeraha mbalimbali kama vile michubuko, macho yaliyovimba na uvimbe kwenye paji la uso.
Akiendelea kueleza kuhusu matukio ya kufanya ngono na wanaume wengine aliwaonesha majaji picha za baadhi ya watu hao na kuthibitisha majina yao pamoja na jinsi walivyoajiriwa.
Akiwataja kwa majina kama Johnny, Latin Men, Jules mwingine akijulikana kama The Punisher. Kulingana na Ventura, Diddy alipendelea wanaume weusi waliokuwa na maumbile makubwa.
Ventura alisema alikuwa akiandikisha vyumba vya hoteli kwa jina bandia “Jackie Star,” huku Combs akitumia majina bandia kama “Frank Black” au “Frank White.” akizungumza kuhusu mafuta ya watoto Ventura alieleza kuwa Diddy alipenda kutumia mafuta hayo kwa wingi mara nyingine hadi chupa 10 kubwa pamoja na vilainishi vingine.

Alieleza kuwa matukio hayo mara kwa mara yaliharibu vyumba vya hoteli, ikiwemo mashuka kuchafuka kwa mafuta na damu kwani alilazimishwa kushiriki vitendo hivyo hata wakati wa hedhi.
Ushahidi wake unatarajiwa kuendelea wiki nzima, huku mawakili wa upande wa utetezi wa Diddy wakitarajiwa kumuhoji kwa kina siku zijazo.