Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mijadala muziki wa singeli, waasisi waeleza chimbuko lake

Muktasari:

  • Ni kauli iliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi Desemba 16,2024  alipokuwa  akipokelewa rasmi katika Ofisi za wizara hiyo, jijini Dodoma.

Dar es Salaam. “Nataka tuweke nguvu kwenye muziki. Kwanza muziki huu ambao ni wa aina yake singeli, leo ikipigwa Brazil, Peru, na India ina mridimo na msisimko wa aina yake kwa wale Waafrika maelfu na mamilioni waliochukuliwa kama watumwa,”.

Ni kauli iliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi Desemba 16,2024  alipokuwa  akipokelewa rasmi katika Ofisi za wizara hiyo, jijini Dodoma.

Kauli hiyo ilizua maswali  kutokana na aina ya uimbwaji na maneno yanayotumika kwenye muziki huo, huku kwa baadhi wakiiona kama faraja ya kuufikisha mbali zaidi.

Licha ya hayo kauli hiyo ilipewa uzito tena baada ya waziri Kabudi alipokuwa akiwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26. Bungeni, jijini Dodoma Mei 7, 2025 aliposema muziki wa singeli upo mbioni kutangazwa rasmi kuwa sehemu ya Orodha ya Urithi wa Dunia.

Ni singeli hiyohiyo ambayo awali waimbaji na wachezaji wake wote walionekana wahuni na wasio na maadili kwa jamii. Lakini kwa sasa ni kati ya kivutio kikubwa nchini hasa kutokana na aina yake ya midundo.

Akielezea historia ya muziki wa singeli, Selemani Msonjele ‘Msaga Sumu’ anasema  muziki huo umetokana na vigodoro na ngoma za asili.

“Huu muziki ni wa Kitanzania chimbuko lake ni hapa hapa na umetokea kwenye asili ya vigodoro, enzi hizo pamoja na ngoma za asili. Kadiri siku zinavyokwenda unabadilika mfano zamani ulikuwa sio wa kasi, ulikuwa unapigwa taarabu. 

“Sisi tunachukua biti tupu ya taarabu tunaingizia maneno yetu lakini kwa sasa, vizazi vipya vinazidi kuja muziki huo unabadilika,”anasema Msaga Sumu ambaye ni kati ya waasisi wa muziki huo

Anasema muziki huo unachukuliwa wa kihuni kutokana na kukubalika na vijana wengi.

“Muziki ulikuwa unachukuliwa wa kihuni kutokana na ulipotokea. Umetokea uswahilini zamani muziki huu ulipokuwa unapigwa sehemu yoyote waliokuwa wanahudhuria wengi ni vijana wa kike na kiume ndio maana unaambiwa ni wa kihuni, lakini muziki huu hauna uhuni wowote.

“Napokea maoni mengi naona ni mazuri watu wengi wanaukubali. Kwa sababu umekuwa gumzo kuanzia serikalini na viongozi wake, unaona kabisa wanavyoufurahia. Lakini bado kuna watu wanataka kuukwamisha ili uonekane huu muziki ni wa kihuni,”anasema Msaga Sumu

Mbali na  Msaga Sumu, Mrisho Kulwa ‘Dj Mrisho’ ambaye pia ni kati ya waasisi wa muziki huo amewahi kueleza kuwa  awali walikuwa wakiufanya muziki huo kwa kupenda bila kujua baadaye utaleta mafanikio.

“Zamani wakati naanza kuurekodi ilikuwa wanaoimba muziki huu ni wachache Msaga Sumu, Khalid Kapala, Majid Bigoma hao ni wasanii wa zamani ambao tulikuwa tunafanya nao na tulienda mpaka chimbuko la wasanii wengine wakaanza kuja,”anasema

Anasema singeli ni biti inayokimbia kwa sasa wanaita bakora na muziki unaoenda taratibu unaitwa ladha.

“Kuna kijana alikuwa anaitwa Dulla Six Bullet  ni msanii anayeimba nyimbo za haraka, alikuwa na dansa wake anaitwa Kisingeli. Alikuwa akipanda jukwaani kuimba anamuita Kisingeli njoo.

“Na yule alikuwa akipanda pale anacheza style zake pale jina liliondoka watu wakaanza kuuita muziki kisingeli lakini hilo ni jina la mtu. Zamani tulikuwa kama tuna ukanda wasanii wa Tandale walikuwa wakiimba muziki wa taratibu kina Msaga Sumu  lakini wa Mburahati waliimba wa  haraka na hao waasisi walikuwa Makaveli, Dulla Six Bullet hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 2005 , 2007, “anasema.

Utakumbuka  hivi karibuni singeli iliibua mjadala bungeni baada ya Waziri Kabudi kuutaja tena kwa mara nyingine. Kati ya waliotoa maoni katika hoja hiyo  iliyowasilishwa Bungeni ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Jesca Msambatavangu.

“Ninaomba sana kuwepo na mjadala wa kitaifa kukubaliana kama singeli itakuwa ndio mchezo au utamaduni wa taifa letu, kwa nyimbo zake, maneno yake, uvaaji wake, uchezaji wake. Je tutakubaliana kwa kuwa ni suala la kitaifa basi ni vizuri tukubaliane kwa pamoja.

“Tunakubaliana singeli ndio ituwakilishe Watanzania na juzi nilituma kitu fulani kwenye group la wabunge. Michezo ile inavyochezwa wakati mwingine kama nyinyi ndiyo wasimamizi basi muone namna ya kudhibiti na nidhamu,”alisema Jesca.

Aidha aliongezea “Maneno yanayotamkwa, uchezaji wake wana mihemko wanacheza hiyo singeli wako uchi wananing’inia kwenye daladala. Kwenye matamasha mbalimbali wanavaa nguo ambazo nyingine zinaonyesha kabisa,”

Hata hivyo, baada ya hoja hizo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma (Mwana FA) alisema muziki wa singeli umewatengenezea vijana wengi ajira.

“Ninachotaka kusema ni kwanza hakuna mtu yeyote aliyesema mahali popote kwamba tunataka kuufanya singeli kuwa muziki wa taifa. Kilichotokea  singeli kama muziki ambao umetoka mtaani umejipigania wenyewe, ukifanywa na vijana wadogo ambao wametengeneza ajira za moja kwa moja.

“Mimi binafsi nimewahi kwenda kwenye maonesho ya singeli nje ya nchi na muziki huu umekuwa unafanya vizuri sana. Ukweli ni kwamba hakuna mtu yeyote kutoka sehemu nyingine duniani anayeweza kuja kudai kwamba singeli ina asili kutoka nchini kwao kimsingi singeli ina asili kutoka Tanzania.

“Tulichofanya tulikuwa tunajaribu kuwasaidia vijana hawa ambao wamejitengenezea ajira ili kuhakikisha tunawasaidia kuubrandi, kuupakeji na kupromoti muziki huu na wakati tunafanya hivyo tuwasaidie kuusafisha muziki wa singeli,”alisema 

Aliongezea kwa kusema  kama ni suala la uhuni upo kwenye aina zote za muziki duniani.
 
“Uhuni ambao unasemwa katika singeli naamini na mimi nikiongea kama mwanamuziki najua kwamba upo katika miziki yote. Na vijana hawa wanahitaji maelekezo na sio kususwa kama ambavyo tumekuwa tunasema kwa ukali,”alisema FA.