Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfumo unamgharimu kuwika zaidi kimataifa

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Diamond, tasnia ya muziki Nigeria imekuwa haimpi heshima anayostahili kutokana na ukubwa wa jina lake Afrika, ila sasa kwa jinsi Komasava inafanya vizuri wenyewe wamejikuta wakikubali yaishe

Dar es Saalam, Wameingia kwenye mfumo!. Ni kauli aliyoitoa staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz baada ya wimbo wake ‘Komasava’ kubamba sehemu nyingi duniani ikiwemo Nigeria ambapo wasanii wake wamekuwa wakifanya vizuri kwa miaka.

Kwa mujibu wa Diamond, tasnia ya muziki Nigeria imekuwa haimpi heshima anayostahili kutokana na ukubwa wa jina lake Afrika, ila sasa kwa jinsi Komasava inafanya vizuri wenyewe wamejikuta wakikubali yaishe.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba kuna eneo moja ambalo linamtofautisha Diamond na washindani wake kimuziki Afrika hasa kutokea Nigeria kama vile Davido na Burna Boy ambao wamewahi kufanya nao kazi miaka ya nyuma.

Nalo ni namna ambavyo wanaandaa kazi zao, kuzitoa na walengwa hasa wa kazi hizo, katika eneo hilo, Diamond amebeba mzigo mkubwa ukilinganisha na wenzake na hapo ndipo wanamzidi kimauzo na hata shoo za kimataifa. Kivipi?

Katika ujumbe wake wa Januari 21, 2023, Diamond alitangaza kuwa mwaka huo angefanya mambo makubwa katika muziki kama ndiyo ametoka leo kimuziki na kuwahakikishia mashabiki wake watafurahi.

“Mawe ya Kibongofleva, Kiafrika na Dunia. Nyimbo za mapenzi, maisha, maumivu na starehe. Video za ndani, Afrika na Dunia. Ni mwaka wa tasnia na Taifa kujivunia kuwa na kiumbe kinaichoitwa Nasibu Abdul, Diamond Platunumz, Simba.” alisema Diamond.

Ukichukua kauli hiyo ya Diamond, utaona kuna mgawanyiko wa makundi matatu katika kuachia nyimbo zake, kuna nyimbo zinazolenga soko la Tanzania (Bongofleva), Afrika na Dunia (kimataifa zaidi).

Kwa lugha rahisi, ukimsikia Diamond ametoa nyimbo na Ne-Yo (Marry You), Morgan Heritage (Hallelujah), Omarion (African Beauty) Rick Ross (Waka), hapo analenga zaidi soko la kimataifa, haya ndio anaita mawe ya kidunia.

Akiachia ngoma na Tiwa Savage (Fire), Koffi Olomide (Waah!), Focalistic (IYO), P-Square (Kidogo), Teni (Sound), Mr. Flavour (Nana), Fally Ipupa (Inama), Rema (Gimmie), ujue analenga soko la Afrika ambalo kwa kiasi kikubwa limetawaliwa na wasanii wa Nigeria.

Na ukimsikia Diamond anaimba nyimbo kama Zuwena, Mapoz, Sikomi, Yatapita, Baba Lao, Haunisumbui, Nawaza, Chitaki, Naanzaje, Kanyaga n.k, ujue hapo analenga soko la ndani zaidi, yaani kwa ajili ya watu wake wa Tandale, hizi ndizo wanazielewa zaidi.

Hata video za makundi hayo matatu zinatofautiana sana, mfano video za nyimbo alizoshirikiana na wasanii kama Ne-Yo, Omarion, Rick Ross na Morgan Heritage, zote zimefanyika nje ya nchi na kusimamiwa na waongozaji wa kimataifa wenye uwezo na uzoefu zaidi.

Hii ni tofauti sana na wasanii kama Wizkid, Burna Boy na Davido, wao wanaamini kazi yao moja tu inaweza kukidhi mahitaji ya maeneo yote matatu, yaani Burna Boy akitoa wimbo wake ‘Last Last’ ni kwa ajili ya watu wake wa Nigeria, Afrika na duniani kwa ujumla.

Wizkid akitoa ngoma zake kama ‘Joro’, ‘Essence’, ‘Daddy Yo’ na ‘Final’ au Davido akitoa ngoma zake kama ‘Fall’, ‘Assurance’, ‘If’ na ‘FIA’, hizi ni kwa ajili ya Nigeria, Afrika na dunia nzima.

Ikumbukwe katika nchi kama Marekani, wasanii wengi wakubwa wanapotoa nyimbo siyo kwa ajili ya Marekani au Amerika Kaskazini tu, bali wanaamini kwa ajili ya dunia nzima (global release) na hutambulisha hivyo mara zote.

Ila ni vigumu kwa Diamond kuachia aina ya nyimbo kama ‘Marry You’, ‘Sound’, ‘African Beauty’ na ‘Hallelujah’ tu, akifanya hivyo tayari soko la ndani amelipoteza maana mashabiki wake wa Tandale hawaelewi sana nyimbo hizo kutokana na kuimbwa kwa lugha ngeni.

Wakati ameachia EP yake, First of All (2022), Diamond alisema alipanga kuweka nyimbo za kimataifa tu kama ‘Fine’, ‘Wonder’, ‘Sona’, ‘Somebody’ na ‘Loyal’, ila akakumbuka kuna soko lake la ndani ataenda kulikosa ndipo akaweka nyimbo kama ‘Mtasubiri’, ‘Nawaza’ na ‘Oka’.  

Ushawahi kujiuliza kwa nini kina Burna Boy na wasanii wengine wakubwa duniani wakitangaza ziara za dunia (world tour) unaweza kukuta wanapita kwenye mabara ya Amerika na Ulaya tu wakati kuna mabara mengi kama Asia, Afrika na Australia?.

Hiyo ni kutokana wanaamini kazi zao zinawafikia watu wote duniani, hivyo wanaohudhuria shoo zao katika maeneo machache wanayopita ni watu kutokana sehemu nyingi duniani.

Kwa mfano Davido, BTS, Beyonce, Bad Bunny, Ed Sheeran au Justin Bieber akitumbuiza 02 Arena, Uigereza au Madison Square Garden, Marekani, anaamini watakaohudhuria siyo wa nchi hizo pekee, kutakuwa na watu kutoka Afrika, Ulaya, Asia, Amerika na Australia, hii ni moja wapo ya sababu ya kuita ziara zao za kidunia.