Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa Bongo katika mtihani wa Kariakoo Derby

Muktasari:

  • Baadhi ya mastaa wa muziki na filamu Bongo, hapo watajikuta katika mtihani pindi Simba na Yanga zitakapokutana katika dabi ya Kariakoo ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania 2024/25 utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. 

Dar es Salaam. Baadhi ya mastaa wa muziki na filamu Bongo, hapo watajikuta katika mtihani pindi Simba na Yanga zitakapokutana katika dabi ya Kariakoo ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania 2024/25 utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. 

Mastaa hao ni wale wanaoshabikia timu hizo na hata kutumbuiza katika matamasha yao ambayo yamekuwa yakivutia idadi kubwa ya watu kila mwaka kutokana na burudani na ubunifu unaopatikana ndani yake. 

Ni kwa namna mbili dabi ya Kariakoo inawapa mtihani, mosi, ni wale mastaa ambao wapo katika uhusiano wa kimapenzi lakini kila mmoja ana timu yake, pili, ni wale ambao wana uhasama wa kikazi ila wanashabiki timu moja. 


1. Mtihani wa uhusiano  

Mitindo ya maisha ya mastaa hasa upande wa uhusiano ni miongoni mwa mambo yanayowavutia mashabiki wao huku wenyewe wakiyatumia kusukuma mbele kazi zao ila kila mmoja ana chaguo lake katika dabi ya Kariakoo kitu ambacho kesho ni mtihani kwao. 


A. Diamond (Yanga) & Zuchu (Simba) 

Mastaa hawa kutokea WCB Wasafi licha ya kupenda sana leo wana mtihani wa kuweka mapenzi yao pembeni na kumuombea mwenzake kushindwa katika dabi ya Kariakoo ambapo Diamond Platnumz yupo Yanga huku Zuchu akiwa Simba. 

Wawili hao ambao wameshirikiana katika nyimbo tatu, Litawachoma (2020), Cheche (2020) na (Raha), awali wote walikuwa mashabiki wa Simba ila Diamond akaja kuhamia Yanga, timu anayoishabikia pia mama yake mzazi, Bi. Sandra au Mama Dangote. 

B. Marioo (Yanga) & Paula (Simba) 

Mwimbaji kutokea Bad Nation, Marioo ameshatoa nyimbo mbili kwa ajili ya timu yake ambazo ni Yanga Anthem (2022) na Yanga Mabingwa (2023) lakini mpenzi wake na mzazi mwenzie, Paula sio shabiki wa nyimbo hizo wala timu hiyo. 

Paula ambaye ameonekana katika video tatu za nyimbo za Marioo, Lonely (2023), Tomorrow (2023) na Sing (2023), ni shabiki wa Simba na alishawahi kuwa miongoni mwa waliotambulisha jezi za timu hiyo, hivyo dabi hii inaweka yote waliyofanya pamoja pembeni. 


C. Rich Mitindo (Simba) & Wolper (Yanga) 

Mume wa muigizaji Jacqueline Wolper, Rich Mitindo ambaye ni mbunifu maarufu wa mavazi ni shabiki wa kutupwa wa Simba, huku Wolper mwenyewe akiwa upande wa Yanga kwa miaka yote tangu amepata kujulikana kupitia filamu na mitindo. 

Hivyo dakika 90 za leo pale Lupaso zinaenda kuwapa mtihani wawili hao ambao walifunga ndoa hapo Novemba 2022 katika Kanisa Katoliki la St. Peter's Oysterbay, Dar es Salaam, na sasa tayari wakiwa wamejaliwa watoto wawili, Pascal (2021) na Min (2022).  


D. Whozu (Simba) & Wema (Yanga) 

Mwimbaji Whozu kutokea Too Much Money aliyevuma na kibao chake, Huendi Mbinguni (2017), hakuna asiyejua mapenzi yake kwa Simba akiwa tayari ameitolea nyimbo mbili, Simba ni Noma (2021) na Simba Yetu (2022), huku zote akizitumbuiza Simba Day. 

Hata hivyo, mpenzi wake Wema Sepetu, Miss Tanzania 2006 na staa wa filamu ni shabiki wa Yanga, kwa hiyo dabi ya Kariakoo inaenda kusambaratisha kwa muda mapenzi ya wawili hao ambao walishirikiana katika video ya wimbo, Ameyatimba (2023). 


2. Mtihani wa bifu 

Upande huu ni ule wa mastaa wa muziki ambao wana uhasama wa kikazi kutokana sababu mbalimbali ila katika dabi ya Kariakoo wanashabikia timu moja, hivyo mtihani wao ni kuungana kuiombea dua timu yao au kuendelea na uhasama wao. 

A. Nandy Vs Ruby (Yanga)

Kwa miaka yote ya umaarufu hawapikiki chungu kimoja licha ya wote kukulia Tanzania House of Talent (THT), kwa mujibu wa Nay wa Mitego kupitia wimbo wake, Moto (2017), Nandy alitengenezwa ili kumshusha Ruby kimuziki kitu kinachofanya kutoelewana. 

Hata hivyo, Ruby, mchezaji wa zamani wa Young Twiga Star ni shabiki wa Yanga sawa na Nandy aliyekabidhiwa kadi ya uanachama na Rais wa timu hiyo, Injinia Hersi Said siku ya harusi yake, hivyo dabi hii ni wao kuchagua bifu au kuungana. 


B. Afande Sele Vs Soggy Doggy (Simba) 

Ndani ya Bongo Records, Soggy Doggy alihusika kutayarisha wimbo wa Afande Sele, Darubini Kali (2003) lakini walikuja kutibuana baada ya Afande kudai kuna wimbo waliutoa ukiwa na mixing mbovu ila P-Funk Majani alipomuuliza akakanusha. 

Kwa mujibu wa Soggy Doggy, hilo lilitaka kumgombanisha na Majani na huo ukawa mwanzo wa uhasama wake kimuziki na Afande Sele ingawa sasa mambo ni shwari kiasi, na wote hawa ni mashabiki wa Simba, bingwa mara 22 wa Ligi Kuu Tanzania. 


C. Madee Vs Nay wa Mitego (Yanga) 

Tatizo la wawili hawa wanaotokea Manzese, kila mmoja anaona anafaa kuwa rais wa mwenzake, Madee akijiita rais wa Manzese, huku Nay wa Mitego akijitambulisha kama Rais wa kitaa, ila wote ni wananchi wa mitaa ya Twiga na Jangwani. 

Ikumbukwe awali waliongoza kambi zao, World Camp Nakoz (Madee) na Small Tiger (Nay) katika mnyukano wao hadi kuja kuishika vilivyo Bongofleva lakini leo hii katika dabi ya Kariakoo wataweka tofauti zao pembeni kwa ajili ya Yanga., bingwa mara 30 wa Ligi. 


D. Roma Vs Roma (Simba)

Wakali hawa wa Hip Hop walionekana kutokuwa sawa kutokana na kunyukana katika nyimbo zao, mathalani Roma katika wimbo wake, 2030 (2013) anasema, 'Hata Pacho ni mwamba ila bado anakata viuno, kaskazini bila Tanga ni Msondo bila Gurumo'. 

Hivyo alimlenga Joh Makini ambaye hujiita Mwamba wa Kaskazini, ila licha ya bifu lao la kikazi wawili ambao wamewahi kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wasanii Bora wa Hip Hop, wote ni mashabiki wa Simba, hivyo dabi hii ya Kariakoo wapo pamoja.