Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majanga yamuandama Kanye West

Muktasari:

  • Mambo yanazidi kumwendea kombo rapa maarufu duniani, Kanye West baada ya msanii mwenzake, Kid Cudi kutangaza kuwa hatafanya naye tena kazi baada ya kushirikiana naye katika kibao cha "Rock N Roll".

Mambo yanazidi kumwendea kombo rapa maarufu duniani, Kanye West baada ya msanii mwenzake, Kid Cudi kutangaza kuwa hatafanya naye tena kazi baada ya kushirikiana naye katika kibao cha "Rock N Roll".

Wimbo huo uko katika albamu ya rapa mwingine, Pusha-T inayosubiriwa kwa hamu na inayokwenda kwa jina la "It’s Almost Dry". Albamu ya "It’s Almost Dry" imetayarishwa na Kanye West na rafiki yake mwingine, Pharrell Williams na inatoka Ijumaa hii.

Katika akaunti yake ya Twitter, Kid Cudi ameandika ujumbe huo kuwataarifu mashabiki wake kuwa wimbo huo ni wa mwisho kufanya kazi na West, ambaye anaonekana kusumbuka tangu mkewe wa zamani, Kim Kardashian aanze mahusiano na mchekeshaji Pete Davidson.

"Hey! Kwa hiyo baadhi yenu umesikia kuhusu wimbo niliofanya na Pusha. Nilifanya wimbo huo mwaka mmoja uliopita wakati mambo yakiwa safi na Kanye," Cudi, ambaye jina lake halisi ni Scott Mescudi aliandika jana (Jumanne).

"Siko sawa na huyo mtu. Si rafiki yangu na niliruhusu wimbo kwa ajili ya Pusha kwa sababu ni mtu wangu.

"Huu ni wimbo wa mwisho mtasikia nikiwa na Kanye," alisema na kumaliza kwa kuandika jina lake halisi chini la Scott.

Awali Cudi alisaini mkataba na lebo iliyoanzishwa na West ya GOOD Music na kuwemo katika nyimbo kadhaa za albamu ya "Stronger" ya Kanye West.

Wawili hao walishirikiana kutoa albamu mwaka 2018 iliyoitwa "Kids See Ghosts".


Baada ya hapo, wawili hao walitengana kutokana na maneno ambayo West, ambaye anatumia jina la Ye, alikuwa akiyatuma mitandaoni.

Hali hiyo inatokana na West kubaini kuwa Cudi ni rafiki wa Davidson ambaye ana uhusiano na Kim kwa muda mrefu sasa.

West alitangaza kuwa Cudi hatasikika tena katika albamu ya Donda 2.

“Kwa hiyo kila mtu anajua kuwa Cudi hatakuwemo ndani ya Donda kwa sababu ni rafiki yako unayemjua nani,” West aliandika Instagram lakini ujumbe huo sasa umefutwa.

Cudi akamjibu Twitter akisema: “Mbaya sana, sitaki kuwa kwenye albamu yako wewe dinasauria, hahaha... Kila mtu anajua nimekuwa kitu kizuri katika albamu zako tangu nikufahamu. Nakuombea kaka... Tulizungumza wiki kadhaa zilizopita kuhusu hili. Unajaribu kupindisha mambo na kuandika uongo kwenye internet ili uonekane. Wewe si rafiki yangu, bye.”

Baadaye West akaandika tena Instagram akisema: “Nilitaka rafiki yangu ajue, kisu kimeingia ndani sana,” alisema akiwepo picha ya zamani inayomuonyesha West, Cudi, Davidson na Timothee Chalamet huku akiweka alama ya ‘X’ usoni mwa Davidson.

Mgogoro umekuwa chinichini baina ya wawili hao. Mwaka 2016, Cudi aliandika Twitter kumnanga West (na Drake) kwa kudai kuwa ni wanamuziki wakubwa na kuongeza maneno "wakati wana watu 30 wanaowaandikia nyimbo”, na Kanye West akajibu kw amaneno ya dharau. Baadaye walisameheana na kukumbutiana jukwaani mwaka 2017 wakati West akitumbuiza.

Tukio hilo ni jipya miongoni mwa matukio mengi yanayomuandama West, rapa tajiri aliyeingia katika mbio za urais mwaka jana.

West alitazamiwa kutumbuiza katika tamasha la Coachella lakini akaondolewa mapema mwezi huu. Pia alipangwa kutumbuiza katika tuzo za Grammy mwaka huu, lakini akaondolewa kutokana na tabia zake.

Mapema mwezi Machi, CNN imeandika, alizuiwa kutuma chochote Instagram kwa saa 24 kutokana na kutumia maneno mabaya dhidi ya mchekeshaji  Trevor Noah.