Kwa hili, bila Wizkid hakuna Diamiond

Muktasari:
- Hata hivyo, ukweli ni kwamba hatuwezi kuzungumzia mafanikio ya wimbo huo bila kumtaja msanii wa Afrobeats kutokea Nigeria, Wizkid ambaye ni mshindi wa Grammy 2021 kupitia wimbo wa Beyonce Knowles, Brown Skin Girl (2019).
Dar es Salaam. Ni miaka mitano imepita tangu Diamond Platnumz kutoa wimbo wake, Jeje (2020) unaoendelea kufanya vizuri na kumpa heshima ya kipekee staa huyo wa Bongofleva na mwanzilishi wa WCB Wasafi iliyowatoa wakali kibao kama Harmonize na Zuchu.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba hatuwezi kuzungumzia mafanikio ya wimbo huo bila kumtaja msanii wa Afrobeats kutokea Nigeria, Wizkid ambaye ni mshindi wa Grammy 2021 kupitia wimbo wa Beyonce Knowles, Brown Skin Girl (2019).
Utakumbuka Wizkid alivuma zaidi Afrika baada ya kuachia wimbo wake ‘Holla at Your Boy’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Superstar (2011) iliyotoka miaka miwili baada ya kusainiwa na Banky W’s Empire Mates Entertainment (E.M.E).

Sasa baada ya Diamond kutoa video ya wimbo, Jeje (2020) iliyoshutiwa huko Zanzibar na Director Kenny chini ya Zoom Extra, ilipata mapokezi mazuri na kuweka rekodi ambazo hadi sasa nyimbo zake nyingi zimeshindwa kuifikia.
Mathalani ndio video ya muziki iliyofanya vizuri zaidi YouTube barani Afrika kwa mwaka 2020 akitazamwa zaidi ya mara milioni 41.6, ikifuatia na ‘Duduke’ yake mwimbaji wa Nigeria, Simi ambayo ilitazamwa zaidi ya mara milioni 28.8.
Lakini pia video hiyo ya Simi, mshindi wa tuzo saba za The Headies, ilikarabiwa sana na nyingine ya Diamond, nayo ni Waah! (2020) akimshirikisha Koffi Olomide kutokea DR Congo ambayo nayo ilifikisha milioni 28.8 na sasa ina milioni 175.
Hapo Agosti 2024 Jeje iliweka rekodi kama wimbo wa kwanza alioimba Diamond peke yake (solo) kwa video yake kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, mtandao wa kucheza video ulioanzishwa Februari 14, 2005, huko San Mateo, California, Marekani.

Ikumbukwe hadi sasa Diamond ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki mwenye video nyingi zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, anazo tano ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Jeje (2020 na Nana (2015).
Lakini kati ya hizo ni Jeje tu ndio kaimba mwenyewe, hizo nyingine ameshirikiana na Innoss’B, Koffi Olomide na Fally Ipupa wote wakitokea DR Congo, pia ameshirikiana na Mr. Flavour wa Nigeria.
Jeje ulikuwa wimbo wa pili Bongo wa mwanamuziki solo kufanya hivyo baada ya ule wa Zuchu, Sukari (2021) ambao Machi 2024 ilifanya hivyo, na huu pia video yake iliongoza Afrika mwaka 2021 ikitazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 60.
Wimbo huo Jeje ambao ulitoka rasmi Machi 21, 2020 kwa kiasi imechukua vitu kutoka kwa ule ya Wizkid ‘Joro’ uliyotoka Septemba 30, 2019, ndio sababu tunasema bila Wizkid hakuna rekodi hizo za Diamond.
Hata hivyo, Sallam SK ambaye ni Meneja wa Diamond na WCB Wasafi kwa ujumla, alisema nyimbo hizo zinafanana kiasi kutokana zote mbili zimetengenezwa na mtayarishaji mmoja, Kelpvibe wa Nigeria.
Ila hata video ya Jeje ambayo mrembo kutoka kisiwa cha Reunion, Malaika Salatis aliinogesha, uchezaji wake na muonekano wake kwa urefu hauna tofauti na mrembo, Georgia Curtis mwenye asili ya Nigeria na Hispania ambaye katokea kwenye video ya Wizkid, Joro.

Malaika ambaye ni mwanamitindo na dansa, fani aliyojifunza tangu akiwa na umri wa miaka 15, kabla ya kukutana na Diamond tayari alishatumbuiza na wasanii mashuhuri kama vile Macklemore na Tiwa Savage, pia alifanya muziki chini ya Warner Music Australia.
Ikumbukwe Diamond pia wimbo wa Diamond ‘Loyal’ kutoka katika EP yake ya kwanza, First of All (2022), umefanana sana na ule wa Wizkid, Essence (2020) akimshirikisha Tems, mshindi wa Grammy mbili kutokea Nigeria pia.
Mtayarishaji S2kizzy alikiri kuwa walipata wazo au hamasa ya kutengeneza wimbo huo kufuatia ‘Essence’ kufanya vizuri zaidi duniani ambapo ilikuja kushinda tuzo zaidi ya 20 ikiwemo BET 2022 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana na pia kuwania Grammy.
Hadi sasa Diamond hajawahi kutoa kolabo na Wizkid licha ya kushirikiana na wasanii wengi wa Nigeria kama Davido, Iyanya, Mr. Flavour, Yemi Alade, Rema, Adekunle Gold, Teni, P-Square na Tiwa Savage, mshindi wa MTV EMAs 2018.