Kusah, Aunty Ezekiel penzi lilianza hivi
Muktasari:
- Ingawa bado hajashinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), Kusah anasifika kwa utunzi mzuri wa nyimbo za mapenzi, kutia moyo na maisha kwa ujumla. Fahamu zaidi.
Dar es Salaam. Ukitaja wasanii wa Bongofleva waliofanya vizuri kipindi cha miaka mitano iliyopita bila kuliweka jina la Kusah, utakuwa umefanya makosa makubwa maana kupitia muziki wake ametengeneza mashabiki wengi ndani ya muda huo.
Ingawa bado hajashinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), Kusah anasifika kwa utunzi mzuri wa nyimbo za mapenzi, kutia moyo na maisha kwa ujumla. Fahamu zaidi.
1. Jina la ‘Kusah’ analolitumia katika muziki, ni la babu yake mzaa baba. Kipindi anaanza kusaka nafasi ya kutoka kimuziki, aliwahi kushauriwa alibadilishe jina hilo lakini akaamua kuendelea nalo hadi alipopata umaarufu.
2. Tangu akiwa shuleni Kusah alipenda muziki kiasi kwamba wakati akiwa na darasa la tano huko Bumbuli, Tanga, alichaguliwa kuandika wimbo wa shule ambao ulipitishwa kutumika rasmi.
3. Alipoamua kujikita rasmi katika muziki alianza kuwatafuta wasanii wakubwa ili kuwaandikia nyimbo na fedha ya kwanza kubwa kulipwa kwa kuandika wimbo ilikuwa Sh50,000.
4. Kipindi cha uhusiano wake na Ruby, ndipo Kusah alimwandikia wimbo wake maarufu, Ntade (2018) ambao ulifanya vizuri sana na kumrudisha Ruby katika muziki baada ya ukimya mrefu uliotokana na changamoto nyingi.
Pia walifanikiwa kutoa nyimbo tatu pamoja ambazo ni Chelewa (2018), Kelele (2019) na Nadondosha (2019). Baada ya nyimbo hizo ukawa mwisho wa penzi lao wakiwa tayari wamejaliwa kupata mtoto mmoja.
5. Baada ya wimbo wake, I Wish (2021) kupata mapokezi mazuri, bei ya Kusah katika soko ilipanda ghafla na kuanza kufanya show kuanzia Sh5 milioni, fedha ambayo hakuwahi kulipwa hapo awali.
6. Kusah hajawahi kutoa albamu ila ametoa Extended Playlist (EP) mbili, Romantic (2022) na Bumbuli Boy (2025). Hiyo ni sawa na Maua Sama ambaye naye hana albamu bali EP mbili, Cinema (2022) na Sama (2024).
7. Marioo na kundi la Mabantu, mtu wa kwanza kuwakutanisha kwa mara ya kwanza alikuwa ni Kusah na wakati wasanii wote walikuwa bado wanajitafuta kimuziki.
8. Kusah ndiye ameandika wimbo wa Nandy, Nibakishie (2020) akimshirikisha Alikiba ikiwa ni kolabo yao ya kwanza, kisha ikafuta Dah! (2024) ambayo Nandy kaandikiwa na Billnass ambaye pia ni mumewe.
9. Kusah alipokea ujumbe (DM) Instagram kutoka kwa Aunty Ezekiel aliyekuwa anampongeza kwa muziki wake mzuri, basi wakaendelea kuwasiliana katika mtandao huo hadi walipojikuta wapo katika uhusiano na sasa wakiwa na watoto wawili.
Mastaa hao wamekuwa wakishirikiana katika kazi zao, mfano Aunty Ezekiel ndiye amecheza kama mke katika video ya Kusah, I Wish (2021) ambayo imetazamwa zaidi ya mara milioni 19 YouTube ukiwa ni wimbo wake kwanza kufikia rekodi hiyo.
10. Video nyingine za Kusah ambazo Aunty Ezekiel katokea ni Mama Lao (2021) na Blessings (2025) ambayo ni kwa ajili ya mtoto wao wa pili ambaye pia Kusah kamwimbia wimbo, Ukiniita (2025) unaozungumzia kuzaliwa kwake.