Prime
Wanaorejea Chadema wajiandae na hili…
Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob ‘Boni Yai’ amesema wanachama wanaorejea katika chama hicho kutoka vyama vingine wasitarajie kupata vyeo kwa haraka.
Pia, aliwataka wawe wavumilivu na kauli au maneno makali ya wanachama kwa hicho walioumizwa cha kuondoka kwao kwa sababu wakati wanaondoka waliondoka katika kipindi ambacho chama kiliwahitaji zaidi.
Boni Yai anaeleza hayo wakati makada wa Chadema waliohamia vyama vingine wakianza kurejea huku wakipokelewa na kupewa uanachama wa chama hicho katika matawi wanakotokea kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.
Makada hao ni Mchungaji Peter Msigwa aliyekuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Patrick Assenga aliyekuwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) pamoja na Joseph Selasini aliyekuwa amerudi NCCR Mageuzi.
Aidha, kuna tetesi kwamba makundi mengine ya makada wa zamani wa Chadema wako mbioni kurejea ndani ya chama hicho, ingawa bado hazijathibitishwa rasmi.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Boni Yai hivi karibuni, ofisini kwake jijini Dar es Salaam ambapo alizungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa ndani ya chama chake ikiwamo hali ya kisiasa ya sasa nchini.
Boni Yai ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, alisema kurejea kwa makada hao kuna sura tatu; mosi, msimamo rasmi wa kamati kuu bado haujatoka kwamba wajiunge au wasiwapokee.
“Hiki ni chama cha siasa, licha ya kuwa na katiba ya chama, lakini tuna Katiba ya nchi ambayo haitaki ubaguzi. Tunapoongelea tusiwe na ubaguzi maana yake tunaongelea tusiwe na sababu nyingine ya kuzuia mtu asijiunge na chama,” anasema.
Boni Yai anasema sura ya pili ni kwamba kuna waliokihama Chadema na kukitukana au kukishambulia, akisema kurudi kwao si tatizo, lakini maoni ya watu yanaeleza wasiaminiwe kwa haraka na kama walikuwa na nyadhifa kubwa wasirudi katika nafasi hizo.
Jambo la tatu, anasema wakiwapokea wakae kwanza sebuleni, si kuwapeleka chumbani, kama maoni ya wanachama wengi yalivyo. Hata hivyo amewatoa wasiwasi.
“Mfano mzuri ni Mchungaji Msigwa, aliondoka Chadema akiwa jenerali, amerudi hawezi kuwa tena jenerali, atakuwa koplo au askari yule wa chini kabisa hadi pale mwenendo wao utakaporidhisha,” anasema.
Kwa mujibu wa Boni Yai, ili Mchungaji Msigwa awe jenerali tena, kuna michakato ya ndani ya chama ambayo lazima aipitie ikiwemo kujijenga kuanzia kwenye tawi, kata, wilaya, mkoa hadi kanda yake.
“Pia, ataangaliwa uwezo wake, kuongea kwake, ushiriki wake, kujizatiti kwake, uaminifu wake, ndivyo vitakavyomwezesha kurudi kuwa jenerali. Sasa unamzuiaje mtu wa namna hiyo,” anasema Boni Yai aliyewahi kuwa meya wa manispaa za Kinondoni na Ubungo.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai (kushoto) akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwandishi wa Mwananchi, Peter Sekla ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Boni Yai alitolea mfano mwingine wa Assenga ambaye alikuwa mhazini wa Kanda ya Pwani, anayeshiriki vikao vikubwa kikiwamo cha Baraza Kuu la Chadema, akisema amerudi lakini hawezi kuwa na cheo cha awali, bali ataishia kwenye ukoplo.
“Aliondoka akiwa juu, amerudi akiwa chini, maana yake ana kazi ya kufanya katika tawi, jimbo, kata, wilaya, mkoa na kanda, uwajibikaji wake na kujituma, vikimjenga hivi anarudi kuwa juu. Lakini haviwezi vikajengwa kwa siku moja au mbili bali miaka,” anasema.
Anafafanua kuwa Chadema si Serikali kwamba ukirudi unateuliwa, bali unapaswa kupambana ili kupata nafasi za uongozi wa ngazi fulani, akisema haoni shida kwa chama hicho kuwapokea makada wake wa zamani.
Boni Yai amewataka wanaChadema na Watanzania kutokuwa na wasiwasi na baadhi waliokuwa makada wa chama hicho wanaorejea na wanaotaka kurejea, akisema michakato ya ndani ya Chadema ndiyo itakayochuja na kubaini malengo yao.
Wavumilie kauli kali
Wakati huohuo, Boni Yai amewataka wanaorejea na watakaoreja ndani ya Chadema kuwa wavumilivu kwa sababu watakutana na maneno makali ya baadhi ya wanachama wa chama hicho waliochukizwa na kuondoka kwao.
“Watahitaji kupita katika msoto upya, lazima wawe tayari kujizatiti ili kukubaliana na hali hiyo. Usitarajie unarudi Chadema utakuwa na ule ujenerali, uliondoka ukiwa hivyo, ukirudi lazima uwe chini yaani uanzie kwenye ukoplo au usiwe hata na cheo kimoja.
“Wakubaliane na hali hii kwa sababu waliondoka katika kipindi kibaya sana, baadhi waliondoka wakati ambao Chadema kilikuwa kinajadiliwa kife, tulikuwa kwenye dripu. Wengine waliondoka kwa kutaka kuondoa dripu ili mgonjwa afe,” anasema kiongozi huyo.
Hata hivyo, Boni Yai anasema wanamshukuru Mungu kwa kukipigania chama hicho, hata wale waliochomoa dripu au kuzima umeme katika chumba cha mgonjwa ili afe, jambo hilo halikuwezekana.
“Ndani ya mwaka mmoja, mwenyekiti wa Chadema (Tundu Lissu) anakamatwa, baadhi ya viongozi wake wanaishi kwa misukosuko na mafichoni. Sasa hivi chombo (Chadema) kimeinuka kipo barabarani kinatembea, sasa waliondoka wanataka kupanda tena.
“Sasa wakipanda wakubaliane na hali yoyote atakayoipokea ya wanachama na umma, kutokana na maumivu ya wananchi aliowaacha wakati wakimuhitaji. Mgonjwa wakati anapigania uhai wake ulichomoa dripu au kuziba swichi ya umeme akiwa chumba cha mahututi (ICU),” anaeleza.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Boni Yai anasisitiza kuwa wanaorejea ndani ya Chadema wasitarajie mapokezi au kushangiliwa bali wanapaswa kukubaliana na hali yoyote watakayokutana nayo iwe kwa wanachama au umma.
Mapokezi mikutano ya hadhara
Katika mahojiano hayo, Boni Yai anagusia kuhusu mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya “Operesheni ya Katiba Mpya” na “Free Tundu Lissu” iliyofanyika kanda za Chadema za Victoria, Serengeti na Kaskazini kwa nyakati tofauti, akisema kumekuwa na mwitikio mkubwa.
Boni Yai anasema mwitikio huo unatokana na viongozi wakuu wa Chadema kujikita kueleza shida zinazowakabili Watanzania na madhara ya kutokuwapo kwa viongozi wa upinzani wa uhakika katika Bunge.
“Katika operesheni ile tujikita katika mambo mawili; mosi, tunapigania Katiba mpya kwa kueleza wananchi kuwa matatizo yote ya nchi hii chanzo ni Katiba, umasikini wa watu ubadhirifu wa fedha za umma na huduma mbovu za kijamii chanzo ni Katiba,” anasema.
Anaeleza kuwa katika mikutano hiyo, viongozi wakuu wa Chadema wanajikita kuwajengea uwezo wananchi kuona umuhimu wa kupatikana kwa Katiba mpya ili kuondoka na changamoto zinazowakabili ikiwamo ubovu wa miundombinu licha kuwapo kwa rasilimali nyingi ndani ya nchi.
“Tunajaribu kuwaambia licha ya Mungu kutubariki rasilimali mbalimbali ikiwamo dhahabu, almasi mkoani Shinyanga, je, vinafanana na umasikini uliopo kwa miaka 60. Shida za kijamii tunazokumba nazo zinafanana na utajiri tuliokuwa nao?” anahoji.
Boni Yai anasema kama Taifa halipaswi kufikia hatua hiyo, hakuna chanzo kingine isipokuwa upatikanaji wa Katiba mpya itakayowaondoa Watanzania kutoka walipo na kusonga mbele.
Mbali na hilo, Boni Yai anasema wanajikita kuwaeleza Watanzania kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma kwa kujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Itaendelea kesho…