Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jaivah: Kuna Marioo kisha Chino Kidd wote wanangu

Akiwa mwenye sauti ya kipekee yenye ujazo wa kutosha (bezi) ambayo kama angeimba kwaya basi angepangwa kwa waimbaji wa sauti ya nne au tano, Sebastian Charles maarufu Jaivah, anaibuka kidedea kwenye Bongo Fleva na kuteka hisia za mashabiki.

Unaweza kusema vya kurithi vinazidi, Jaivah katika mbili tatu na Mwananchi anafichua kwamba, katika familia yao yeye si wa kwanza kufanya muziki kwani hata mdogo wake Abbah Process ambaye ni produza amekuwa akifanya vizuri anga hizo. Pia kuna waimbaji wengine wa kutosha tu ndani ya familia.

2015 ndiyo mwaka ambao msanii huyu alianza kazi ya muziki baada ya kuachia ngoma yake ya kwanza ya ‘Jaiva’ na ndiyo ikabeba jina lake la kisanii.

 “Nilitoa ngoma ya kwanza iliyoitwa ‘Jaiva’, jina la Kizulu lenye maana ya ‘dansi’, mtangazaji wa redio Adam Mchomvu baada ya kuchukua ngoma yangu kwenda kuipiga redioni, akaniuliza jina gani natumia, sasa kipindi hicho nilikuwa nina majina mengi nilijiita Seba the producer mara S4C, akaniuliza maana ya Jaiva nikamwambia, akaamua kuanzia siku hiyo nitaitwa Jaivah, basi hapo  jina ndiyo likazaliwa”.

Licha ya sauti yake nzito inayobamba mashabiki wengi hasa wa kike, Jaivah anasema hajapoteza mashabiki wa kiume kwani vitu anavyoimba ni kwa ajili ya masela kitaani, anaamini ujumbe kupitia ngoma zake unawagusa zaidi washikaji ingawa warembo wanavutiwa zaidi na sauti.

Anasema amejipanga vizuri kwani ana ngoma nyingi ambazo bado hajazitoa hivyo anategemea akizitoa zitakwenda kuhit huku akiwa na matarajio makubwa miaka mitano ijayo.

“Ndani ya miaka mitano natamani kumuona Jaivah akisimama ni sawa na kuona bendera ya Tanzania. Unajua ukifiki level hiyo basi unakuwa tayari umefanya vizuri,” anasema Jaivah anayetamba na ngoma yake mpya ya Buruda akimshirikisha Marioo.

Kuhusu tuzo za muziki, akili ya Jaivah iko zaidi anga za kimataifa akiweka michakato ya kufanya vizuri ili kushindana na kunyakua tuzo kubwa duniani.

“Tuzo ni kati ya vitu ambavyo vinakupa sura ya kazi na muelekeo wako wa sasa na baadaye kwa sababu ili uipate ni lazima kuwe na ushindani na watu wenye uwezo mkubwa. Inapotokea umeshinda kuna kazi fulani imefanyika, naendelea kuomba Mungu na mashabiki na ‘timu’ yangu tupambane siku moja tuwe kwenye anga hizo na kutangaza Tanzania”.

Mchongo wa wasanii wachache wa Tanzania kupiga show na kupokea tuzo za mamtoni, Jaivah anasema hayo yanatokana na wasanii wengi wa Bongo kukosa wawakilishi sahihi kwenye majukwaa ya kimataifa.

“Kuna nafasi nyingi za kutupeleka mbali zaidi kimuziki. Wenzetu Nigeria wamejijenga sana kwenye eneo hilo na ndio sababu wanasikika, wanafanya vizuri na muziki wao kuteka masikio ya mashabiki kwenye mataifa mbalimbali. Kuna kundi kubwa sana la Watanzania linaishi nje ya mipaka ya nyumbani, hawa tunahitaji kushirikiana nao kwa karibu kutengeneza majukwaa ya kazi. Tunahitaji kuwa na mabalozi wa muziki wa Tanzania kimataifa,” anasema Jaivah na kuongeza:

“Tunafanya sana promo lakini tunahitaji watu watakaosaidia kuvuka mipaka na kuwa mabalozi wazuri, Bongo Fleva ni muziki wenye ujumbe na ladha tamu, tunahitaji kusogea mbele.”

Kama ilivyo kawaida miyeyusho ya baadhi ya mashabiki kushindanisha wasanii, ndivyo ilivyojitokeza  kwa msanii huyu, wapo wanaodai kuwa kwa moto wake kama Chino Kidd asipokaza basi jamaa atasepa na nyota yake, kwa sababu aina ya muziki wanaofanya inaendana sana.

Kutokana na maneno hayo ya mitandaoni, Jaivah anasema kila mtu ana nafasi ya kutoa maoni yake hakuna anayezuiwa, lakini kibaya ni tabia ya kumkandamiza mmoja ili kumsifia mwingine.

“Chino ni mdogo wangu uzuri ni ‘bondi’ yetu ni kubwa kiasi kwamba kugombana kirahisi  ni ngumu. Kwa sababu ingekuwa mtu mwingine, inavyosemwa fulani anachukua upepo wake huenda maneno hayo yangemjia vibaya.

 Sijachukua upepo wa mtu, kila kitu kina nafasi kikubwa ni kama kwamba wakati wa Mungu ukifika kila mtu atapata keki yake, yani hii keki ni kubwa sana” .

Anasema uhusiano wake na Chino sio wa kimjinimjini yaani haujaanza leo, anamjua Chino tangu anafanya kazi na Rich Mavoko.

“Chino Kidd nimeanza kufahamiana naye tangu mwaka 2007 kipindi ni ‘dansa’ wa Rich Mavoko, ni mdogo wangu wa muda mrefu hatujakutana tu ukubwani au kwenye ‘ustaa’ ni watu wa muda mrefu na ndiyo sababu hadi leo tupo pamoja ‘bondi’ yetu ni kubwa mno”.

Hata hivyo, mkali huyu anafichua kuwa ukaribu wake na Marioo nao umeweka bondi kwenye damu na mara ya kwanza walifahamiana tangu mwaka  2014.

“Abbah kama producer alikutanishwa na Marioo, kisha akaja kuniambia, kuna kijana anaonekana  noma sana, nikamwambia kama  kuna uwezekano wa ‘kumsapoti’ fanya hivyo. Nakumbuka  Marioo alikuwa  na ngoma yake moja inaitwa ‘Mboni yangu’ ilikuwa kali  hadi leo bado namuomba airudie, hapo tukawa naye na mpaka sasa amekuwa  Marioo huyu mnayemfahamu”.


Jaivah ni nani?

Sebastian Charles (Jaivah) ni mwanamuziki, mtunzi wa nyimbo, na mtayarishaji wa muziki, alizaliwa na kukulia jijini Dar es Salaam. Ni mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto wa tatu. Mtoto wa pili kwenye familia yao ni Abbah Process mtayarishaji wa muziki, kisha anafuata mdogo wao wa kike ambaye ni mhandisi.

Mwaka 2006 na  2007, ndiyo aligundua kipaji chake cha muziki baada ya ndugu yao mmoja kuwatambulisha yeye na Abbah kwa mtayarishaji wa muziki aitwaye Mtani.

Rasmi alianza muziki mwaka 2015, amewahi kufanya kazi na wasanii mbalimbali wakiwemo  Giggy Money, Country Wizzy na Darassa.

2021, alitoa EP yake ya kwanza inayoitwa ‘Jaivah Vibes’ ikiwa na ngoma saba kati ya hizo zikiwemo ‘Hata iwaje’, ‘Tungi’, ‘Locked’ na nyinginezo.

Wengi wameanza kumzingatia mwaka 2023 baada ya kuachia kibao chake cha ‘Supu’ akiwa amewashirikisha Marioo na Chinno Kidd.

Hakuishia hapo miezi mitano iliyopita alidondosha jiwe lingine la ‘Pita kule’ akiwa na Marioo.

Jaivah ni mtaalamu wa elimu ya biashara aliyoipata kwenye Chuo cha Biashara Dar es Salaam (CBE)