Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ibraah atii wito Basata, Harmonize hajafika

Muktasari:

  • Ibraah amezungumza na waandishi wa habari na kusema wamezungumzia migogoro iliyopo kati yake na Harmonize, hata hivyo anashukuru mambo yanaenda vizuri.

Dar es Salaam. Msanii Ibrahim Abdallah 'Ibraah' ameondoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) baada ya kumaliza mazungumzo yaliyofanya yeye na bosi wake Harmonize waitwe katika ofisi hizo.

Ibraah amezungumza na waandishi wa habari na kusema wamezungumzia migogoro iliyopo kati yake na Harmonize, hata hivyo anashukuru mambo yanaenda vizuri.

"Nashukuru Mungu mambo yanaenda vizuri na sababu ya kuitwa ni kuzungumzia migogoro inayoendelea. Kwa hiyo tumefanya mazungumzo na BASATA tumewaachia uongozi washughulikie wao watatoa majibu," amesema Ibraah.

Naye Mwanasheria wa Ibraah amesema, BASATA watakapotoa majibu juu ya kinachoendelea Ibraah ataendelea kufanya kazi zake kama kawaida.

"Kuhusu Ibraah kuendelea kufanya kazi zake kama kawaida, tunasubiri majibu ya BASATA,baada ya hapo Ibraah ataendelea na kazi zake kama kawaida," amesema mwanasheria wake Ibraah bila ya kutaja jina lake.

Hata hivyo Harmonize bado hajafika kwenye ofisi hizo, ambazo walitakiwa kufika tangu saa 7 mchana.

Ikumbukwe mzozo baina ya wawili hao ulianza Mei 3, 2025 baada ya Ibraah kuweka wazi kwenye akaunti yake ya Instagram anaomba michango kutoka kwa Watanzania ili kujinasua kwenye Lebo ya Konde Gang, inayomilikiwa na Harmonize.

Hata hivyo baada ya mnyukano huo mkali kwenye mitandao, Uongozi wa Kampuni ya Harmonize Ent.Ltd kupitia Lebo ya Konde Gang Music Worldwide ulitoa taarifa rasmi ya kumsimamisha Ibraah kutoa na kushiriki katika shughuli zozote za muziki hadi suala lake la kujitoa kwenye lebo hiyo litakapopatiwa ufumbuzi.

“Uongozi wa kampuni ya Harmonize Entertainment Ltd kupitia lebo yake ya Konde Gang Music Worldwide unapenda kutoa taarifa kwa umma kama ifuatavyo. Mnamo tarehe 03/05/2025, tulipokea barua ya madai (Demand Notice) kutoka kwa Wakili wa msanii wetu, Ibrahim Abdallah Nampunga IBRAAH.

HATMA Pict

“Barua hiyo iliainisha madai kadhaa ambayo uongozi umeanza kuyafanyia kazi mara tu baada ya kuipokea, kwa mujibu wa taratibu za kisheria na kimkataba. Licha ya juhudi zetu kujaribu kumuelekeza msanii taratibu za kufuata kulingana na mkataba wake.

“Hivi karibuni, tumebaini kuwepo kwa machapisho, matamshi, na mawasiliano kutoka kwa Ibraah katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii, ikiwemo Instagram na Facebook,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliendelea kwa kueleza machapisho hayo yanaonyesha malalamiko na lugha isiyofaa kwa afya ya lebo pamoja na kumhusisha mkurungezi muwekezaji wa lebo ambaye bado anaendelea kufanya kazi chini ya lebo hiyo.

“Tungependa kufafanua kuwa machapisho na matamshi hayo siyo tu yanachafua taswira ya lebo na wasanii wake, bali pia yanakiuka utamaduni wetu kama Watanzania na kukiuka masharti ya mkataba aliosaini na lebo hii. Aidha, yanaenda kinyume na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kampuni yetu inahifadhi haki zake zote za kisheria katika suala hili. Wakati huu ambapo mchakato wa kushughulikia masuala haya unaendelea, umma unapaswa kufahamu kwamba Ibrah bado ni msanii halali wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide na ina haki ya kuendelea au kusitisha mkataba wake kwa kufuata na kuzingatia taratibu rasmi zilizowekwa katika mkataba aliosaini,” ilieleza taarifa hiyo na kuongezea kuwa.

“Konde Gang inampiga marufuku Ibraah dhidi ya kuchapisha, kutamka, au kufanya mawasiliano yoyote kuhusu suala hili kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii (kama vile Instagram, WhatsApp, Facebook, n.k.). Hii ni pamoja na mawasiliano ya aina yoyote ambayo yanaweza kuharibu taswira ya lebo au kumdhalilisha mkurugenzi muwekezaji wa lebo ambaye ni msanii.”

Aidha taarifa hiyo ilisisitiza kuwa inatoa onyo kali iwapo masharti hayo yatakiukwa, lebo haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yake katika Mahakama za Tanzania.

Mnyukano huo uliokuwa ukipokea maoni mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii ulifika Basata na kupelekea Mei 12,2025 wawili hao kuitwa.

Hata hivyo katika wito huo wa mara ya kwanza alifika Ibraah pekee bila ya Harmonize kuonekana ofisini hapo. Baada ya mazungumzo na msanii huyo Mkuu wa Kitengo cha Sheria Basata, Christopher Kamugisha alisema wamesikiliza malalamiko ya pande zote mbili kuhusu wito wa wasanii Harmonize na Ibraah, maamuzi waliyokubaliana ni kufika wote kwenye ofisi za Basata leo Jumatano kwa ajili ya kusikilizwa.

Licha ya mazungumzo hayo kufanyika tena leo Mei 14,2025 bado Harmonize hakuweza kufika kwa mara nyingine .