DJ Mushizo aokolewa ajali ya moto Tabata, alazwa Amana

Muktasari:
- Mashizo alikumbwa na ajali hiyo jana saa 12 jioni, Juni 12,2025 wakati akiwa nyumbani kwake Tabata Jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Msanii maarufu wa nyimbo za singeli na DJ, Mussa Ramadhan Omary maarufu DJ Mushizo, ameokolewa baada ya kupata ajali ya moto iliyotokea katika nyumba anayoishi eneo la Tabata, jijini Dar es Salaam, mnamo saa 12 jioni ya Juni 12, 2025.
Kwa mujibu wa Meneja Msaidizi wa msanii huyo, Ally Masupu, chanzo cha ajali hiyo ni shoti ya umeme iliyotokea ndani ya nyumba anayoishi Mushizo, wakati akiwa amelala.
“Wakati moto unazuka Mushizo alikuwa usingizini. Alishtuka akiwa tayari moto umeshashika kasi, hakuweza kujiokoa mwenyewe,” amesema Masupu alipozungumza na Mwananchi.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio, wananchi wa jirani walilazimika kung’oa bati juu ya paa ili kufanikisha juhudi za kumtoa msanii huyo ndani ya nyumba hiyo iliyokuwa ikiteketea kwa moto.

Masupu ameeleza kuwa msanii huyo alipatiwa huduma ya kwanza katika zahanati ya karibu kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Amana ambako anaendelea na matibabu.
“Japokuwa amejeruhiwa sana na moto, lakini kwa sasa anaendelea vizuri. Mwenyezi Mungu anabariki,” ameongeza.
Taarifa za ajali hiyo zilianza kusambaa jana Alhamis Juni 13, 2025 kupitia mitandao ya kijamii ya DJ Mushizo, ambapo aliandika;
“Nimepata ajali ya moto jioni ya leo (jana) baada ya ninapoishi kushika moto na mimi nilikuwa ndani ya nyumba. Namshukuru Mungu nipo hospitali sasa naendelea na matibabu, maombi yenu ndugu zangu sana.”
Wakazi wa eneo la Tabata wameeleza kuguswa na tukio hilo na kutoa wito kwa mamlaka husika kuimarisha huduma za zimamoto na kuhakikisha usalama wa mifumo ya umeme katika makazi ya watu.