Basata yamlilia Hashim Lundenga, yataja mchango wake kwenye sanaa

Muktasari:
- Dk Mapana amezungumza hayo nyumbani kwa marehemu Bunju B, Dar es Salaam, na kwamba wakati wa Lundega wasichana zaidi ya 400 waliweza kushiriki mashindano hayo.
Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dk Kedmond Mapana amesema marehemu Hashim Lundenga, kupitia shindano la urembo la Miss Tanzania alitengeneza jukwaa la mafanikio kwa wanawake wengi nchini ambapo baadhi yao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali.
Dk Mapana amezungumza hayo nyumbani kwa marehemu Bunju B, Dar es Salaam, na kwamba wakati wa Lundega wasichana zaidi ya 400 waliweza kushiriki mashindano hayo.
“Kwa hiyo unaangalia namna gani jukwaa hili lilikuwa kubwa, lakini wote ni mashahidi kwamba warembo wote waliopitia katika jukwaa hili la Miss Tanzania wakati ule wa Hashim Lundenga wamekuwa ni watu waliopewa nafasi kubwa sana na Serikali.
"Tumeona kuna wakuu wa wilaya wengi wameteuliwa, tumeona hata mabalozi wameteuliwa, tumeona wamepata nafasi nyingine na wengine wameingia kwenye Sanaa, kwa hiyo sisi Basata tumepoteza mtu mahumu sana,” amesema Dk Mapana.

Lundenga alifariki dunia Aprili 19,2025 katika Hospitali ya Kitengule iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya homa ya mapafu na anatarajiwa kuzikwa leo Aprili 22, 2025 Kidatu, Morogoro
Atakumbukwa kwa mchango wake kama muasisi na mratibu wa mashindano ya Miss Tanzania tangu mwaka 1994 hadi 2018. Pia amewahi kuhudumu katika kamati ya Klabu ya Yanga.