Prime
ANKO KITIME: Pepe Kale aliwahi kupiga muziki Njombe na Buguruni

Leo naendelea kusimulia mikasa iliyowahi kuwapata wanamuziki kutoka Kongo walioalikwa nchini na kufanya maonyesho ya muziki hasa katika kipindi kati ya mwaka 1990 na 1999. Wiki iliyopita nilianza kwa kuhadithia mkasa wa Diblo Dibala katikati ghafla jina likabadilika na kuwa Dally Kimoko hii ilifanyika kimakosa, usahihi ni kuwa mkasa ule ulimhusu Diblo Dibala na kundi lake mwanzo hadi mwisho.
Mwanamuziki mwingine aliyewahi kupata mkasa baada ya kuingia nchini alikuwa Sam Mangwana. Huyu alialikwa nchini na kufanya maonyesho kama ilivyokuwa kwenye mkataba wake, lakini baada ya kumaliza kazi yake kukawa na matatizo ya kumkamilishia malipo, hivyo akakwama kwa muda mrefu hapa nchini, mwenyeji wake alikuwa marehemu Anania Sangula ambaye kwa shukrani na urafiki wao alitajwa mara kwa mara katika wimbo ulioitwa Toujours aliouimba Sam Mangwana mwenyewe na Franco Luambo Luanzo wakisindikizwa na kundi zima la TP OK Jazz. Kukwama kwa Sam Mangwana kulikuwa na faida inayodumu mpaka leo kwani katika kuitembelea Vijana Jazz Band alitoa mchango katika upangaji wa vyombo wa wimbo maarufu wa Mary Maria.
Kundi zima la Soukous Stars nalo liliwahi kujikuta likikwama Tanzania baada ya kumaliza maonyesho yake. Hiyo ilikuwa enzi Dr Sarungi akiwa Waziri wa Utamaduni na Michezo. Ililazimika Waziri kuitisha kikao wizarani kujadili janga la mapromota kuwaleta wanamuziki kisha kukwama kukamilisha mikataba nao, pamoja na kikao kile kukwama kutokana na baadhi ya wajumbe kudai hawawezi kufanya kikao bila posho, lakini muda mfupi baada ya hapo taratibu mpya zilikuja kutolewa ambapo promota alitakiwa kuonyesha uwezo wake wa kukamilisha mkataba.
Ilikuwa wakati huuhuu ambapo mfanyabiashara mmoja wa magari alipodhamini mashindano ya wapiga gitaa la solo, ulikuwa mpambano mkali sana, uliohusisha wapiga solo wa bendi mbalimbali za wakati ule, lakini mashindano hayo hayakufikia tamati kutokana na wanamuziki washiriki kugoma kuendelea na shughuli hiyo kwa kutolipwa stahiki zao. Shindano lilivunjika baada ya onyesho lililofanyika katika Ukumbi wa Vijana Social Hall Kinondoni, onyesho hilo ambalo lilihudhuria na Waziri Sarungi na baadhi ya wanamuziki wa Soukous Stars, mmoja wao akateuliwa kuwa mwamuzi wa pambano siku ile.
Pepe Kalle, jitu la miraba minne naye alipata sekeseke tosha katika moja ya mialiko aliyowahi kupata hapa nchini. Wadau wa muziki kadhaa waliweza kumshawishi mfanya biashara mmoja wa madawa ya kilimo kumukaribisha Pepe Kalle na kundi lake na wakamuaminisha kuwa atapata faida kubwa kutokana na ziara ya nguli huyo. Rafiki yangu ambaye alikuwa pia rafiki wa mfanyabiashara yule alinitaarifu kuhusu biashara ile, lakini nilipoiona ratiba ambayo bendi ya Pepe Kalle ilisemekana angeifuata, mara moja nikagundua kuwa haitekelezeki. Ilitengenezwa kumrubuni mfanya biashara yule atoe fedha tu. Katika ratiba hiyo Pepe Kalle alikuwa onyesho moja Dar es Salaam, kisha aanze ziara ambayo ingeanzia kwa onyesho la mchana katika Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro, usiku angefanya onyesho katika ukumbi mmoja wapo hapo Morogoro, na baada ya onyesho bendi ingesafiri usiku na kesho yake mchana kufanya onyesho Uwanja wa Samora Iringa na usiku kufanya onyesho katika Ukumbi wa Iringa na kuendelea na safari kuelekea Njombe. Nikamwambia rafiki yangu ni vizuri tumtaarifu huyu jamaa hali halisi. Tulijaribu kila njia kuwasiliana naye akakataa kutuona, nguvu za upande wa pili nazo zilikuwa kubwa, baada ya kumsubiri nyumbani kwake mpaka saa nne ya usiku asionekane tukaamua kuliacha jambo hilo. Ratiba ilibadilika kidogo onyesho la kwanza likapangwa kufanyika kwenye ukumbi mmoja Kinondoni, lakini dakika za mwisho kabla dansi halijaanza mwenye ukumbi akagundua kuna tatizo akabadili taratibu na kutangaza kuwa anataka alipwe chake kwanza ndipo onyesho liendelee. Hii ilikuwa kinyume cha taratibu wakati huo, ambapo kumbi zilikuwa zikilipwa asilimia ya mapato ya mlangoni.
Huo ukawa mwanzo wa matatizo, yule mfanya biashara akalazimika kutafuta fedha haraka alipie ukumbi ili onyesho lisiharibike. Onyesho lilipoanza ghafla ikasemekana kuna tiketi bandia zinauzwa, wauza tiketi wakabadilishwa, kimsingi lilikuwa onyesho la hasara kifedha. Baada ya hapo Pepe Kalle akapelekwa Njombe alikopangiwa afanye onyesho Ukumbi wa Kibena Club, ukumbi ulio nje kidogo ya mji wa Njombe, bahati mbaya siku ile mvua kubwa ikanyesha na kuharibu mambo. Wakati huohuo Idara ya Uhamiaji Makao Makuu ikatoa amri kuwa kundi zima la Pepe Kalle lirudi Dar es Salaam mara moja kwani kulikuwa na taratibu zimekiukwa.
Baada ya kurudi Dar es Salaam, Pepe Kalle akapangiwa onyesho ukumbi wa Bahama Mama uliokuwa Kimara Baruti. Meneja wa Ukumbi wakati ule naye aliona mambo hayaendi inavyotakiwa naye akadai alipwe kabisa fedha zake badala ya kungojea kugawiwa stahiki zake kutoka pato la mlangoni.
Baada ya hapo hata Pepe Kalle akaanza kumuonea huruma yule mfanyabiashara kwani maonyesho yote yalikuwa ni hasara tupu, akakubali kufanya onyesho moja bila kulipwa. Na ikatangazwa Pepe Kalle angefanya onyesho katika ukumbi wa Y2K wa Buguruni hata huko biashara ilikuwa mbovu kwani hakukuwa na matangazo stahiki kwa mwamba kama Pepe Kalle. Kwa kifupi ilikuwa hasara kubwa kwa mfanyabiashara yule.Ilipita muda mrefu tukakutana na mfanyabiashara yule kwenye msiba, alipotambulishwa kuwa, ‘Huyu ndie John Kitime aliyekuwa akikutafuta kabla ya maonyesho ya Pepe Kalle’, aliniangalia kisha akasema, ‘ Loh, mbona niliambia wewe bonge la mtu mwenye umbo la kijambazi, ndio maana sikutaka hata kukuona’