Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ANKO KITIME: Sio zilipendwa bali zinaendelea kupendwa

Muktasari:

  • Kwa ujumla watu huita vipindi hivi vya muziki, vipindi vya  ‘Zilipendwa’. Neno hili lilizaliwa Radio Tanzania Dar es Salaam ilipoanzisha kipindi kilichokuwa kikirushwa Jumamosi usiku na kurudiwa Jumapili asubuhi, kipindi ambacho kilikuwa kikipiga nyimbo za zamani.

Dar es Salaam. Moja ya vipindi maarufu karibu kila redio nchini kwa sasa ina kipindi cha muziki wa zamani, vipindi hivyo vina majina ya kufurahisha kama vile, Zilipendwa, Zama Zile, Za Old is Gold, Ya Kale Ghahabu, Old School na kadhalika.  

Kwa ujumla watu huita vipindi hivi vya muziki, vipindi vya  ‘Zilipendwa’. Neno hili lilizaliwa Radio Tanzania Dar es Salaam ilipoanzisha kipindi kilichokuwa kikirushwa Jumamosi usiku na kurudiwa Jumapili asubuhi, kipindi ambacho kilikuwa kikipiga nyimbo za zamani. 

Katika zama hizi asilimia kubwa ya vituo vya redio vinapoanza kurusha matangazo kwa mara ya kwanza, hasa katika kipindi kile cha majaribio, muziki wa zamani hupigwa mfululizo kutaarifu kuwa kuna redio mpya. 

Kwa kupiga muziki huu watu huzoea masafa mapya kabla redio haijaanza kazi rasmi. Jambo la ajabu mara nyingi radio hizo huachana na muziki huo ambao umesaidia kutangaza masafa mapya mara baada ya kuanza rasmi matangazo yake. 

Katika radio nyingi kipindi cha nyimbo za zamani huwa mara moja au mara mbili kwa wiki. Ni wazi kuwa vipindi hivi vya muziki wa zamani vina wasikilizajji wengi sana kwani watangazaji au watayarishaji wa vipindi wa nyimbo hizi za zamani wengi wamekuwa na  umaarufu mkubwa kwa kazi hiyo. Majina kama Masoud Masoud, Zomboko, Stazo, Churchil, Adam Zuberi, ni majina maarufu katika masikio ya wapenzi wa muziki wa zamani. 

Vipindi hivi vina ladha tofauti kadri ya mpangilio wa mtayarishaji wake. Kuna vingine hupiga muziki ukifuatana na maelezo matamu ya matukio mbalimbali ya enzi hizo, watangazaji wegine ni mahiri kwa kumbukumbu za majina ya wanamuziki wahusika katika nyimbo mbalimbali wanazozipiga, na wengine ni mabingwa wa kupangilia nyimbo za zamani na hivyo bila maneno mengi huhakikisha wasikilizaji wao hawabanduki kwa kuwateremeshia muziki mtamu mmoja baada mwingine.

Lakini pia kuna watangazaji vijana ambao kwao muziki wa zamani ni ule uliopigwa miaka ya 90, hivyo basi nao vipindi vyao vina ladha aina nyingine kabisa ya muziki wa zamani. Tafsiri ya muziki wa zamani nayo ni pana, unaweza kujiuliza  je, muziki wa zamani unaanzia wapi? Mara nyingi mtayarishaji ndiye anakuwa na uamuzi katika kipindi chake juu ya tafsiri ya zamani. 

Kuna vipindi vinapiga nyimbo hata za miaka ya 50, redio nyingine huanzia miaka ya 60 na kama nilivyosema wengine muziki wa zamani ni ule wa miaka ya 90, kila mmoja ikijinadi kuwa inapiga muziki wa zamani na hakika hakuna aliyekosea kati ya hao. 

Ni nini kinafanya muziki huo uendelee kutamba? Kama umeangalia kamwe sijauita muziki huu ‘zilipendwa’, kwani ni muziki uliopendwa enzi hizo, unapendwa sasa na utaendelea kupendwa. 

Kwa bahati nzuri  mimi ni mwanamuziki wa zamani, na pia ninaendesha kipindi cha muziki wa zamani, huwa nami najiuliza nini kinafanya nyimbo hizi zilizorekodiwa kwa gharama ndogo sana katika studio duni za  miaka ya 60 ziendelee kupendwa kwenye ulimwengu huu wa kidijitali wenye nyimbo zilizorekodiwa kwa ubora wa hali ya juu na gharama kubwa  na zikiwa zimeambatana na video zilizotengenezwa kwa mamilioni ya shilingi?

Hata kwangu mimi sina jibu, huwa nashangaa pale ninapoona vijana wadogo wakipenda sana nyimbo hizi. Kuna wale ambao huzifuatilia hufuatilia kwa makini vipindi hivi vya nyimbo za zamani, kuna wale ambao huzicheza kwa furaha zikipigwa dansini,  kwa vile nyimbo hizi nyingi hazikuweza kuwekwa katika video kuonyesha zilikuwa zinachezwaje, huwa inachekesha vijana wa kisasa wanapocheza kwa mitindo wanayoibuni, huwa tofauti kabisa na uchezaji wa asili wa nyimbo hizo.

Kwa mfano ukipiga wimbo wa twist, wazee wakiingia unakuta wanajitahidi kuchezesha visigino na magoti, bahati mbaya uzee unawanyima uwezo wa kuonyesha umahiri, sasa akiingia kijana hapo anaanza kukata kiuno kama feni, twist haikuwa inachezwa hivyo, hakika mtu angecheza staili hiyo enzi hizo angefukuzwa mtaa kwa kuonekana anavunja maadili.

Kati ya mambo ambayo nadhani yanafanya nyimbo za zamani ziendelee kupendwa ni maneno matamu yenye maana na mafupi, na kwa kuwa kulikuwa na chujio nyingi hakukuwa na nyimbo zenye lugha chafu, pia nyimbo za siku hizi unaweza kukuta ni ndefu mno, hata kurasa mbili za hadithi katika wimbo mmoja. 

Wimbo mfupi  unakuwa rahisi kuukariri. Kingine ni mpangilio wa vyombo, hili nadhani ndilo kubwa zaidi. Kati ya vitu vilivyokuwa vinasisitizwa katika tungo za zamani ni muafaka wa vyombo. Kila chombo kinachopigwa lazima kiwe na mahusiano na kingine, si mradi kimepigwa tu. 

Taaluma hii bahati mbaya haipo kwenye muziki unaotengenezwa studio, tatizo likiwa ‘producers’ wengi hawakupitia kwenye elimu ya ‘music arrangement’. Taaluma hii pia imekuwa nadra hata kwenye bendi zetu, hivyo unakuta bendi ina wimbo wenye melodia nzuri sana ya uimbaji na ikisha rekodiwa inaishia kupendwa kwa siku chache kutokana na vyombo vilivyopigwa kutokuvutia sikio la msikilizaji.