Wasanii wa kizazi kipya wanavyopita na ngoma za zamani

Muktasari:
- Upangiliwaji wa mistari hiyo ndiyo moja ya sababu ya ngoma hizo kufanya poa hadi sasa kwenye ulimwengu wa Amapiano na Singeli.
Dar es Salaam, Ukali wa nyimbo zilizotolewa miaka ya 2000, ulitokana na stori tamu zilizokuwa zikipangiliwa kwenye mashairi, huku ngoma nyingi mistari yake ikiwa imepangwa katika mtindo wa stori za masimulizi.
Upangiliwaji wa mistari hiyo ndiyo moja ya sababu ya ngoma hizo kufanya poa hadi sasa kwenye ulimwengu wa Amapiano na Singeli.
Ngoma kama Kafia Ghetto, Ghetto Langu, ‘King’asti, Binti Kiziwi, Zali la Mentali, Wrong Number, Baby Candy, Vaileti, Latifa, Kidato Kimoja na nyinginezo ni kati ya zilizofanya vizuri kwa miaka hiyo na hadi sasa zikipigwa watu wanaruka nazo.
Licha ya kuwa wasanii wa kizazi kipya wamekuwa wakipita na biti za Amapiani, Singeli, na Rnb kufanya vizuri kwenye biti hizo lakini bado wanaonekana kuamini na kuvutiwa na tungo za mistari iliyopangiliwa na wasanii wa zamani kwenye ngoma zao jambo linalopelekea wengi wao kuzirudia na kuzifanya mpya .
Baadhi ya ngoma zilizorudiwa
Yule - Ay na Marioo
Yule ni ngoma ya Ay yenye dakika 03 na seknde 32 ilikuwa moja ya nyimbo zilizofanya vizuri kwenye albamu yake iliyotitwa Hisia Zangu. Mistari ya ngoma hiyo imebeba ujumbe wenye kuonesha namna ambavyo Ay amedata kwa msichana ambaye hana mambo mengi, huku akimwaga sifa kibao.
Ngoma hiyo baada ya kuachiwa ilifanya poa, lakini kwa sasa mkali wa muziki nchini Marioo naye amepita kwenye biti, ikiwa kama kuifufua upya ngoma hiyo ambayo watu walitamba nayo zaidi ya miaka 17 iliyopita.
Yule mpya imeachiwa siku nane zilizopita na hadi sasa kwenye mtandao wa YouTube ina watazamaji zaidi ya laki mbili na themanini.
Shisha - Marioo na Mr Nice
Shisha ni ngoma ya mwanamuziki Marioo ambayo aliiachia miezi saba iliyopita na hadi sasa kwenye mtandao wa Youtube tayari imetembelewa na watu milioni 2.3.
Ndani ya ngoma hiyo inasikika mistari ya mwanamuziki wa zamani Mr Nice, aliyoimba kwenye ngoma yake ya King’asti iliyotoka zaidi ya miaka kumi iliyopita. Uimbwaji wa wimbo huo kwa mara nyingine na mwanamuziki Marioo, ulienda kuwakumbusha mashabiki enzi za Mr Nice zilivyotikisa kupitia tungo zake.
Mapoz - Diamondplatnumz ft Mr Blue na Jay Melody
Mapoz ulikuwa wimbo wa mwanamuziki Mr Blue ambao alitoa zaidi ya miaka miaka kumi na tano iliyopita, lakini wimbo huu ulirudiswa na kuwa mpya na mwanamuziki Diamond kwa kuufanyia remix ambayo ndani yake alikuwepo Jay Melody na Mr Blue mwenyewe.

Wimbo huo mpya hadi sasa umefikisha watazamaji 15 Milioni ndani ya miezi minne tangu utoke.
Raha ya Tunda - Dully Sykes, Young Lunya na Yammi
Raha ya tunda ni wimbo wa Hot Galz, waliomshirikisha mwanamuziki Dullu Sykes , wimbo huo umerudiwa tena miezi saba iliyopita na wanamuziki Young Luya , Yammi akiwemo na mwenyewe Dully.

Urudiwaji wa ngoma hiyo ulirudisha usikivu upya kwenye masikio ya mashabiki na kuufanya uwe kama mpya.
Tangu itolewe remix ya Raha ya tunda hadi sasa imefikisha watazamaji laki tatu na elfu ishirini na saba kwenye mtandao wa Youtube.
Subal kheri - Nandy na Aslay
Miaka sita iliyopita wasanii Nandy na Aslay walifanya marudio ya wimbo wa mwanamuziki wa zamani Nasma Khamis, Subal kheri, wimbo ambao ulirudi upya masikioni mwa watu licha ya kuwa wimbo halisi ulitolewa miaka mingi iliyopita.
Hadi sasa wimbo huo umefikisha watazamaji 9.5 milioni kwenye mtandao wa Youtube.
Lody Music - Nilizama (Bi Shakira - Nimezama)
Naye mwanamuziki na mtunzi wa nyimbo nchini Lody Music miezi tisa iliyopita aliufanya upya wimbo wa mwanamuziki wa zamani Bi Shakira na kuufanya uonekekane mpya.
Wimbo huo hadi saa una watazamaji zaidi ya elfu kumi na tisa kwenye mtandao wa Youtube.
Si hivyo tu zipo nyimbo nyingine pia kama vile ‘Zilipendwa’ iliyofanywa na wasanii wa WCB kwa kipindi hicho, Siri ya nini ya Hussein Jumbe pia ilirudiwa na mwanamuziki Rayvanny na nyingine nyingi.
Mitazao ya wadau kuhusu wasanii kurudia nyimbo
Mdau wa muziki James Mbazi ameeleza kuwa kurudia Wimbo si jambo baya kwa dhana ya kuukubali ubora wa wimbo husika na pia kuchanganya vionjo tofauti kwa hadhira .
“Ni vyema upate ruhusa ya mtunzi/mmiliki wa haki kisheria, ikiwezekana kimaandishi,vinginevyo utakua umeiba kazi ya mtu,” alieleza
Hata hivyo alieleza kuwa wasanii wa sasa wanatakiwa kukubali kuwa muziki ni taaluma.
“Muziki ni taaluma tujishughulishe kuijua kweli ya muziki nayo kweli itatuweka huru kiutunzi na kimbinu, nasema hivyo kwakua hata wakongwe wa zilipendwa waliopo sasa hawana tungo mpya, kama ambavyo wamekua wakifanya zama zao, labda walivyofanya vinatosha, hili tuliache, kazi kwetu tunao anzisha zama mpya,”alieleza.
Abdull Ibbu, mdau wa muziki kutoka DSM amesema kufanya wasanii kutumia nyimbo za wakongwe ni ubunifu wa wasanii.
“Mimi naangalia katika pande mbili, pande ya kwanza ni sehemu ya ubunifu, kwa sababu kurudia nyimbo siyo jambo jipya, toka miaka hiyo wasanii huwa wanakawaida ya kurudia nyimbo, nchini Marekani ni kitu cha kawaida japo kwetu ndiyo inaonekana bado kama jambo baya,
“Kwa sababu kurudia kunasababisha pia kuongeza mashabiki wapya ambao hukuwa nao kabla, mashabiki wa enzi ya hiyo nyimbo na kuwafanya watu wakupe sikio upya,”amesema na kuongeza kuwa wasanii wanatakiwa kuboresha mashairi ili kazi zao pia zije kurudiwa kama wanavyofanya wao.
Hata hivyo akizungumza na gazeti hili mwanamuziki Lody Music ambaye amerudia wimbo wa Bi Shakira amesema kuwa kilichofanya arudie wimbo huo ni kumuenzi baba yake ambaye alikuwa mtunzi wa nyimbo zamani.
“Makuzi ya Kilwa Pwani, mzee mwenyewe alikuwa mwandishi wa taarabu alikuwa anaandikia wasanii wa zamani katika historia na mama aliongelea hivi vitu, na huu ulikuwa wimbo pendwa wa mzee kwa hiyo nikaona niifanya kama kumbukumbu kwa mzee lakini pia inafanya vizuri,”alisema.
Mbali na hayo amesema haoni kama kuna hasara yoyote kwa msanii kurudia wimbo badala yake anaona kuna faida zaidi
“Nadhani kuna faida zaidi pengine kuna kizazi kipya ambacho hakikuweza kupata muziki wa zamani, lakini walikuwa wanasikia stori kwa hiyo kuuwakilisha huo muziki watu wanajua kumbe ilikuwa hivi,”alisema.
Lody alikanusha tuhuma za mashairi ya muziki wa sasa kutokuwa na nguvu kwa kueleza kuwa kinachopelekea nyimbo za sasa kusahauli mapema ni uwepo wa wasanii wengi.
“Zamani muziki ulikuwa mgumu kwa sababu ya vifaa havikuwa vingi, lakini kwa sasa vifaa ni vingi wanamuziki wengi, msikilizaji anachagua nini cha kusikiliza kwa hiyo inakuwa ngumu muziki kukaa kwa muda mrefu, zamani msanii akiachia ngoma inaweza kukaa hata miaka miwili bila kuachia wimbo mpya lakini kwa sasa ni tofauti ndiyo maana wasanii wanaendelea kutafuta kiki ili waendelee kuwepo”,alisema
Malipo wakirudia nyimbo za zamani
“Kuna aina mbili kama unataka kuifanya yako kama Marioo alivyofanya ‘Shisha’ lazima kuwepo na makubaliano na ndiyo maana hata Mr Nice aliposti.
“Lakini ikiwa kama cover, inafanyika bila kutoa taarifa na ndiyo maana hata wasanii chipukizi wanafanya sana, lakini kwa kufanya cover pesa inakuwa inaenda kwa muhusika mwenye wimbo, kwa hiyo YouTube wanakagua wanapeleka mapato kwa muhusika, na usipoandika kuwa ni cover wanaifunga unahesabika kama mwizi,”alisema