Abigail Chams aandika historia hii kwenye Bongo Fleva

Muktasari:
- Mapema jana kupitia ukurasa wake wa instagram alishare taarifa hiyo huku akitoa shukrani kwa mashabiki wanaomsapoti pamoja na kuahidi kuwakilisha utamaduni wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa
Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Abigail Chams, ameweka historia kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kuwania tuzo ya kimataifa ya BET katika kipengele cha ‘Best International Act’, hatua ambayo hapo awali ilifikiwa na Diamond Platnumz pekee.
Mapema jana kupitia ukurasa wake wa instagram alishare taarifa hiyo huku akitoa shukrani kwa mashabiki wanaomsapoti pamoja na kuahidi kuwakilisha utamaduni wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.
Utakumbuka mwaka 2014 historia hiyo ilishikiliwa na mwanamuziki Diamond Platnumz akiiwakilisha Tanzania kwa mara ya kwanza katika kuwania kipengele hicho ambacho awali kilifahamika kama ‘Best International Act: Africa’.
Baada ya kugonga mwamba mwaka huo Simba alijaribu tena bahati yake mwaka 2016 na 2021 lakini hakufanikiwa kutwaa tuzo hiyo.

Hata hivyo, mbali na Simba msanii Rayvanny naye alitajwa kuwania tuzo hizo katika kipengele cha Viewer’s Choice na kufanikisha kushinda huku akiwa msanii pekee kutoka Bongo kushinda tuzo hizo za BET.
Uteuzi huu wa Abigail katika kipengele hicho unathibitisha mchango wake mkubwa katika kukuza muziki wa Bongo Fleva kimataifa. EP yake iliyopewa jina la ‘5’ iliweza kushika nafasi ya tatu kwenye orodha ya albamu zinazopigwa sana katika mtandao wa Audiomack Africa, hatua iliyoinua zaidi jina la Tanzania katika muziki wa Afrika.
Aidha, Abigail aliweka rekodi nyingine ya kuwa mmoja wa wasanii wachache wa kike waliowahi kupewa heshima ya kuwa ‘Spotify EQUAL Ambassador’ kwa mwezi Desemba 2023, nafasi ambayo hapo awali iliwahi kutolewa kwa Zuchu mwaka 2022.
Mpango wa Spotify EQUAL hulenga kuwawezesha wasanii wa kike kutoka Afrika kwa kuwapa msaada na rasilimali ili waweze kukua na kuwafikia mashabiki wengi zaidi duniani.
Wimbo wake maarufu ‘Mee Too’ umeendelea kufanya vizuri kwenye chati mbalimbali barani Afrika na hata nje ya bara hilo, jambo linaloonyesha mafanikio yake kimataifa.
Kutokana na mafanikio haya, kupitia ukurasa wa Instagram Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilitoa pongezi kwa msanii huyo.
“Uteuzi huu ni ushahidi wa kazi kubwa, nidhamu, na ubunifu wa hali ya juu unaofanywa na wasanii wetu, pamoja na mchango mkubwa wa mashabiki wanaoendelea kuunga mkono sanaa ya Kitanzania. Ni fahari kwa Taifa kuona utamaduni wetu ukiwakilishwa kwa heshima kubwa duniani,” walisema.
BASATA pia lilimtakia kila la heri katika safari yake ya kimataifa na kuahidi kuendelea kushirikiana naye kwa ukaribu.

Mbali na BASATA msanii huyo alipata pongezi nyingine kutoka kwa wasanii wenzake, watangazaji wa redio, mameneja wa sanaa, na wadau mbalimbali wa tasnia ya burudani nchini, wote wakimpongeza Abigail kwa hatua hii kubwa ambayo inaandika upya historia ya muziki wa Bongo Fleva.