50 Cent alinunua viti 200 kwenye show ya Ja Rule na kuviacha wazi

Muktasari:
- Pamoja na kuwa yapo matukio mengi kwenye muziki lakini vita ya 50 Cent na Ja Rule ni kati ya vitu ambavyo havitasahaulika kwenye ulimwengu wa muziki
Upinzani na ushindani umekuwa kitu cha kawaida kwa watu wanaofanya jambo la kufanana,kama ilivyo kwa wafanyabiashara katika kuvuta wateja, kwenye michezo hali hiyo ipo kwa Simba na Yanga, japo hili linaonekana hata katika upande wa muziki.
Ndiyo maana unaweza kukuta msanii f'lani ana upinzani na mwingine kwenye upande wa kazi, kwa sababu kila mmoja anataka mashabiki wamuone yeye ndiye bora. Jambo hilo si Tanzania tu walipo Diamond na Ali Kiba, bali duniani kote upinzani unatokea.
Pamoja na kuwa yapo matukio mengi kwenye muziki lakini vita ya 50 Cent na Ja Rule ni kati ya vitu ambavyo havitasahaulika kwenye ulimwengu wa muziki.
Wapinzani hawa wawili wa muziki wa #Hip Hop kutoka Marekani, kutokana na upinzani wao mwaka 2018, ulimfanya 50 Cent anunue tiketi 200 za viti vya mbele kwenye tamasha la Ja Rule na kuviacha wazi kwa lengo la kumkomoa staa huyo ili aonekane hajajaza watu kwenye tamasha lake.
Kutokana na tukio hilo ilipelekea viti vyote vya mbele kuachwa wazi huku mashabiki waliokuwa wamebahatika kupata tiketi wanaokadiriwa kuwa hawakufika hata 50, wakiwa wamekaa viti vya nyuma kabisa mbali na sehemu aliyokuwa akitumbuiza Ja Rule.
Ugomvi wa wakali hawa wawili unatajwa kuwa wa kitambo kwani ulianza mwishoni mwa miaka ya 90 na kila mmoja amekuwa akimvimbia mwenzake kwa namna yake hadi kufikia 50 Cent kufanya hivyo katika tamasha hilo ambalo Ja Rule alikuwa akifanya na Ashanti, ambapo kila kiti kilikuwa kikiuzwa kwa dola 15 ambayo ni zaidi ya shilingi 30,000.