Ugomvi wa Marioo unanunulika

Muktasari:
- Kwenye muvi wanamtaja mtu Keanu Reeves, steringi wa muvi za Matrix na John Wick. Tafiti za mitaani zinaonyesha hakuna mtu anayemchukia jamaa kwa sababu hana majivuno anaishi maisha kama sio milionea.
Dar es Salaam. Mitandaoni kunakuwa na mijadala ya watu maarufu wasiochukiwa. Katika soka anatajwa mtu kama N'golo Kante kwamba hata uwe na chuki vipi huwezi kumchukia, hana makuu, hana mbwembwe, anachokifanya ni kuingia uwanjani kucheza mpira, basi.
Kwenye muvi wanamtaja mtu Keanu Reeves, steringi wa muvi za Matrix na John Wick. Tafiti za mitaani zinaonyesha hakuna mtu anayemchukia jamaa kwa sababu hana majivuno anaishi maisha kama sio milionea.

Anatoa misaada kwa wasio nacho, hayupo kwenye mikumbo ya wasanii wa Hollywood na huwezi kumkuta kwenye skendo chafu za watu wa tasnia hiyo.
Kibongobongo katika muziki wa Bongofleva, Marioo anaweza kuingia kwenye hiyo listi. Ni kama vile hakuna shabiki anayemchukia Marioo.
Haonyeshi kugombana na wasanii wenzake na hata inapotokea mikwaruzano na wasanii wenzake, na ikafika kwenye mitandao ya kijamii, basi mashabiki huingilia kati na kumtetea utadhani walikuwepo wakati ugomvi unatokea yaani kwa lugha nyepesi unaweza kusema ugomvi wa Marioo unanunulika.
Kumbuka wakati anazinguana na Chinno watu walimtetea sana kwenye uwanja wa maoni. Pia, muziki wa Marioo unapendwa. Ni msanii anayeshikilia namba na rekodi mbalimbali bila kiki wala skendo za aina yoyote.
Lakini licha ya yote hayo, mashabiki wa Marioo wamekuwa wakimuongelea kuwa ana upungufu sehemu moja. Hana mipango ya kukuza muziki wake kimataifa.

Mashabiki wamekuwa wakisema hivyo kwa sababu ndani ya nchi Marioo ameshika vibaya. Watanzania kibao wanajua na kuziimba ngoma zake sio vijijini sio mjini, si wazee si watoto. Lakini wanadhani nje ya Tanzania ni wa kawaida sana. Hakuna anayemjua.
Na Marioo mwenyewe haonekani kufanya jitihada za kwenda kimataifa. Na jitihada zinazoongelewa hapa ni kufanya kolabo na wasanii ambao sio Watanzania.
Nadhani Marioo amesikia kuhusu hilo na ndiyo maana ameamua kuanza kukata kiu ya mashabiki polepole. Na ameonyesha hilo kupitia albamu yake inayoitwa The Godson.
Kwenye albamu hiyo yenye ngoma 17 Marioo amefanya ngoma nne na wasanii wa nje ya Tanzania. Ngoma namba nne amefanya na Bien wa Sauti Sol kutoka Kenya inaitwa Nairobi. Ngoma namba sita amefanya na Kenny Soul wa Rwanda inaitwa Happiness.
Ngoma namba tisa ya My Eyes amefanya na Patoranking wa Nigeria. Ngoma namba 11 amefanya na ELEMENT EleeeH wa Rwanda inaitwa Njozi. Kisha kwenye ngoma namba 12 amemshirikisha msanii wa Ghana anayeitwa King Promise inaitwa No One. Na akamaliza na Joshua Baraka wa Uganda kwenye ngoma ya High.
Hata kama Tanzania tumewahi kupata kolabo za wasanii wa nje wenye majina makubwa zaidi ya hao, lakini Marioo anaonyesha kiu ya kutaka kukata kiu ya mashabiki upande wa kufanya muziki kimataifa. Ameanza hapa naamini albamu yake ijayo itakuwa imepiga hatua kubwa upande wa kolabo za kimataifa zaidi.