Cassie aendelea kuanika mapya akitoa ushahidi kesi ya Diddy

Muktasari:
- Mwanamuziki huyo ameeleza kuwa kumbukumbu mbaya zilimwelemea sana mpaka akajaribu kuondoka nyumbani akiwa na mpango wa kujitupa barabarani ili ajiue, lakini mume wake alimzuia na ndipo akaanza kwenda kupata ushauri wa kisaikolojia.
Marekani. Akihitimisha siku ya pili ya kutoa ushahidi katika kesi ya inayomkabili Sean "Diddy" Combs. Mwanamuziki Cassie Ventura alilia kwa uchungu huku akifichua kwamba aliwahi kufikiria kujitoa uhai miaka miwili iliyopita.
Mwanamuziki huyo ameeleza kuwa kumbukumbu mbaya zilimwelemea sana mpaka akajaribu kuondoka nyumbani akiwa na mpango wa kujitupa barabarani ili ajiue, lakini mume wake alimzuia na ndipo akaanza kwenda kupata ushauri wa kisaikolojia.

Katika maelezo yake mapya katika kutoa ushahidi aliweka wazi kuwa mara kadhaa, Diddy alimtishia kuposti video za ngono walizorekodi wakati alipokuwa akishiriki kufanya mapenzi na wanaume wengine. Na hii ni baada ya kugundua mrembo huyo ana mahusiano na Kid Cudi.
Sababu iliyopelekea kumfungulia kesi Diddy
Alieleza kuwa wakati alipoachana na Diddy mwaka 2018 alitaka kuandika kitabu kuhusu maisha na uzoefu wake alipokuwa kwenye uhusiano na nguli huyo wa Hip Hop Marekani.
Aliiambia mahakama kuwa alitaka Combs asome kitabu hicho kabla hajakitoa ili aelewe kile alichopitia kwenye mahusiano yao miaka 10. Ndipo akaamua kuwasiliana na Diddy kupitia wakili wake kuomba asome kitabu hicho na ampe fidia kwa yote aliyoyapitia.
Ventura aliweka wazi kuwa alitaka Diddy alipe dola 30 millioni ili apate haki ya kutumia kitabu chake. Hata hivyo baada ya madai kwamba Diddy hakujibu ombi hilo ndipo msanii huyo aliamua kufungua kesi Novemba 23,2024 akimtuhumu kwa kumhusisha na usafirishaji haramu wa binadamu, kumbaka, na kumfanyia ukatili wa kimwili.
Aidha baada ya sakata hilo kupamba moto kwenye mitandao ya kijamii wawili hao walifikia makubaliano ambapo kwa mujibu wa Ventura, Diddy alilipa dola 20 milioni kama fidia.
Diddy mwenye umri wa miaka 55, amekana mashtaka yote huku mawakili wake wamesema kwamba wale wanaodai kuwa waathiriwa wake akiwemo Ventura, walishiriki kwa hiari kufanya ngono na wanaume ambao walilipwa.
Hata hivyo Ventura anatarajiwa kurejea kizimbani leo Alhamisi Mei 15,2025 kwa ajili ya kuhojiwa na upande wa utetezi wa Diddy