Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ZRA yakusanya Sh238 bilioni ikivuka lengo makusanyo robo ya tatu

Muktasari:

  • Matumizi ya mifumo na uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuiwezesha mamlaka hiyo kufanya vizuri kwenye makusanyo

Unguja. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25, imekusanya Sh238.746 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 100.06 wa makadirio ya kodi kwa kipindi hicho ambayo yalikuwa ni Sh238.611 bilioni.

Taarifa iliyotolewa jana Aprili 3, 2025 kwa vyombo vya habari na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Said Kiondo Athumani imeeleza kuwa makusanyo hayo ni kuanzia Januari hadi Machi 2025.

Kwa mujibu wa Kiondo, makusanyo hayo ni ukuaji wa asilimia 14.9, sawa na ongezeko la Sh31.090 bilioni ikilinganishwa na makusanyo halisi kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2023/24, ambapo walikusanya Sh207.715 bilioni.

“Kwa Januari mwaka 2024/25, makisio yalikuwa Sh80.984 bilioni na makusanyo halisi yalikuwa Sh81.512 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 100.65, ikiwa ni ongezeko la Sh11.332 bilioni na sawa na ukuaji wa asilimia 16.15,” amesema.

Kwa Februari, makadirio yalikuwa Sh83.229 bilioni lakini makusanyo halisi ni Sh83.483 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 100.30 ikiwa ni ongezeko la Sh10.558 bilioni na ukuaji wa asilimia 14.48.

Katika taarifa yake, Machi 2025 makisio yalikuwa ni Sh74.397 bilioni ambapo makusanyo halisi ni Sh73.750 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 99.15.

Akizungumzia sababu za kufanya vizuri, Kiondo amesema ni kuimarika na kustawi wa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, zinazotokana na sera na uongozi imara wa viongozi wakuu wa nchi ambazo zimeimarisha biashara.

Pia, uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi Zanzibar unaotokana na utekelezaji wa sera nzuri za kiuchumi za Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Sababu nyingine alisema ni kuimarishwa kwa programu mbalimbali za elimu kwa walipakodi ili kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari, kuimarika kwa matumizi sahihi ya mifumo katika usimamizi wa kodi ikiwemo mfumo wa risiti za kielektroniki (VFMS) na matumizi ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa ZIDRAS.

Hata hivyo, Kiondo amesema kuongezeka kwa ufuatiliaji wa karibu wa walipakodi katika maeneo mbalimbali ya biashara kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za kikodi kwa walipakodi na jamii kwa ujumla.

Katika kuongeza makusanyo, kwa mujibu wa Kiondo, ZRA imepanga kuendeleza programu mbalimbali za elimu kwa walipakodi wa makundi mbalimbali ili kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari.

Hivi Karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya na maofisa wa mamlaka hiyo walianzisha operesheni maalumu kwa wafanyabiashara ambapo walibaini baadhi yao walikuwa wakikwepa kodi kwa kutotoa risiti za kielektroniki.

Wafanyabiashara wengine huwaambia wateja iwapo akitaka risiti ya kielektroniki akitaka risiti bei ya bidhaa itakuwa kubwa na asipochukua inapungua.

Kupitia hali hiyo, Dk Saada amesema watahakikisha wanalishughulikia jambo hilo na kila mmoja alipe kodi kulingana na anachostahili, kwa ajili ya maendeleo ya nchi.