Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar yawataka wananchi kuwa makini na matumizi ya maji

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa akizindua mradi wa ufundishaji wa fani ya maji kwa ajili ya taasisi binafsi na Serikali unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia(Kist) na Taasisi ya Ausbildungsverbund Teltow( AVT).

Muktasari:

  • Waziri Lela amesema kuanzishwa kwa mradi wa ufundishaji wa fani ya maji kwa ajili ya taasisi binafsi na Serikali utasaidia kudhibiti maji yasipotee kiholela.

Unguja. Katika kukabiliana na uhaba wa maji kisiwani Zanzibar, wananchi wametakiwa kuwa makini katika matumizi ya maji ili kudhibiti upotevu wa rasilimali hiyo muhimu, kwani tone moja lina thamani kubwa katika maisha ya binadamu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa amesema hayo leo Jumatano Aprili 9, 2025 wakati akizindua mradi wa ufundishaji wa fani ya maji kwa taasisi binafsi na Serikali, uliofanywa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume (KIST) na Taasisi ya Ausbildungsverbund Teltow (AVT) kutoka Ujerumani.

Lela amesema mradi huo utasaidia Zanzibar kutoa wataalamu ambao watatumia teknolojia kudhibiti upotevu wa maji, na kuongeza kuwa maji yaliyopo kisiwani humo bado ni haba na hayatoshelezi mahitaji ya kila siku.

Amewahimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji ili kuepusha upotevu wa maji safi na majitaka.

“Dunia ya sasa inakwenda kwa kasi zaidi katika matumizi ya teknolojia, na mradi huu utasaidia kuhakikisha maji yanapatikana kwa urahisi hasa katika viwanda, hoteli na familia, hivyo kuondoa migogoro inayosababishwa na changamoto ya maji,” amesema Waziri Lela.

Aidha, ametahadharisha Taasisi ya KIST kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi ili vijana wapate mafunzo bora na ya vitendo, hivyo  kusaidia katika maendeleo ya Zanzibar.

Waziri Lela amesisitiza umuhimu wa sayansi na teknolojia katika kufanikisha sera za maendeleo ya viwanda, uchumi wa buluu na ukuaji wa teknolojia.

Pia, ametoa wito kwa wamiliki wa hoteli kuwapa nafasi wataalamu hao ili kuendeleza utaalamu wao kivitendo, hasa katika usafi wa maji na majitaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya KIST, Dk Mahmoud Alawi amesema mradi huo utasimamiwa na Idara ya Ujenzi na Usafirishaji, na kwamba taasisi hiyo ina mikakati ya kutoa mafunzo ya stashahada kuhusu masuala ya maji, ambapo ifikapo mwaka 2026/27 wataanza kuchukua wanafunzi katika fani hiyo.

Meneja wa mradi kutoka Taasisi ya AVT, Hans Allgaier, ameeleza kuwa mradi utaanza mwaka huu na kumalizika mwaka 2027.

Amesema mradi huu utasaidia Zanzibar kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji, na kuwajengea vijana uwezo wa kutatua changamoto hiyo.

Meneja huyo amesisitiza pia umuhimu wa kuwa na miundombinu endelevu ya kuhifadhi na kudhibiti maji safi na majitaka, hasa kutokana na ongezeko la watalii kisiwani Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Khamis Abdalla Said amesema Zanzibar inafanya mageuzi katika sekta ya elimu kwa kuzingatia ufundishaji wa vitendo, na mradi huu ni moja ya hatua muhimu katika mageuzi hayo.