Z’bar yaainisha maeneo manne ya kimkakati Mpango wa Maendeleo 2026/27
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akil
Muktasari:
- Maeneo hayo ni kuimarisha mageuzi ya kiuchumi, miundombinu wezeshi, kukuza uwezo wa watu na maendeleo ya jamii na kuimarisha utawala bora na uhimilivu.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeainisha maeneo manne makuu ya kimkakati yatakayoongoza utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2026/27, huku ikitarajia kutumia Sh5.778 trilioni katika utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Maeneo hayo ni kuimarisha mageuzi ya kiuchumi, kuboresha miundombinu wezeshi, kukuza uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, pamoja na kuimarisha utawala bora na uhimilivu.
Akizungumza leo Juni 11, 2026 katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Unguja, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil, amesema kati ya fedha hizo, Sh4.433 trilioni sawa na asilimia 76.72 zitatokana na mapato ya ndani, huku Sh1.345 trilioni sawa na asilimia 23.28 zikitokana na ruzuku na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Amesema fedha hizo zinatarajiwa kugharamia utekelezaji wa programu 38 na miradi 54 ya maendeleo.
“Kiasi hiki ni ongezeko la asilimia 27.30 ikilinganishwa na bajeti ya maendeleo ya mwaka 2025/26 iliyokuwa Sh4.539 trilioni,” amesema Dk Malik.
Kwa mujibu wa makadirio ya awali, uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.5 mwaka 2026 kutoka asilimia 7.0 mwaka 2025.
Amesema Serikali itaendelea kutekeleza sera na mikakati ya kuendeleza miundombinu ya bahari kuu, viwanda vya kuchakata mazao ya baharini pamoja na kukuza utalii wa bahari na visiwa.
Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha kilimo cha biashara, usalama wa chakula na kuwezesha upatikanaji wa ajira katika sekta ya umma na binafsi, ambapo jumla ya Sh669.94 bilioni zinatarajiwa kutumika.
Dk Malik amesema ongezeko la idadi ya watu Zanzibar linaifanya Serikali kuhitaji takwimu sahihi zaidi ili kuwezesha upangaji bora wa mipango ya maendeleo.
Kwa mwaka 2026/27, Serikali imepanga kutumia Sh3.797 trilioni, sawa na asilimia 65.71 ya bajeti ya maendeleo, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati, huku Sh1.381 trilioni zikielekezwa katika miradi mingine, ikiwemo ile ambayo haijakamilika katika mwaka wa fedha 2025/26.
Pia, Sh600 bilioni zimetengwa kwa ajili ya Mfuko wa Ulipaji wa Madeni ya Miradi ya Maendeleo.
Katika kuboresha huduma za jamii, Serikali inatarajia kutumia Sh1.275 trilioni kuimarisha miundombinu na huduma za afya, elimu, michezo na mifumo ya hifadhi ya jamii.
“Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na upatikanaji wa haki ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu na amani, sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dk Malik.
Ameongeza kuwa Sh216.95 bilioni zinatarajiwa kutumika katika sekta za ulinzi, usalama, haki na mazingira.
Ukuaji wa uchumi
Akieleza sababu zinazotarajiwa kuchangia ukuaji wa uchumi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2026, Dk Malik amesema ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii kwa asilimia 9.3, kutoka watalii 917,167 mwaka 2025 hadi watalii 1,002,917 mwaka 2026.
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa barabara za mjini na vijijini, viwanja vya ndege na bandari.
Pia, amesema ukuaji huo utachangiwa na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na usimamizi mzuri wa matumizi ya umma.
Kwa mujibu wake, matarajio hayo yanategemea kuendelea kuimarika kwa sera za kifedha, upatikanaji wa nishati ya mafuta na gesi kwa gharama nafuu, pamoja na ongezeko la uwekezaji katika sekta ya viwanda ili kuongeza thamani ya bidhaa kwa matumizi ya ndani na mauzo ya nje.
“Pia, tunategemea kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na usalama nchini na katika nchi jirani,” amesema.
Hata hivyo, Dk Malik ameonya kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi inaweza kuwa chini ya asilimia 7.5 endapo migogoro ya kimataifa, ikiwemo mvutano unaohusisha Marekani, Israel na Iran, itaendelea kwa muda mrefu na kuathiri sekta muhimu kama utalii, usafirishaji, uwekezaji na biashara.
Amesema Serikali inapendekeza hatua madhubuti za kisera ili kudhibiti athari za mishtuko ya nje na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wa Zanzibar mwaka 2026.
Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha sera za fedha na bajeti, uthabiti wa sekta ya fedha, usimamizi wa sekta ya nje, kuongeza uzalishaji wa ndani, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa jamii.
“Kwa ujumla, utekelezaji madhubuti wa sera hizi utawezesha Zanzibar kupunguza athari za mishtuko ya nje, kuimarisha uthabiti wa uchumi na kulinda matarajio ya ukuaji wa uchumi mwaka 2026 licha ya changamoto zinazoendelea katika uchumi wa dunia,” amesema.