Waziri Soraga: Tuna jukumu kutanua wigo kuacha utalii wa msimu

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhani Soraga akizungumza katika ufunguzi wa mkutano watatu wa ZSummit. Picha na Zuleikha Fatawi
Muktasari:
- Licha ya kutaka watalii wengi waongezeke kisiwani hapa, wanapaswa kuandaa mazingira mazuri ambayo yataweza kuwabeba wageni hao.
Unguja. Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhani Soraga amesema ili Zanzibar kuacha dhana ya utalii wa msimu lazima waandae matukio yatakayowafanya watalii kuendelea kubaki kutembelea kisiwani hapa.
Soraga amesema uwepo wa matukio ya aina hiyo itaongeza chachu ya watalii kubaki na kuacha dhana ya (high na low season katika utalii) kwani matukio haya yatajenga uzoefu wa kuendelea kuja kwa kipindi chote.
Soraga ameyasema hayo leo Alhamisi Februari 20, 2025 katika Mkutano wa ZSummit unaofanyika Unguja.
"Uwepo wa matukio kama sauti za busara, maonyesho ya utalii, Trace Music Awards na matukio mengine, hayo ndiyo yanayowafanya watalii kuendelea kuongezeka kisiwani hapa na kujionea vivutio vilivyopo," amesema Soraga.
Amesisitiza kupitia Tukio la Trace Music Awards linalotarajia kufanyika mwezi huu, wageni 3,000 wanatarajiwa kushiriki katika tamasha hilo.
Soraga amesema Zanzibar ina kila sababu ya kutanua wigo wa utalii ili kuwavutia watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Korea, India na China kwani bado watalii wa maeneo hayo siyo wengi kisiwani hapa.
Pia, amesema licha ya kutaka watalii wengi waongezeke kisiwani hapa, wanapaswa kuandaa mazingira mazuri ambayo yataweza kuwabeba wageni hao.
"Unaweza kuwa na wageni wengi ili usiwe na sehemu ya kuwalaza hivyo tunapaswa kuweka usawa baina ya uwekezaji na watalii kwani kadri ya wanavyoongezeka ndivyo inavyohitajika uwekezaji mkubwa zaidi ikiwemo makazi," amesema Soraga.
Amesema kawaida ya mkutano huo unawakutanisha pamoja wadau na wawekezaji wautalii kujadiliana kwa lengo la kuweka mazingira bora katika sekta hiyo.
Mkutano huo wa kibiashara umefanikiwa kuwaleta wadau wa biashara za utalii na kubadilishana mawazo, kutanua wigo wa mitandao yao ili kusukuma mbele utalii wa visiwa hivi.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwapongeza waandaaji wa mkutano huo unaochangia ongezeko kubwa la uingiaji wa wageni kisiwani hapa.
Mkurugenzi wa wa Kampuni ya Kilifair Promotion Limited ambao ndio waandaaji wa mkutano huo, Dominic Shoo amesema huo ni mkutano wa tatu kufanyika kisiwani hapa.
Amesema katika mkutano huo zipo kampuni zaidi ya 150 ambazo zinatangaza biashara zao na washiriki 300 kutoka nchi 25.
Pia, amesema baada ya kumalizika mkutano huo kisiwani hapa uliondaliwa kwa siku mbili wafanyabiashara hao wataelekea kisiwani Pemba kuangalia soko la bidhaa zao.
"Mkutano huu umekuja na matazamio ya kukifungua kisiwa cha Pemba hivyo wadau hao baada ya kumaliza hapa watakuwa kisiwani huko kuuza bidhaa zao," amesema Shoo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Hoteli Zanzibar (Zati), Suleiman Mohammed amesema Jumuiya hiyo kwa lengo la kuunganisha taasisi binafsi kutoa mchango katika sekta ya utalii.
Amesema utalii endelevu ni msingi kutengeneza nguzo imara ya utalii kisiwani hapa kasa katika utalii wa utamaduni kwani na michezo kwani lengo kuu la kukitangaza kisiwa hichi.
Amesema kupitia mkutano huo, wadau wa utlii waliofika hapo wataibua fursa mpya ambazo zitawavutia watalii wengine kuja kutembelea Zanzibar.