Waziri ataka ushirikiano sekta ya elimu Zanzibar

Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Zanzibar, Leila Muhamed Mussa (kulia) akimkabidhi kitendea kazi mwenyekiti mpya bodi ya ushauri ofisi ya mkaguzi mkuu wa elimu, Hussein Ali Suleiman. Picha Muhammed Khamis
Muktasari:
- Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa amesema, ushirikiano kwa watendaji ndio msingi imara wa kuleta mageuzi yaliyo imara katika sekta ya elimu.
Unguja. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa, amewahimiza watendaji wa taasisi za wizara ya elimu kuwa na ushirikiano ili kuleta ufanisi katika kazi zao.
Amesema hayo leo Novemba 10 wakati wa kikao cha kumkaribisha Mwenyekiti mpya wa bodi ya Ushauri ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu Zanzibar, Hussein Ali Suleiman anayechukua nafasi ya Dk Ali Makame Ussi.
Amesema, kuwepo kwa ushirikiano kwa watendaji ndio msingi imara wa kuleta mageuzi yaliyo imara katika sekta ya Elimu.
Aidha, amesema, wizara ya elimu bado ina kazi kubwa ya kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuboresha sekta ya elimu katika kuimarisha ufaulu wa wanafunzi wa Zanzibar.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya hiyo, Khamis Abdulla Said, amesema wapo wapo tayari kutoa ushirikiano ya karibu na mwenyekiti huyo mpya wa bodi ya ushauri ili lengo liweze kufikiwa.
Amemuomba mwenyekiti mpya kuwasimamia walimu kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kuimarisha mageuzi ya Elimu
Akizungumza awali, Dk Ali Makame Ussi ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), amemuomba mwenyekiti kiti mpya kuweka kitengo cha ukaguzi wa ndani na kitengo cha ununuzi ili kurahisisha utendaji kazi.
Naye Mwenyekiti mpya Hussein Ali Suleiman ameahidi kutumikia nafasi hiyo kwa kutoa mashirikia na Wizara ili kuweza kuleta Maendeleo ya kielimu nchini.