Wawekezaji 500 wa biashara kukutana Zanzibar
Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tamasha la kimataifa la uwekezaji Zanzibar 2026.
Muktasari:
- Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2026 linatarajiwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Unguja. Zaidi ya wawekezaji na wafanyabiashara 500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kukutana Zanzibar kushiriki Tamasha la Kimataifa la Uwekezaji Zanzibar 2026 litakalofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 Juni 2026 katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar Airport.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 24, 2026, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff alisema tamasha hilo litawakutanisha pia watunga sera, washirika wa maendeleo na wanadiaspora kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
"Tamasha hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kufungua fursa za uwekezaji na kuharakisha mageuzi ya uchumi wa Zanzibar kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu," amesema.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, tamasha la mwaka huu linaongozwa na kaulimbiu isemayo Promoting Investment Diversification for Sustainable Development in Zanzibar: Shaping Zanzibar’s Next Growth Story inayolenga kupanua wigo wa uwekezaji na kukuza uchumi jumuishi.
Aidha, alibainisha kuwa tamasha hilo litafunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, hatua inayoonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi.
Akifafanua zaidi, Waziri Shariff amesema washiriki wa tamasha hilo watapata fursa ya kutembelea maeneo ya kimkakati ya uwekezaji, kushiriki maonesho ya miradi mbalimbali pamoja na kuhudhuria majadiliano ya kiwango cha juu yatakayowakutanisha wadau wa sekta mbalimbali za uchumi.
Ameongezea kuwa kutakuwepo pia madarasa maalumu ya uwekezaji, mikutano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na Serikali (B2B na B2G), pamoja na kikao maalum cha wanadiaspora kitakacholenga kuimarisha ushiriki wao katika maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar.
Vilevile, tamasha hilo litahitimishwa kwa hafla ya chakula cha jioni kitakachoyofanyika katika Hoteli ya Diamonds Bijoux Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo wawekezaji bora wa mwaka 2025 watatambuliwa na kupewa tuzo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imetangaza shindano la kubuni nembo rasmi ya tamasha hilo, ambapo mshindi atazawadiwa Sh2 milioni kutambuliwa rasmi na mwisho wa kuwasilisha kazi hizo ni Mei 15, 2026.
Pia, ametoa wito kwa wawekezaji, wafanyabiashara, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tamasha hilo, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu ya kukuza uchumi na kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika ramani ya uwekezaji duniani.