Mamcu yajitosa usafirishaji wa mizigo, yazindua mradi wa Sh1.2 bilioni
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya (wa pili kulia) akimkabidhi mfano wa ufunguo Mwenyekiti wa Chama cha MAMCU, Azamu Julajula.
Muktasari:
- Mamcu inaundwa na vyama vya msingi 210 kutoka wilaya za Mtwara, Masasi na Nanyumbu, ambavyo vinatarajiwa kunufaika moja kwa moja na mradi huo, hususan katika kupunguza gharama za usafirishaji ambazo hapo awali zilikuwa kubwa na wakati mwingine kukwamishwa na uhaba wa magari.
Mtwara. Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao (Mamcu) kinachohudumia wakulima wa wilaya za Mtwara, Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara, kimezindua mradi wa magari ya kubebea mizigo wenye thamani ya Sh1.2 bilioni.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mazao na kuinua mapato ya chama pamoja na wanachama wake.
Magari hayo matano yana uwezo wa kubeba wastani wa tani 30 kila moja, sawa na jumla ya tani 150 kwa safari moja, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda maghalani na masokoni.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo, Alhamisi, Aprili 23, 2026, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, ambaye amesisitiza umuhimu wa uwekezaji huo katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima.
Mwaipaya ametaka kuwepo kwa usimamizi madhubuti wa mradi huo, akieleza kuwa mafanikio yake yatategemea uwajibikaji, uadilifu na matumizi sahihi ya rasilimali hizo ambazo ni mali ya wakulima.
Aidha, ameonya dhidi ya uzembe na ubadhirifu, akisisitiza kuwa magari hayo yanapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha yanawanufaisha wakulima na kuongeza mapato ya chama.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya akiwa anafanya majaribio ya kuendesha moja ya magari hayo matano yaliyonunuliwa na chama cha MAMCU
“Ni muhimu kuhakikisha magari haya yanasimamiwa kwa weledi na uwazi; yasigeuzwe kuwa mali binafsi ya wachache, bali yawe chombo cha kuwaletea maendeleo wakulima wote,” amesema Mwaipaya.
Mamcu inaundwa na vyama vya msingi 210 kutoka wilaya za Mtwara, Masasi na Nanyumbu, ambavyo vinatarajiwa kunufaika moja kwa moja na mradi huo, hususan katika kupunguza gharama za usafirishaji ambazo hapo awali zilikuwa kubwa na wakati mwingine kukwamishwa na uhaba wa magari.
Mbali na kupunguza gharama, mradi huo unatarajiwa kupunguza muda wa kusafirisha mazao kutoka mashambani hadi maghalani na masokoni kutoka wastani wa siku mbili hadi chini ya saa 12, jambo litakalosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Mwenyekiti wa Mamcu, Azamu Julajula, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa chama hicho wa kuboresha huduma kwa wakulima na kuongeza thamani ya mazao yao.
Ameongeza kuwa Mamcu inaendelea kutekeleza miradi mingine, ikiwemo ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 5,000 za mazao, pamoja na mipango ya kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ili kuongeza thamani kabla ya kuuzwa.
Baadhi ya wakulima wamepongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa itasaidia kupunguza changamoto ya usafirishaji iliyokuwa ikiathiri uwezo wao wa kufikia masoko yenye bei nzuri.
Mkulima kutoka Masasi, Amir Juma, amesema hapo awali walikumbana na gharama kubwa za usafirishaji na ucheleweshaji wa mazao kufika sokoni kwa wakati.
“Tulikuwa tunapata hasara kutokana na gharama kubwa za usafiri na kuchelewa kufikisha mazao sokoni kwa wakati; magari haya yatatusaidia kuongeza kipato chetu,” amesema.
Kwa upande wake, Jamali Michael wa Nanyumbu amesema mradi huo unaonesha mafanikio ya mfumo wa ushirika na mchango wake katika maendeleo ya wakulima.
“Hili ni jambo kubwa kwetu; linaonesha nguvu ya ushirika na ni mfano wa mageuzi ya kimaendeleo yanayopaswa kuigwa,” amesema.