Wanolewa kuhusu hedhi salama Zanzibar

Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea kupatiwa mafunzo juu ya namna bora ya hedhi salama. Picha ha Muhammed Khamis
Muktasari:
- Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetoa elimu kuhusu hedhi salama kwa wanafunzi ili kuhakikisha hawakosi masomo pindi wawapo katika hedhi, jambo ambalo litaongeza ufaulu.
Unguja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema uelewa juu ya hedhi salama kwa wanafunzi mashuleni, ni muhimu kwani itawaongezea wanafunzi wa kike kujiamini na ufaulu.
Hayo yamesemwa leo Novemba 28,2023 na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari wa wizara hiyo, Mfaume Jaffar Mfaume wakati akifunga mafunzo juu ya uhifadhi wa hedhi salama, Mjini Unguja.
Amesema kuwasaidia watoto wa kike kunahitaji ushirikiano wa hali ya juu ili wasiweze kukwama katika dhamira ya kutimiza ndoto zao.
Amesema kila mmoja ni msimamizi wa suala zima la elimu, hivyo kushirikiana na kuwasaidia watoto wa kike kutaongeza ufaulu.
“Bado elimu inahitajika kuwapa taaluma watoto wakati wa uhifadhi wa hedhi salama kwani tathmini zinaonyesha kuna asilimia ndogo ya wasichana wanaofahamu juu ya jambo hilo. Hivyo kutoa elimu juu ya hedhi salama, kutawasaidia kujiskia huru kwenda shule kipindi cha hedhi.
"Tumekua na kundi kubwa la watoto wa kike baadhi ya maeneo wanashindwa kuhudhuria shuleni kipindi chote cha hedhi na kukosa masomo muhimu,”amesema.
Kwa upande wa Radhia Bakari kutoka Jumuiya ya Wajamama Foundation, ambaye ndiye alikuwa mtoa mada, amesema elimu kuhusu masuala ya uhifadhi wa hedhi salama shuleni, kunawapa watoto wa kike ufahamu juu ya jambo hilo.
“Wengi hukosa masomo kwa kukosa elimu sahihi ya kujistiri wakihofia kuchafua nguo na kuchekwa na wenzao, hivyo kutohudhuria masomo kipindi chote cha hedhi,”amesema Radhia.