Waliopitiwa mradi wa bandari Mangapwani kulipwa fidia

Rais Wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi
Muktasari:
- Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 24, 2023 alipozungumza na wananchi wa Bumbwini Misufini, Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa nyumba za fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo.
Unguja. Serikali ya Zanzibar, imeahidi kuwalipa fidia ya vipando na majengo wananchi wa Bumbwini waliopitiwa na mradi wa barabara na ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, Unguja Zanzibar.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 24, 2023 alipozungumza na wananchi wa Bumbwini Misufini, Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa nyumba za fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo.
Bila kutaja kiwango cha fidia kitakachotolewa, Dk Mwinyi amesema tayari kazi ya ulipaji wa fidia kwa baadhi ya wananchi hao limeanza kwa wakazi wa Mangapwani na baadaye watamalizia katika vijiji vingine.
“Kwa wale wote wanaostahili kulipwa fidia iwe ya vipando au majengo, tunahakikisha fidia zenu mtalipwa nyote kwa kipidi kifupi,” amesema Dk Mwinyi
Pia, Dk Mwinyi amewashauri viongozi wa jimbo hilo, kamati inayosimamia ujenzi huo, kushirikiana na mkandarasi wa mradi wa nyumba za wananchi zinazoendelea kujengwa kwenye maeneo ya Mwembemdema na Mangapwani kwa kuangalia mahitaji halisi ya aina ya nyumba wananchi watakazoridhika nazo.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Dk Khalid Salum Muhamed amesema hatua za ujenzi wa awali wa nyumba hizo zitasaidia kuboresha mwendelezo wa nyumba zitakazofuata kwa kuepuka changamoto zilizojitokeza baada ya kukamilika nyumba mbili za mwanzo.
Mbali na fidia za mazao na nyumba, Dk Khalid amesema pia wananchi waliopoteza maeneo yao, vikiwemo viwanja, tayari Serikali imeunda kamati inayojumuisha wataalamu wa ardhi na wanasheria kulishighulikia suala hilo ili kukamilisha ahadi ya Serikali ya kulipwa.
Naye, Mkandarasi wa ujenzi wa nyumba hizo kampuni ya Orkun kutoka Uturuki, IIhan Karadeniz imeiahidi Serikali kufanya maboresho kwa mujibu ya maelekezo wanayokubaliana.
Nyumba 370 zinatarajiwa kujengwa kwa ajili ya wananchi wa maeneo ya Bumbwini Misufini na Mangapwani ikiwa ni sehemu ya fidia yao watakayopewa na Serikali baada ya kupisha miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara na ujenzi wa bandari kubwa ya Mangapwani.
Pamoja na nyumba hizo, mradi huo unatarajia pia kujenga maduka ya biashara na shule ya maandalizi, miundombinu ya maji safi na maji taka, zikiwemo barabara za ndani ya eneo hilo za kiwango cha lami pamoja na mitaro ya maji machafu.