Rais Mwinyi aagiza wafanyabiashara kituo maalumu wasitozwe ushuru miezi mitatu

Muktasari:
- Rais Mwinyi aagiza wafanyabiashara kituo maalumu wasitozwe ushuru miezi mitatu
Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amezindua kituo maalumu cha wafanyabiashara na wajasiriamali na kuagiza waendeshe shughuli zao bila kulipa ushuru kwa miezi mitatu.
Kituo hicho cha wafanyabiashara na wajasiriamali Mtule, kimegharimu Sh4.16 bilioni hadi kukamilika, kinajumuisha biashara za mbao, karakana, wachoma vyuma, gereji za magari, maduka ya bidhaa mbalimbali na wajasiriamali wa kuchora hina na piko, kina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 300 kwa kwa eneo moja.
Ahueni hiyo ameitoa akiwa ziarani mkoani humo jana Oktoba 25, 2023 baada ya kuzindua kituo maalumu cha wafanyabiashara na wajasiriamali eneo la Kitogani kijiji cha Mtule, Wilaya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika mwendelezo wa ziara zake za kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo nchi nzima ikiwa ni shamrashamra za miaka mitatu ya uongozi wake.
"Mtafanya biashara zenu kwa miezi mitatu bila kutozwa ushuru, kwahiyo fanyeni biashara zenu kwa uhuru," amesema Dk Mwinyi.
Pia, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kusini kutowawekea kodi kubwa wajasiriamali wa eneo hilo ili kuwapunguzia mzigo mkubwa wa gharama za maisha na kuwapa wepesi wa kufanyabiashara zao kwa utulivu ili kukidhi haja ya biashara zao.
Pia aliitaka halmashauri hiyo kuyatunza na kuyadumisha kwa kuyakarabati majengo hayo yatakapoanza kuchakaa.
Katika hatua nyengine Rais Dk Mwinyi amewataka wafanyabiashara waeneo hilo kudumisha usafi na kutenganisha biashara zao na maeneo ya barabara ili kuheshimu mipango ya miji iliyowekwa mkoani humo kwa kudumisha mwonekano mzuri wa Zanzibar.
Kadhalika, Rais Dk Mwinyi aliitaka Halmashauri ya wilaya ya Kusini kutengeneza vyanzo zaidi vya mapato ili kuwapa uwezo wa kuendeleza miradi ya maendeleo.
Akiwa ziarani Kijiji cha Jozani wakati akiweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa barabara inayounganisha vijiji vinne vya Jozani, Ukongoroni, Charawe hadi Bwejuu, Rais Mwinyi aliiagiza Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi kuwalipa fidia wananchi wote waliopisha ujenzi wa barabara hiyo kabla kumalizika kwa ujenzi huo.
Rais Mwinyi amewaahidi wakulima wa Mkoa Kusini Unguja kuwafikishia huduma za umeme mashambani ili wazalishe zaidi mboga mboga na matunda.
Alisema, Zanzibar inazaidi ya hoteli za utalii 600 zenye mahitaji mengi kutoka kwa wakulima wa ndani.
Dk Mwinyi amesema hakuna haja kwa Zanzibar kuagiza matunda na mboga mboga kutoka nje badala yake ameliagiza Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) kuwafikishia huduma ya umeme wakulima wote wa mkoa huo ili kuwapa fursa ya kutumia vyema rasilimali zilizomo kwenye vijiji vyao.
Katibu Mkuu wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Khadija Khamis Rajab, alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Jozani Charawe Ukongoroni na Bwejuu ni miongoni ujenzi wa barabara ndefu za kikomita 42.5 ambapo barabara hiyo itakua na urefu wa kilomita 23.3 hadi kukamilika kwake.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amesema mkoa unaendelea kutawaliwa kwa amani na utulivu wa wananchi na kupongeza juhudi za Rais Mwinyi kwa kuendelea kuwaekea wananchi wa mkoa huo eneo maalumu la wajasiriamali ili kukuza vipato vyao.
Pia, amesema kuna maendeleo mengine ya huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa barabara za kisasa zilizounganisha vijiji vya mkoa huo, huduma bora za afya zinazotolewa na hospitali ya kisasa ya Kitogani, shule za kisasa na maji safi.