Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyabiashara Michakaini walia kukosa wateja, waiangukia Serikali

Hiki ndio kituo cha wajasiriamali Chakechake ambacho wameomba kuwekwa kituo cha daladala ili kupanua wigo wa upatikanaji wa wateja

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa Soko la Michakaini halijazoeleka, mazingira yanapaswa kuboreshwa ili kuwavutia wananchi kuja kufanya ununuzi hapa

Pemba. Wafanyabiashara wa Soko la Michakaini, Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba, wameiomba Serikali kuwasaidia kutafuta njia mbadala itakayowezesha kuongeza idadi ya wateja ili kukuza mitaji yao.

Wakizungumza leo Jumapili, Aprili 27, 2025, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya alipotembelea sokoni hapo, wafanyabiashara hao wamelalamikia mzunguko mdogo wa fedha kutokana na uchache wa wateja, wakieleza kuwa umbali wa soko hilo kutoka makazi ya watu nayo ni changamoto kubwa.

Juma Bikso William, mmoja wa wafanyabiashara  hao, amesema ili kupunguza changamoto hiyo, mamlaka zinapaswa kuweka kituo cha daladala karibu na soko hilo ili kuongeza upatikanaji wa wateja.

“Kwa kuwa hakuna kituo cha daladala hapa karibu, inakuwa vigumu kwa watu kufika sokoni. Serikali itusaidie kwa kutuwekea kituo cha daladala au bajaji ili kurahisisha huduma za usafiri na kuongeza mzunguko wa wateja,” amesema Juma.

Mfanyabiashara Ali Bakari amesema bila hatua za haraka, mitaji yao iko hatarini kupotea kutokana na biashara kudorora.

“Soko hili halijazoeleka na bado liko mbali, hivyo mazingira yanapaswa kuboreshwa ili kuwavutia wananchi kuja kufanya ununuzi hapa,” amesema.

Ibrahim Ali, mmoja wa wateja wa soko hilo, amesema umbali wa soko kutoka mjini unasababisha gharama kubwa za usafiri kwa wateja, hali inayowafanya wengi wao kusita kufika sokoni hapo.

“Kutoka mjini hadi Michakaini tunalipa nauli mara mbili, jambo linalotuongezea gharama. Kama Serikali itaweka kituo cha daladala, naamini itarahisisha huduma na kuvutia wateja wengi zaidi,” amesema Ibrahim.

Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya amesema Serikali tayari imeanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na Baraza la Manispaa ili kuanzisha kituo kidogo cha daladala karibu na soko hilo.

“Tunatambua changamoto hii na tunaendelea kushirikiana na Baraza la Manispaa kuhakikisha kituo cha daladala kinaanzishwa ili kusaidia kuleta abiria karibu na soko,” amesema.