Wachekelea biashara ya bodaboda kurasimishwa Pemba

Baadhi ya vijana ambao ni waendesha boda boda wakisubiri abiria katika moja ya eneo la mji wa chakechake Pemba. Picha na Muhammed Khamis
Muktasari:
- Wamesema kurasimishwa pikipiki (bodaboda) na bajaj kuwa vyombo vinavyotumika kutoa huduma ya usafiri kisiwani Pemba, kumenusuru kundi kubwa la vijana kujingiza matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya.
Pemba. Wakati Serikali na mamlaka zake zikiendelea kuhubiri kuhusu umuhimu wa nguvu kazi za vijana katika kukuza maendeo ya nchi inaelezwa kuwa kisiwani Pemba kwenye idadi ya watu wapatao 280,584 kwa mujibu wa idadi ya sensa ya watu na makaazi 2022 vijana wapatao 1,393 wamenusurika na wimbi la uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya.
Wakizungumza na Mwananchi Digital kisiwani Pemba vijana hao wamedai kuwa kunusurika kwao na wimbi hilo kumetokana na kujihusisha na utoaji wa huduma za usafiri wa bodaboda na bajaj.
Ali Othman kutoka Shehia ya Wara Chakechake, Pemba amesema kuanza kwake kutoa huduma ya usafiri kumenusuru kwa kiasi kikubwa maana kuna wakati kabla ya kuanza kazi hiyo alikua tayari ameanza kuvuta sigara na wakati mwengine hata kutumia bangi kwa sababu aina ya marafiki aliokua nao kijiweni.
‘’Hivi sasa sipati muda kabisa wa kukaa mtaani kwetu muda mwingi niko barabarani muda wa kurudi nyumbani ni usiku na huwa nimechoka sana sina tena muda wa kukaa maskani mwezi wa sita sasa,’’amesema.
Naye Abdalla Nassir kutoka Chanjamjawiri amesema amekuwa dereva wa bodaboda kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja na nusu na alianza kazi hiyo akiwa kama dereva aliepewa pikipiki kwa mkataba lakini hivi sasa tayari anamiliki pikipiki yake na pia anaendesha familia kwa kazi hiyo hiyo.
Mwatima Abdalla ni mama watoto wawili ambaye mume wake ni mtoa huduma ya usafiri wa pipiki amesema kwenye kipindi chote ambacho mume wake anafanya kazi hiyo kwa miaka miwili sasa hajawahi kukutana na changamoto yoyote ile ya kifamilia.
Amesema mume wake anafanya wajibu wa kutunza familia kwa wakati na kutekeleza majitaji yote kama mume, huku akiweka pia hakiba ya chakula na matumizi mengine nyumbani kwao.