Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti waibua changamoto zinazoukabili ushirika, Mwinyi ataka zishughulikiwe haraka

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Ushirika Online TV alipomwakilisha Rais Hussein Mwinyi katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya Ushirika duniani kwa Zanzibar yamefanyika Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.

Muktasari:

  • Kukosa elimu ya ushirika, vijana kudhani ni vikundi vya kujikopesha fedha na kukosa mifumo ni miongoni mwa changamoto zinazoukabili. Rais Mwinyi awaondolea hofu wanaushirika wa kukosa mitaji, akitaka Benki ya Ushirika Tanzania kuanzisha tawi lake Zanzibar na kutoa mikopo isiyokuwa na riba.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza mazungumzo na Benki ya Ushirika Tanzania ili itoe mikopo nafuu isiyo na riba kwa vikundi vya ushirika.

Amesema lengo ni kutaka kuondoa hofu ya upatikanaji wa mitaji kwenye biashara zao.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwezesha wananchi kiuchumi na kuimarisha sekta ya ushirika, ambayo imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kutoa ajira kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa kupitia hotuba yake iliyosomwa leo, Jumamosi Julai 5, 2025, na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk Mwinyi amesema utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji umebainisha changamoto kadhaa zinazoukabili ushirika Zanzibar, na ameagiza hatua za haraka zichukuliwe kuzitatua ili kuleta mabadiliko chanya.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni uelewa mdogo wa wanachama kuhusu misingi ya ushirika na haki zao, kasoro kwenye mifumo ya usajili na usimamizi, ukosefu wa takwimu sahihi, na mfumo dhaifu wa ufuatiliaji na tathmini.

Pia amesema ushiriki mdogo wa vyama vya ushirika katika sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara ndogo na za kati umetajwa kama kikwazo.

Aidha, Rais Mwinyi amehimiza mageuzi ya kisheria na kisera, ikiwamo kupitia upya Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya 2014, Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 15 ya 2018, na kanuni zake za 2019.

Ameagiza kuanzishwa kwa taasisi ya ukaguzi wa hesabu za vyama vya ushirika Zanzibar na mfumo wa kidijitali kwa ajili ya usajili na usimamizi.

"Hatupendi kuona tafiti zikibaki kwenye makabati. Zitekelezwe kwa vitendo kwa kuweka mikakati ya kweli ya kimageuzi," amesema, huku akiitaka wizara husika kushirikiana na Muungano wa Vyama vya Ushirika Zanzibar na wadau wengine kuhakikisha utekelezaji wa mapendekezo unafanyika kwa haraka.

Rais Mwinyi amesema Serikali imefanikiwa kuunganisha vyama 383 vya uzalishaji na Saccos ili kupata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.

Ameeleza kuwa kati ya Saccos 224 zilizosajiliwa, 78 zinafanya kazi vizuri na zimekusanya mtaji wa Sh21.876 bilioni na kutoa mikopo kwa wanachama 12,260.

Kwa upande wake, Katibu wa Muungano wa Vyama vya Ushirika Zanzibar, Suleiman Ali Haji, amesema ushirika umekuwa mkombozi na kuwaondolea wananchi umaskini, akiomba Serikali kuupa kipaumbele, kuanzisha kamisheni ya ushirika na mfumo mpya wa usajili.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi, Uchumi na Uwekezaji), Shariff Ali Shariff, amesema Zanzibar imesajili vyama vya ushirika 7,779 na wizara itaendelea kushirikiana na wadau ili kuujengea uwezo zaidi.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya Ushirika Tanzania, Yahya Jumanne, amesema benki inahudumia vyama 3,400 na ina mpango wa kutoa mikopo kwa wakulima na wajasiriamali, huku asilimia 10 ya Sh5 bilioni zilizotolewa na Rais Samia ikiwa imewekezwa Zanzibar.

Naye mwakilishi wa Mfuko wa Pass, Osca Kimara, amesema mfuko umeweka dhamana za mikopo yenye jumla ya Sh2 trilioni na asilimia 50 ya walionufaika ni wanawake na 25 vijana, huku Sh1.8 bilioni zikitolewa Zanzibar kwenye sekta za ufugaji nyuki, samaki na uchumi wa buluu.