Ukuta wadondoka Forodhani, 10 wanusurukia kifo

Muktasari:
- Fundi mmoja aliyekuawa akiendelea na ukarabati wa majengo ya Mji Mkongwe Zanzibar amejeruhiwa baada ya kudondokewa na ukuta huku wenzake wakinusurika.
Unguja. Takribani mafundi 10 wamenusurika kifo na mmoja kujeruhiwa baada ya kudondokewa ukuta wakati wakiendelea na ukarabati wa moja ya majengo ya Mji Mkongwe, Zanzibar.
Tukio hilo limetokea majira ya mchana leo Januari 17, 2024 katika jengo ambalo lilikuwa linafanyiwa marekebisho karibu na Ngomwe Kongwe, Forodhani Zanzibar.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi Digital, Kamishna wa kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Rashid Mzee Abdallah amesema hakuna aliyepoteza maisha katika tukio hilo.
"Ndiyo ni kweli leo mchana ukuta wa jengo umeondoka, mafundi walikuwa wanagongagonga kwa ajili ya kupiga plasta," amesema.
Amesema mtu mmoja ndiye aliangukiwa na kifusi lakini wamewahi na kukiondoa kifusi juu yake, lakini amepata mikwaruzo na michubuko kadhaa na amepelekwa Hospitali ya Mnazimmoja.
Jengo hilo zamani la Kamisheni ya Ardhi na lilikuwa Makao Makuu ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).
Baadhi ya mafundi waliokuwa wanaendelea na ujenzi katika jengo hilo walisema upande huo wa nyuma ya jengo kulikuwa na nyufa kubwa.
Hassan Khalid amesema "sisi tulikuwa chini na huyu aliyeumia alikuwa juu, kwa hiyo ameshuka na ukuta lakini bahati nzuri hakufunikwa, bali aligandamizwa zaidi sehemu za miguuni."
Fundi mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema kabla ya ukuta huo kuanguka ulitoa ishara kwa hiyo wengi walikimbia.
Majengo mengi ya Mji Mkongwe yamekuwa yakidondoka kutoka na uchakavu wake.
Miaka ya karibuni Jengo la kihistoria la Beit-al-Ajaib lililopo mji Mkongwe lilianguka likiwa linafanyiwa ukarabati na kuathiri watu kadhaa, waliokuwa mafundi ujenzi.