Tafiti 112 kutoa mbinu mbadala kutathmini utahini wa umahiri

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania,(Necta).
Unguja. Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Said Ally Mohammed amesema tafiti 112 zimewasilishwa zinazotoa mbinu na njia mbadala ya kutathmini utahini wa umahiri.
Kati ya tafiti hizo, 63 zimeonekana kuwa bora zaidi na zitawasilishwa katika kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya baraza hilo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo leo Novemba 27, 2023 Mjini Unguja, Dk Said amesema maeneo ambayo wamejikita katika kufanya tathmini ni eneo la utahini na upimaji kwa kutumia teknolojia ikiwemo umahiri na usimamizi wa mitihani.
"Hizi tafiti zitasaidia kufanya tathmini kwa kutumia teknolojia, kwa hiyo utaona jinsi zilivyo muhimu," amesema Dk Mohammed.
Amesema miaka 50 ya baraza hilo limepata mafanikio makubwa ikiwemo kuanza upimaji wa umahiri na kupanua matumizi ya teknolojia ambalo limechangia kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi nchini.
Amesema changamoto inayowakabili na wamejipanga kupambana nayo ni udaganyifu unaotokea katika vyumba vya mitihani, mwaka jana katika matokeo ya darasa la saba walifungia vituo 25 na walifuta matokeo ya wanafunzi zaidi ya 2,000. Mwaka huu wamefungia vituo viwili na wametoa onyo vituo vitatu, kati ya hivyo wanafunzi 31 wamefutiwa mitihani na wamekiri kutenda kosa hilo.
"Baraza limejipanga kuondoa udanganyifu unaotokana na vituo vya elimu, ndio maana kuna utaratibu wa kufungiwa na kufuta matokeo hatutaki vyeti visivyoendana na ujuzi wa mtu,"amesema Dk Said.
Ametoa wito kwa jamii kuwa suala la mitihani si suala la baraza pekee, ni jambo la kila mmoja hivyo wanapaswa kushirikiana ili kutoa elimu bora na yenye tija.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa amesema tathmini si tu kuangalia matokeo ya mtu binafsi, badala yake kutathmini kwa kuangalia njia za kutumia walimu wanapopeleka maudhui kwa wanafanzi.
Amesema tathmini ni njia mojawapo ya kuitumia kwa mwanafunzi, ili kukuza ufanisi kwa kutoa matokeo chanya kwani hiyo itawasaidia kutoa mafunzo yenye ubora.
Amefafanua kuwa kongamano hilo limejumuisha wataalamu mbalimbali watakaojadiliana mbinu za tathmini ambazo zinaendana na karne ya 21, lengo ni kutoa ufanisi kwa wanafunzi nchini.
Pia, tafiti ambazo zitawasilishwa zitawarahisishia watunga sera kuona jinsi ya kutunga mitaala, kwani kwa sasa sekta ya elimu ipo katika mabadiliko makubwa.
"Tafiti zitakazowalishwa katika kongamano hili zitatupa nafasi watunga sera kuona jinsi kutunga mitaala yetu na kuiboresha, kwani kongamano hili limefanywa muda muafaka kwa kuwa wizara ipo katika mabadiliko yanayoendana na dunia," amesema Waziri Lela.
Kwa mujibu wa waziri huyo, wataalamu hao wametoa tafiti mbalimbali za kutathmini wanafunzi kwa kutumia njia za kidigitali badala ya kutumia njia za makaratasi, hivyo tafiti hizo zitatoa takwimu sahihi na taarifa za ukweli na uhakika ambazo zitaisaidia Serikali katika maamuzi.
Amebainisha tafiti hizo zinatoka maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar, Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika na wataalamu hao wataelezea hali ya tathmini katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuboresha upungufu ambao upo katika tathmini za ndani.
"Tathmini zote zitamuwezesha mwanafunzi kuwa na ujuzi wa kuishi katika karne ya 21 na hilo ndio lengo kuu la kuondoa mitihani ya darasa la nne, miaka michache ijayo tutaondoa mitihani ya kidato cha pili, mwanafunzi anatakiwa kutahiniwa kwa njia ambayo sio ya pepa," amesema Lela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzanian Central for Education, Yussuf Ogutu amesema wapo Zanzibar kufanya semina kwa ajili ya kuongeza ufaulu na kuwaandaa vijana katika mfumo wa umahiri.