Sh21 bilioni zawafikia wajasiriamali 20,000 Zanzibar

Rais Mwinyi akizungumza baada ya kuwaapisha wakuu wa Mikoa na Wilaya Ikulu Zanzibar leo Novemba 20, 2023.
Muktasari:
- Milango ya fursa zilizofunguliwa katika miaka mitatu ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi imewezesha pia kuwafikia zaidi ya Wazanzibar 20,000 kupitia mikopo ya Sh21.3 bilioni.
Dar es Salaam. Milango ya fursa iliyofunguliwa katika miaka mitatu ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi imewezesha pia kuwafikia zaidi ya wazanzibar 20,000 kupitia mikopo ya Sh21.3 bilioni.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 25, 2023 na Mkurugenzi wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea), Juma Burhan Mohammed wakati wa kampeni ya ‘Mkono Kwa Mkono’ katika mikoa mitano ya Zanzibar.
Kampeni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ikiwa ni siku ya 12 leo kabla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa ZBC, kampeni hiyo inazunguka katika mikoa yote na leo iko Mkoa wa Mjini Magharibi kwa lengo la kuibua fursa, mbinu na suluhisho la changamoto za wananchi.
“Hadi kufikia Oktoba 30, 2023 tulikuwa tumeshatoa Sh21.3 bilioni zilizofikia wanufaika 20,000, upande wa Mkoa wa Mjini Magharibi zimetoka Sh8 bilioni kusaidia wananchi kukuza uchumi wao,” amesema Mohammed.
Kwa mujibu wa wakala huo, baadhi ya majukumu yake ni kuwezesha wajasiriamali kwa kuwapa mikopo, mitaji, mafunzo ya fedha, uzalishaji unaozingatia ubora wa bidhaa na kuwasaidia kupata vyeti vya ubora wa bidhaa. Pia kuwaunganisha katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mohammed amesema wakala huo umegusa sekta tofauti kwa lengo la kuhakikisha kila fursa iliyofungwa inafunguliwa kwa wananchi kwa huduma ya kifedha, mafunzo au masoko.
Amesema lengo la kampeni hiyo ni kusaidia wazalishaji wa bidhaa za mikono na waagizaji kutoka nje kubadilisha mtazamo wa huduma zinazotolewa na wakala huo.
“Ukimpatia mtu pesa bila kuwa na elimu ya kuitumia ni sawa na kuitupa, tunataka mjasiriamali achukue pesa kwa manufaa yake na arejeshe ili wengine pia wapate,” amesema Mohammed.