Rais Mwinyi aalika wawekezaji viwanda, biashara kutoka China

Muktasari:
- Shirikisho la viwanda na biashara la China linahusisha kampuni kubwa na viwanda 700 wakiwemo wafanyabiashara wa madini, kampuni za vifaa vya ujenzi, teknolojia na kilimo.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewakaribisha Zanzibar wafanyabiashara wakubwa na wenye viwanda kutoka China.
Mwinyi amewakaribishwa wawekezaji hao leo Novemba 21, Ikulu mjini Unguja alipokuwa akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda na wafanyabiashara 15 kutoka China, Xu Lejiang.
Amewaeleza utalii hasa wa hoteli na maeneo ya kupumzikia una fursa nyingi za uwekezaji, kwani Zanzibar ina maeneo mazuri ya fukwe nyeupe zinazowavutia wageni na watalii wengi.
Kuhusu sekta ya uchumi wa buluu, Rais Mwinyi amewakaribisha wafanyabiashara hao kuangalia fursa eneo hilo, kwani Zanzibar mbali sekta ya utalii inayoingiza asilimia 30 ya pato la Taifa, uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya samaki ni sekta muhimu pia kwa uchumi wa nchi, hivyo alilitaka shirikisho hilo kutoka China kuangalia fursa za uwekezaji kwenye eneo hilo.
Akiizungumzia sekta ya mafuta na gesi, Rais Mwinyi pia amelitaka shirikisho hilo kuangalia pia eneo hilo kwa uwekezaji.
Naye, Xu Lejiang amemweleza Dk Mwinyi kwamba shirikisho hilo limeziweka pamoja zaidi ya kampuni kubwa na viwanda 700 wakiwemo wafanyabiashara wa madini, kampuni za vifaa vya ujenzi, teknolojia na kilimo.
Kiongozi huyo alimwahidi Rais Mwinyi kuwashawishi wafanyabiashara wengi zaidi kuja kuwekeza Zanzibar.